Jan 04, 2017 07:37 UTC
  • Sayansi na Teknolojia

Karibuni katika mjumuiko huu mpya wa vipindi ambavyo vinaangazia maendeleo mapya katika sekta za sayansi, teknolojia na tiba duniani na hasa nchini Iran. Karibuni kujiunga nasi ambapo leo tutaangazia mafanikio ya wanasayansi wa Iran katika kutengeneza chombo cha kutibu magonjwa ya ubongo kama vile Parkinson kati ya mengine. Karibu kujiunga nami hadi mwisho.

Wasomi na watafiti Wairani katika Chuo Kikuu cha Kiviwanda cha Amir Kabir wamefanikiwa kuunda chombo cha kuibua harakati katika ubongo kwa lengo la kutibu ugonjwa wa Parkinson. Kwa kifupi ni kuwa, ugonjwa wa Parkinson ni ugonjwa unaoathiri neva ya kati ya ubongo na kumfanya mgonjwa kutetemeka, kupungua kwa uwezo wa kutenda na kutembea kwa kuchechemea. Watu wenye ugonjwa wa Parkinson, taratibu hupoteza uwezo wa kudhibiti harakati za usogezaji wa mwili.

Watafiti hao kwa kushirikiana na Idara ya Sayansi na Teknolojia katika Ofisi ya Rais wa Iran walifanikiwa kuunda chombo cha kuibua harakati katika ubongo. Ujenzi wa chombo hicho umezingatia hitajio la watafiti kukiunganisha na kompyuta.

Ugonjwa wa Parkinson uligunduliwa kwa mara ya kwanza na Daktari wa Uingereza James Parkinson mwaka 1871 na ukaitwa baada yake na aghalabu huathiri wazee. Baadhi ya takwimu zinaonyesha kuwa duniani kote kuna watu karibu milioni 10 wanaokabiliwa na Parkinson na katika bara la Afrika kuna ongezeko la idadi ya watu wanaoripotiwa kuwa wanaishi na ugonjwa huo. Sababu ya kuharibika seli za ubongo na hivyo kuibuka Parkinson bado haijajulikana kikamilifu na pia hakuna tiba ila kuna mbinu mbali mbali za kuudhibiti na kuzuia athari zake kuwa mbaya kwa mgonjwa.

 

Parkinson ni ugonjwa unaoathiri neva ya kati ya ubongo

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za Shirika la Afya Duniani WHO, kati ya kila watu 100 walio juu ya umri wa miaka 60 mtu moja ana Parkinson. Aidha takwimu hizi zinaonyesha kuwa ni asilimia 10 tu ya wenye Parkinson ndio walio chini ya umri wa miaka 50. Inatabiriwa kuwa watu wanaougua Parkinson watafika takribani milioni 16 ifipakpo mwaka 2050.

Dalili za Parkinson huanza kujiri hatua kwa hatua ambapo viungo vya mwili hutukisika au kutetemeka hasa viganja vya mikono, sehemu za juu za mikono, miguu, taya na uso. Aidha wanaokumbwa na Parkinson huwa na mwendo wa polepole pamoja na matatizo ya kusimama na kuangukaanguka mara kwa mara. Aidha wenye Parkinson huwa  na sauti ya chini ya matamshi yasiyosikika inayoitwa hypohonia na pia hukumbwa na ugumu wa kumeza au kushindwa kumeza kwa kawaida hali ambayo yamkini husababishwa na kutokuwa na mate.

Kati ya dalili za Parkinson ni kutetemeka hasa viganja vya mkono

Hali hii humsababishia mgonjwa msononeko mkubwa.  Hizo ni baadhi tu ya dalili za Parkinson kwani kuna dalili nyingine nyingi ambazo hujiri katika mwili wa anayeugua. Kama tulivyosema bado wataalamu hawajaweza kubaini kwa yakini sababu ambazo hupelekea kuibuka ugonjwa wa Parkinson lakini pamoja na hayo, wataalamu wanaamini kuwa yamkini ugonjwa huu ukasababishwa na mazingria anaomoishi mtu na pia sababu za kijenetiki. Kwa hivyo kuna uhusiano wa moja kwa moja baina ya jenetiki za Parkinson lakini bado haijaweza kufahamika kwa yakini kuhusu nafasi ya urithishano katika kuibuka Parkinson.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliochapishwa katika semina za kitiba na majarida ya kisayansi mwaka 2007, kati ya sababu ambazo yamkini zikapelekea kuongezeka uwezekano wa kuibuka ugonjwa wa Parkinson ni mada za dawa za kuua wadudu au insecticides kuingia katika mwili kwa wingi, upungufu wa asidi ya foliki mwilini na kisukari aina ya pili.

Hali kadhalika wataalamu wanasema moja ya njia za kupunguza uwezekano wa kupata ugonjwa wa Parkinson ni kutumia mafuta yenye afya ambayo kwa Kiingireza hujulikana kama polyunsaturated au monounsaturated kama vile mafuta ya zeituni na mafuta ya canola badala ya siagi na mafuta mshabaha yaani saturated fats.

