Jan 14, 2017 00:25 UTC
  • Jumamosi, 14 Januari, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe 15 Mfunguo Saba Rabiu Thani 1438 Hijria sawa na tarehe 14 Januari 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 142 iliyopita, alizaliwa Albert Schweitzer katika mji wa Alsace-Lorraine hukoUfaransa. Albert Schweitzer ambaye alikuwa daktari na mtaalamu wa muziki, alielekea barani Afrika baada ya kukamilisha elimu katika fani ya udaktari na kuanzisha hospitali nchini Gabon. Hadi mwishoni mwa umri wake, Dakta Albert Schweitzer alijisabilia kuwasaidia na kuwatibu wananchi maskini wa Kiafrika. Tabibu huyo aliyekuwa na hisia za kibinadamu, ameandika vitabu kadhaa muhimu zaidi kikiwa kile cha "Falsafa yaUstaarabu". Mwaka 1952 Schweitzer alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobel kutokana na huduma zake kubwa kwa wagonjwa. Tabibu huyo Mfaransa alifariki dunia mwaka 1965. ***

Albert Schweitze

Katika siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, ulianza mkutano wa kihistoria wa kimataifa wa Casablanca nchini Moroco. Mkutano huo ambao ulihudhuriwa na Rais wa wakati huo wa Marekani Franklin Roosevelt na WaziriMkuu waUingereza Winston Churchill, wakiwa viongozi wa nchi muhimu za waitifaki, ulijadili mpango wa mashambulizi dhidi ya Sicily huko Italia, misaada ya nchi waitifaki kwa Russia na masuala mengine ya vita. Mwishoni mwa mkutano huo wawakilishi wa nchi zilizoshiriki walitoa taarifa ya pamoja ambayo kwa mujibu wake nchi waitifaki ziliapa kuendeleza vita hadi wakati wa kusalimu amri mahasimu wao bila ya masharti. ***

Mkutano wa Casablanca

Miaka 38 iliyopita katika siku kama ya leo, baada ya maandamano mtawalia ya wananchiwa Iran dhidi ya utawala wa kidikteta wa Mfalme Shah, kulitokea mapigano makubwa baina ya wanajeshi wa utawala huo na wananchi. Katika hali hiyo, baadhi ya wanajeshi ambao walikuwa wamefahamu na kudiriki, haki ya wananchi ya kuendesha mapambano, walikimbia kutoka katika vituo na kambi za kijeshi na kujiunga na harakati za wananchi na hivyo harakati za mapinduzi ya wananchiwa Iran kuzidi kupata nguvu. ***

Katika siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, maafisa wa shirika la ujasusi la Israel Mossad walitekeleza mauaji ya kigaidi dhidi ya Salah Khalaf maarufu kwa jina la Abu Iyad akiwa pamoja na maafisa wengine wawili wa ngazi za juu wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) huko Tunisia. Salah Khalaf alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu na kiongozi nambari mbili wa Fat'h baada ya Yaser Arafat. Mauaji ya viongozi hao wa ngazi za juu wa  PLO tena baada ya kukiukwa mamlaka ya kujitawala ya nchi nyingine yaani Tunisia, yalionyesha kwamba utawala haramu wa Israel hauheshimu sheria yoyote ile katika suala la kuwaangamiza wapinzani wake. ***

Salah Khalaf

Na miaka 6 iliyopita katika siku kama ya leo, Rais Zainul Abidin Bin Ali wa Tunisia na dikteta wa nchi hiyo alikimbilia Saudi Arabia kufuatia vuguvugu la mapinduzi ya wananchi. Zainul-Abidin aliingia madarakani mwaka1987 kupitia mapinduzi ya kijeshi bila umwagaji damu na kumwondoa madarakani Habib Bourguiba aliyekuwa amejitangaza kuwa rais wa maisha wa nchi hiyo. Bin Ali aliiongoza Tunisia kwa mkono wa chuma kwa miaka 23 huku akiendeleza siasa za kutegemea Wamagharibi na kupiga vita Uislamu. Kujichoma moto kijana mmoja muuza mboga katika kulalamikia dhulma na ukatili wa maafisa usalama wa utawala wa nchi hiyo, kuliibua harakati ya wananchi wa Tunisia dhidi ya utawala wa fisadi wa Bin Ali na hatimaye kupinduliwa dikteta huyo.***

 

Zainul Abidin Bin Ali