Jan 30, 2017 06:46 UTC
  • Maadhimisho ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sehemu ya Tatu)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi wa Idhaa ya Kiswahili, Radio Tehran. Hivi sasa tumo katika maadhimisho ya Alfajiri 10 za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Leo tumeamua kukuleteeni kipindi maalumu kwa mnasaba huo ambapo tutajaribu kutupia jicho kwa muhtasari historia ndefu na chungu ya uingiliaji wa madola ya kibeberu hususan Marekani katika masuala ya ndani ya Iran.

Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran ambayo yana utambulisho wa kupiga vita mfumo wa kibeberu na dhulma ya aina yoyote ile, ni kikwazo kikubwa kwa madola ya kiistikbari ulimwenguni. Kimsingi, kupambana na uistikbari ni moja ya misingi isiyotetereka ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Fikra za kisiasa za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu zimesimama juu ya msingi wa mapambano katika njia ya haki na uadilifu na ni kwa sababu hiyo ndio maana historia ya Mapinduzi ya Kiislamu imejaa mapambano na kusimama imara taifa la Iran katika kukabiliana na madhihirisho yote ya dhulma na ukosefu wa uadilifu. Katika moja ya miongozo yake iliyojaa hekima, Imam Khomeini, MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema:

Kama mnataka kuyashinda matatizo yote, mnapaswa kuwa imara mbele ya madola ya kibeberu. Kama ambavyo mnapaswa pia kuwa na msimamo imara katika kulinda uhuru wenu; uhuru wa kiutamaduni, uhuru wa kiuchumi na uhuru wa kijamii. Inabidi yote hayo myalinde kwa nguvu zenu zote. Na hilo linawezekana chini ya kivuli cha kushikamana na mafundisho ya Uislamu, na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu Mkubwa na kuwa kitu kimoja; sambamba na matabaka yote ya watu kujiona kuwa ni ndugu. Adui yuko mawindoni.

Imam Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

 

Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu umezaliwa ndani ya mapambano makali dhidi ya uistikbari na kila moja ya matukio yaliyoambatana na mapambano hayo ni mfano wa kuigwa wa muqawama na mapambano katika njia ya kuangamiza dhulma na ukosefu wa uadifu na katika njia ya kujiimarisha na kujikamilisha kiasi kwamba harakati hiyo haijawahi kukwama wala kusita hata mara moja. Kwenye miaka yote hii, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haijawahi kulegalega katika kukabiliana na siasa za kibeberu za Magharibi na Mashariki, na katika vipindi nyeti vya kihistoria, kila pale Marekani ilipojitokeza hadharani kukabiliana na Iran, taifa hili limesimama imara zaidi kukabiliana na njama za madola ya kibeberu na kuonesha kivitendo kwamba, kusimama imara kukabiliana na uistikbari wa kimataifa si maneno matupu, bali ni bango la matukufu ambayo taifa la Iran lina imani nayo na limesimama imara kuyalinda mbele ya njama za mabeberu. Katika sehemu nyingine ya miongozo yake iliyojaa busara na muono wa mbali, Imam Khomeini MA alisema:

Leo hii Mwenyezi Mungu Mtukufu ameijaalia nchi kuwa mikononi mwenu na hivi sasa mnaitumikia na mnapaswa kulizingatia vizuri jambo hilo na mtambue kuwa nchi yenu leo hii iko peke yake kati ya nchi zote nyingine. Nchi zote ziko dhidi yetu, ukitoa nchi chache tu. Lakini kwa vile nchi yenyewe ni ya waumini, na watu wake wana imani na wanaitakidi kwamba wanapaswa kutawakali kwa Mwenyezi Mungu kutatua matatizo yao, tutafanikiwa katika malengo yetu matukufu. Hivi sasa kuna fikra zimeanza kufanyiwa kazi, kuna harakati mbalimbali zimeanza na leo hii Iran imeendelea zaidi kuliko wakati ule ambapo kulikuwa kunapigwa makelele mengi ya kudai kuwa Iran ni taifa lenye ustaarabu mkubwa. Amma lililo muhimu zaidi ni kwamba sasa hivi tuko huru na hakuna mtu yeyote duniani anayeweza kumdhalilisha hata topasi wetu. Nyinyi muko huru sasa hivi na ni mabwana wa nafsi zenu.