Oktoba mwaka 2016, Daktari Farzad Tauhid-Khow, mhadhiri wa uhandisi wa kitiba katika Chuo Kikuu cha Kiviwanda cha Amir Kabir mjini Tehran alitangaza habari ya kuundwa chombo cha kuibua harakati katika ubongo wakati wa kutibu ugonjwa wa Parkinson. Alisema chombo hicho, ambacho kwa lugha ya Kiingereza kinajulikana kama brain stimulator  transcranial direct current stimulation (tDCS) device,  kimeundwa na watafiti wa chuo hicho.

Kwa mujibu wa Daktari Tauhid-Khow, chuo hicho kimetengeneza sampuli mbili za chombo hicho kwa kuzingatia viwango vya kimataifa. Amesema chombo hicho kinaweza kuibua mawimbi ya DC au Direct Current kwa ajili ya kutumika katika utafiti. Chombo hicho huibua harakati katika ubongo na baada ya vikao kadhaa vya matibabu, mgonjwa huonyesha dalili za kuboreka.

Chombo hiki hadi sasa kinaundwa katika nchi za Uhispania, Ujerumani na Marekani pekee na gharama za kukitengeneza Iran ni asilimia 33 rahisi kuliko chombo kinachotengenezwa nje ya nchi ambacho hugharimu takribani dola 5,300. Hivi sasa wataalamu wako katika mkakati wa kutegeneza chombo hicho kwa wingi ili kukiuza hapa Iran na katika soko la kimataifa.

Wataifiti  Wairani wamefanikiwa kutegeneza rangi ya samawati ya Phthalocyanine yenye kustahamili joto la juu sana 

Mbali na mafanikio hayo, katika kipindi hicho cha mwezi Oktoba mwaka 2016, wataalamu wa Chuo Kikuu cha Zanjan kaskazini-magharibi mwa Tehran walifanikiwa kutengeneza nano za kiviwanda zenye rangi ya samawati yaani Phthalocyanine ambazo zinaweza kustahimili joto la juu sana. Mada hii inaweza kutumika kutengeneza rangi nyinginezo ambazo katika miaka ya nyuma Iran imekuwa ikiziagiza kutoka nchi kama vile China, India na Ujerumani. Hivi sasa Iran imeweza kuzalisha kwa wingi rangi ya samawati ya Phthalocyanine kwa ubora wa juu sana na rangi hii hutumika katika sekta ya utengenezaji magari, viwanda vya nguo, wino, sanaa za mikono, viwanda vya kemikali n.k.

Rangi ya samawati ya Phthalocyanine inayozalishwa Iran ni ya kiwango cha juu sana kwa matazamo wa uhalisia ikilinganishwa na zinginezo. Rangi hiyo iliyotengenezwa Iran inaweza kuvumilia kiwango cha nyuzi jote 250 katika hali ambayo rangi zinazotengenezwa nje ya Iran haziwezi kuvumilia kiwango nyuzi joto zaidi ya 200.

Hali kadhalika watafiti Wairani wamefanikiwa kuunda nano-catalyst kwa ajili ya maabara ambayo inaweza kusaidia katika utengenezaji dawa ya kukabiliana na saratani ya matiti na kwa bei nafuu. Moja ya sababu kuu za vifo baada ya maradhi ya moyo hasa katika nchi za kiviwanda ni saratani ambapo saratani iliyoenea sana ni saratani ya matiti. Kwa wastani katika kila wanawake 10 mmoja amewahi kuugua aina hii ya saratani. Kwa msingi huo utengenezaji wa mada mpya za kemikali katika kutibu saratani hii ni jambo lenye umuhimu mkubwa.

Watafiti Wairani wameunda nano-catalyst  ya kusaidia utegenezaji dawa za kutibu saratani ya matiti

Hali kadhalika kwa mara ya kwanza nchini Iran, kumetengenezwa dawa  ya kibiolojia yenye kutibu saratani ya kibofu na ambayo inaweza kudumu kwa muda mrefu. Tatizo la dawa zilizopo za kutibu saratani ya kibofu ni kuwa haziwezi kudumu kwa muda mrefu na usafirishaji wake ni mgumu pamoja na kuwa inapaswa kuhifadhiwa katika sehemu yenye nyuzi 20 chini ya sufuri. Lakini hivi sasa Iran imezalisha dawa ambayo haina matatizo hayo na inazalishwa kwa wingi kiasi cha kuuzwa katika maeneo mengine duniani.

Na mwisho kabisa nchini Brazil mwezi Oktoba mwaka jana, wanasayansi walitangaza kuzalisha mamilioni ya mbu katika kiwanda ambao watatumika kuwaangamiza mbu wenzao wanaosababisha magonjwa.

Mbu hao waliofanyiwa mabadiliko ya kijenetiki wataenezwa ili watatumike kuwaangamiza mbu wanaosaababisha magonjwa hatari na yanayoua kama vile Zika, dengue na homa ya manjano. Kiwanda hicho ambacho kiko katika mji wa Piracicaba kaskazini magharibi mwa mji wa Sao Paulo kinaweza kuzalisha mbu milioni 60 kwa wiki na kimetajwa kuwa kiwanda cha kwanza na kikubwa zaidi duniani chenye uwezo wa kuzalisha mbu waliofanyiwa mabadiliko ya kijenetiki.

Brazil kuzalisha mbu milioni 60 kwa wiki ili wawaangamize mbu wanaosababisha Zika