Imam Khomeini akirejea nchini Iran siku chache kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran

 

Unapoangalia historia ya uhusiano wa Iran na Marekani utaona kuwa katika siasa zake kuhusiana na Iran, siku zote Marekani imekuwa ikifuata mkondo wa kuingilia mambo ya ndani ya Iran; hiyo ikiwa ndiyo ajenda yake kuu. Katika kila kona ya historia ya uhusiano baina ya nchi hizi mbili, unaonekana kwa uwazi sana uingilia wa moja kwa moja na usio wa moja kwa moja wa Marekani katika masuala ya ndani ya Iran.

Watafiti wengi wamefichua kwamba, mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika nchini Iran tarehe 19 Agosti 1953 ulikuwa ndio mwanzo wa uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Iran. Wakati huo huo tunaweza kuuona pia uingiliaji wa miongo mingi wa Marekani katika masuala ya ndani ya Iran wakati tunapotupia jicho siasa za migawanyo ya kisiasa wakati wa vita baridi. Kwa mfano wakati wa mapinduzi ya mwaka 1917, muungano wa nchi waitifaki uliivamia ardhi ya Iran, na wakati huo Marekani ikaanza kuukodolea macho ya tamaa utajiri wa mafuta wa Iran. Matukio ya Vita vya Pili vya Dunia yaliifanya Marekani iweke mkataba wa kijeshi na Iran. Uhusiano huo ulipelekea kuwekwa mkataba wa dola milioni 10 za kuiuzia silaha Iran. Hata hivyo matukio ya mwanzoni mwa muongo wa 1950 yalileta mabadiliko makubwa na ya kimsingi katika uhusiano wa Iran na Marekani. Mabadiliko hayo yalikwenda sambamba na uingiliaji mkubwa na wa pande zote wa Marekani katika masuala ya ndani ya Iran. Mapinduzi ya kijeshi ya Agosti 19, 1953, yaliandaa uwanja wa kuingilia Marekani masuala ya ndani ya Iran katika miaka mingi ya baadaye.

Mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Marekani na Uingereza mwezi Agosti 1953 yaliyoipindua serikali halali na ya kisheria ya wakati huo, yaani serikali ya Dk Mosadiq, yanakumbushia kipindi kichungu katika historia ya kisiasa ya Iran kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kwa mujibu wa nyaraka za siri ambazo zilisambazwa baadaye, Shirika la Kijasusi la Marekani CIA lilikuwa na nafasi kuu katika kupanga na kuongoza mapinduzi hayo na hatimaye kumpindua Waziri Mkuu wa wakati huo wa Iran katika kipindi cha baina ya mwaka 1952 hadi mwezi Agosti 1953.

Mark Gaziyorsky, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha George Washington anasema:

Watu 155 wanakuja kuisaidia CIA. CIA yatia mkono hali ya mambo nchini Iran mwezi mmoja kabla ya mapinduzi ya kijeshi na kuandaa mazingira ya kufanyika mapinduzi. Baadhi ya magazeti yamepewa hongo ili kumwandika vibaya Mosadiq kwenye magazeti yao na kuonesha kwamba hana uwezo wa kuongoza nchi.

Dk Mohammad Mosadiq, Waziri Mkuu wa zamani wa Iran

 

Mapinduzi ya kijeshi yaliyofanywa na Marekani na Uingereza dhidi ya serikali halali ya Iran wakati huo, tena katika kipindi ambacho taifa la Iran lilikuwa linapita kwenye kipindi nyeti cha kulinda utajiri wake wa mafuta, lilikuwa ni pigo kubwa kwa manufaa ya kisiasa na kiuchumi ya Iran. Hivi sasa miaka 60 imepita tangu kutokea mapinduzi hayo ya kijeshi yaliyoongozwa na Marekani na Uingereza nchini Iran, lakini hadi leo hii madola hayo mawili ya kibeberu yanatumia mbinu tofauti na kwa nyakati mbalimbali kuingilia masuala ya ndani ya Iran.

Madeline Albright, waziri wa mambo ya nje wa Marekani wakati wa urais wa Bill Clinton, mwaka 2000 alikiri waziwazi kuwa Marekani ilihusika kwenye mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 19 Agosti 1953 nchini Iran lakini hapo hapo alidai kuwa kupinduliwa serikali ya kitaifa ya Iran mwaka 1953 kulitoa mwanya kwa Iran kupiga hatua kubwa za ustawi wa kisiasa.  Alisema:

Iran na Marekani zina mambo mengi ya pamoja, lakini mambo hayo yamefifilizwa na masuala mengine ya pembeni. Hatua zilizochukuliwa na Marekani mwaka 1953 zilichukuliwa kwa sababu za kiistratijia. Hata hivyo mapinduzi ya kijeshi ya mwaka huo yalikuwa ni kulirejesha nyuma taifa la Iran. Hivyo mtu anaweza kufahamu kiurahisi sana kwa nini Wairan hadi leo hii wanachukizwa na uingiliaji huo wa Marekani katika masuala yao ya ndani.

Mwaka 2009 pia, Barack Obama, na mwaka 2011 Hillary Clinton, waziri wa mambo ya nje wa wakati huo wa Marekani walielezea kusikitishwa kwao na mapinduzi hayo ya mwaka 1953 dhidi ya serikali halali nchini Iran. Katika mahojiano aliyofanyiwa na gazeti la New York Times tarehe 15 Januari 2009, Barack Obama, rais wa zamani wa Marekani alisema: Wakati tunapotupia jicho historia ya Iran uhakika huu unaonekana wazi kwamba sisi tulihusika katika mapinduzi ya serikali iliyochaguliwa kidemokrasia nchini Iran.

 

Ukurasa wa Intaneti wa Usalama wa Taifa wa Marekani kwa mara ya kwanza mwezi Aprili 2000 ulisambaza nyaraka za siri kuhusiana na mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 19 Agosti nchini Iran na kwa mara ya kwanza ukajulikana kwa undani zaidi mwenendo mzima wa mapinduzi hayo. Makala hiyo iliwekwa wazi kwa walimwengu wote kuweza kuisoma ndani ya makala ya gazeti la New York Times kwenye Intaneti. Hata shirika la habari la BBC nalo liliithibitisha habari hiyo kwa kusema:

Nyaraka ambazo leo hii CIA imezisambaza baada ya kupita miongo 6 ya kutokea kwake zimeondoa shaka zote zilizokuwepo kuhusiana na kuhusika Marekani na Uingereza katika mapinduzi ya Agosti 19 (1953 nchini Iran).

Baada ya mapinduzi hayo, Marekani ilipanua ubeberu wake nchini Iran. Serikali ya Dwight D. Eisenhower, rais wa 34 wa Marekani ilifuata sera ya kuzitia nguvu tawala za nchi zilizo dhidi ya Umoja wa Kisovieti katika Ulimwengu wa Tatu. Hivyo katikati ya muongo wa 1960 serikali ya Marekani ilianza kutekeleza mpango mkubwa wa kuwapa mafunzo na silaha za kivita wanamgambo, polisi na mashirika ya kijasusi katika nchi vibaraka wake kwenye eneo hili ikiwemo Iran. Katika hotuba yake ya kwanza rasmi baada ya kuwa rais wa Marekani, Eisenower alisema:

Sidhani kwamba kuna eneo lolote lililo muhimu zaidi katika ramani ya dunia kuliko Iran... Hatupaswi kuruhusu Iran iwe ni dola kubwa lenye nguvu za kijeshi. Hatupaswi kuruhusu kutokea siku ambayo Iran itarejea kwenye zama zake za kale na kuwa dola lenye nguvu za kijeshi. Itakuwa ni hasara kubwa kwetu siku ambayo nguvu za kijeshi za Iran zitafufuka. Nendeni mkasome historia ya nchi hiyo, ili muweze kuelewa ninasema nini.

Wakati alipouawa John F. Kennedy rais wa 35 wa Marekani mwaka 1963, na makamu wake, Lyndon B. Johnson kushika madaraka na kuwa rais wa 36 wa Marekani, alifanya haraka sana kupasisha muswada ambao kwa mujibu wake, Iran ingelinunua silaha za kijeshi za Marekani zenye thamani ya dola milioni 200. Sambamba na kuunga mkono mapinduzi meupe ya Shah, Johnson aliunga mkono pia ukandamizaji uliofanywa na serikali ya Shahd dhidi ya maandamano ya wananchi ya mwezi Juni 1963. Kwa mtazamo wa rais huyo wa Marekani, Shah mwenyewe alikuwa ni mlinzi na mdhamini wa manufaa ya Marekani. Uungaji mkono wa Johnson na washauri wake kwa Shah wa Iran ulikuwa mkubwa kiasi kwamba hata waliona ukandamizaji uliofanywa na Shah dhidi ya wananchi wa Iran hautoshi na waliamini kwamba alipaswa kuchukua hatua kali zaidi za kuwakandamiza wapinzani wake.

Baada ya Johnson, Richard Nixon alikuwa rais wa 37 za Marekani na hapo ulianza ukurasa mpya wa mahusiano ya karibu sana na ya kushibana baina ya Shah na utawala wa Marekani. Miezi michache kabla ya kuchaguliwa kuwa rais wa Marekani, Nixon alitembelea Iran na kuonana na Shah mjini Tehran. Inaonekana alitoa ahadi za kumpa rafiki yake wa siku nyingi, yaani Shah wa Iran silaha zaidi za kivita zinazotengenezwa Marekani.

Maadhimisho ya Alfajiri Kumi hufana zaidi mwaka baada ya mwaka

 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo wa Marekani alisema:

Tangu mwaka 1953 wakati Shah aliporejea Iran, tulikuwa tunafuatilia kikamilifu nyendo zote za Shah hadi mwaka 1972. Ni sisi ndio tuliokuwa tukimwambia kwamba wewe huhitajii silaha fulani kwani hazina faida kwako na matokeo yake katika kipindi hicho cha miaka 22; thamani ya silaha ambazo Marekani ilipendekeza na kuidhinisha kupewa Shah haikupindukia dola bilioni 1 na milioni 300. Lakini baada ya mwaka 1972 yaani baada ya Nixon na Kissinger kumpa hiari Shah ya kununua silaha anazotaka, kiwango cha silaha zilizonunuliwa na Shah kutoka Marekani kiliongezeka kwa mara 20 katika kipindi cha miaka 7 tu. Kwa kweli kitendo tulichofanya kilikuwa ni kama vile kumkabidhi mtu mlevi kupindukia, funguo za ghala ya pombe.

Katika kipindi chote cha urais wake, Nixon alimimina silaha za kila namna na washauri wake wengi wa kijeshi nchini Iran na wakati wote akawa anamuunga mkono kikamilifu Shah katika siasa zake za kiimla na za ukandamizaji nchini Iran. Ni wakati huo ndipo Richard Helms, mkuu wa zamani wa Shirika la Kijasusi la Marekani CIA alipoteuliwa kuwa balozi mkubwa wa Marekani nchini Iran na kupewa jukumu la kusimama kazi zote za kiusalama na kijasusi za Marekani nchini Iran na ni wakati huo ndipo ujasusi wa Marekani ulipoongezeka kupindukia humu nchini. Kituo cha CIA nchini Iran kiliimarika zaidi, na Tehran iligeuzwa kuwa kambi kuu ya Shirika la Kijasusi la Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati. Kipindi hicho kilikwenda sambamba na kutiwa mbaroni kwa wingi sana wapinzani wa utawala wa kiimla wa Shah pamoja na kutolewa hukumu za vifo na mateso katika jela za kuogofya za Shah ambaye hakusita kuchukua hatua yoyote ya kinyama dhidi ya wapinzani wake. Pamoja na hali kuwa mbaya kiasi chote hicho, lakini hakuna radiamali yoyote wala upinzani wa aina yoyote uliooneshwa na serikali ya Marekani kupinga ukandamizaji na mateso hayo yaliyokuwa yakifanyika nchini Iran.

Hata wakati yalipokaribia kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Brzezinski, mshauri wa masuala ya usalama wa taifa wa Jimmy Carter, Rais wa 39 wa Marekani ambaye naye alikuwa miongoni mwa waungaji mkono wa vitendo vya ukandamizaji dhidi ya wapinzani wa Shah, alimtaka mfalme huyo wa Iran atumie nguvu kukabiliana na uasi wa mitaani. Cyrus Vance, waziri wa mambo ya nje wa Marekani wakati wa urais wa Jimmy Carter alihalalisha uungaji mkono huo wa Marekani kwa Shah wa Iran akisema: Kwa kuzingatia hali ya kimataifa ilivyo hivi sasa na ili kuweza kulinda manufaa ya Marekani, hatuna njia nyingine ila kumuunga mkono kikamilifu Shah kwa nguvu zetu zote.

Maadhimisho ya Alfajiri Kumi nchini Iran huwa na sura ya kimataifa

 

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia, taasisi za kisiasa, kipropaganda, kiusalama, kisheria na kiuchumi za Magharibi hususan Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel, zimeelekeza nguvu zao zote kwenye kuupiga vita mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Mara baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ubalozi wa Marekani mjini Tehran uligeuka kuwa makao makuu ya njama za maadui wa mapinduzi hayo matukufu. Siku ya pili tu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yaani tarehe 23 Bahman 1357 (mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia siku iliyosadifiana na tarehe 12 Februari 1979) ubalozi huo ulianzisha njama za kuigawa vipande vipande Iran. Kuna nyaraka zinazoonesha kuwa, serikali ya Marekani tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ilianzisha njama za kuikata vipande vipande Iran kama nia ya kuudhoofisha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Moja ya nyaraka hizo zinaonesha kuwa, ubalozi wa Marekani mjini Tehran ulikuwa na hamu ya kutumia hisia za kikaumu na kikabila kuipindua Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Njama za Wamarekani dhidi ya taifa la Iran hazijawahi kusita hata mara moja. Viongozi mbalimbali wanaoingia madarakani huko Marekani, hawazembei fursa yoyote wanayoipata ya kutoa pigo kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Miongoni mwa njama kubwa zilizofanywa na mabeberu wa dunia dhidi ya taifa la Iran, ni kuushawishi utawala wa Saddam wa Iraq kuivamia Iran na kuanzisha vita vya miaka minane dhidi ya utawala mchanga wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu. Hata baada ya vita hivyo vya miaka minane ambayo Iran ililazimishwa kupigana, chuki na uadui wa Marekani umeendelea kuwepo ikiwa ni pamoja na kudai viongozi wa Marekani kuwa eti Iran ni katika mhimili wa shari, matamshi yaliyotolewa mwaka 2002 na George W. Bush, rais wa wakati huo wa Marekani.

"Marekani haiwezi kuifanyia Iran upuuzi wowote"

 

Vikwazo dhidi ya Iran ni mbinu nyingine chafu inayotumiwa na mabeberu wa dunia hasa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hata baada ya kufikiwa makubalino ya nyuklia ambayo yalisisitiza kuondolewa vikwazo vyote dhidi ya Iran, hadi leo hii si tu vikwazo hivyo havijaondolewa, lakini kila leo Marekani inapasisha vikwazo vipya dhidi ya Iran ya Kiislamu huku watawala wapya wa nchi hiyo ya kibeberu wakitishia kuyachana makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa baina ya Iran na kundi la 5+1 maarufu kwa jina la makubaliano ya JCPOA.

Alaakullihaal, matukio hayo katika historia ya mapambano ya taifa la Iran yanaonesha kuwa taifa hili la Kiislamu haliko tayari kudhalilishwa na bila ya shaka ni kwa kuangalia historia hiyo ndio maana wananchi wa Iran wanachukizwa na viongozi wa Marekani na hawana imani nao hata kidogo.

Naam wasikilizaji wapenzi, na kufikia hapa ndio tunafikia tamati ya sehemu nyingine ya mfululizo wa makala hizi maalumu tulizokuandalieni kwa mnasaba wa maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran maarufu kwa jina la Alfajiri Kumi. Ishini Salama.