Hadhithi ya Uongofu (65)
Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia suala la subira na ustahamilivu na tulisema kuwa, subira ni nguzo muhimu ya imani. Kiasi kwamba, Imam Ali bin Abi Talib as anaitaja nafasi ya subira katika imani kwamba, ni mithili ya nafasi ya kichwa katika mwili.
Maisha ya hapa duniani siku zote huambatana na panda shuka, vizingiti, vikwazo na matatizo mbalimbali. Kwa msingi huo bila ya mwanadamu kuwa na subira na kusimama kidete mbele ya mawimbi ya matatizo, bila shaka hawezi kufika popote. Kisingi ni kuwa, ufunguo mkuu wa ushindi na mafanikio ni subira na stahamala. Kwa kuzingatia kwamba, dini ni majimui ya maamrisho na makatazo, hapana shaka kuwa, kutii na kuacha maasi hakuwezi kutimiana kudumu pasina ya subira na kusimama kidete.
Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana Imam Ali bin Abi Talib as anaambatanisha subira na kupata ushindi pale anaposema:
“Subira ni sawa sawa na ushindi.”
Aidha katika Kitabu kitakatifu cha Qur’ani kumetajwa sharti muhimu la ushindi kwa wanaopigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kuwa ni kusubiri na kusimama kidete n kwamba, kufanya hivyo huwafanya wapate ushindi hata kama wao ni wachache ukilinganisha na maadui.
Aya ya 65 ya Surat al-Anfal inabainisha jambo hilo kwa kusema:
“Wakiwapo kati yenu ishirini wanao subiri watawashinda mia mbili. Na wakiwapo kati yenu mia watawashinda elfu moja katika walio kufuru.”
Subira na kusimama kidete humpa nguvu mtu mmoja mwenye subira ya kuweza kukabiliana na watu kumi na watu mia moja wenye subira kuweza kukabiliana na watu elfu moja. Watu ambao wana irada dhaifu na hamu ndogo ya kusimama kidete, hukimbia haraka kutoka katika medani ya matukio au huwa hawakii kupiga magoti na kusalimu amri. La kufahamu ni kwamba, si dunia wala akhera ambayo mtu hupewa asina ya kuwa na suibira na ustahamilivu. Ndio maana hii leo tunashuhudia kwamba, mataifa yaliyopiga hatua na kupata maendeleo na ustawi ulimwenguni ni yale ambayo yamesimama kidete na kuwa na subira zaidi mbele ya mawimbi na misukosuko.
Hadithi ifuatayo imenukuliwa kutoka kwa Imam Ali bin Abi Talib as ya kwamba amesema:
Mtu mwenye kupanda kipando cha subira na ustahamilivu hutia mguu katika medani ya ushindi.”
Katika upande mwingine watu wenye subira ndogo na wasiosimama kidete na imara, haraka hutumbukia katika uchafu wa dhambi. Hii ni kutokana na kuwa, dhambi ina mvuto na nguvu kwa nafsi yenye kukengeuka na kama mtu hataonyesha kusimama kidete mno mkabala wa nguvu hiyo ivutayo, basi huvutwa katika dhambi.
Imam Ja’far Sadiq as amenukuliwa akisema kuwa: Mara nyingi imetokea kuwa, saa moja ya kusubiri na kustahamili ilipelekea furaha ya muda mrefu; na mara nyingine imetokea kwamba, ladha ya muda mfupi katika saa moja, ilipelekea ghamu na huzuni ya muda mrefu.”
Mtu kuwa na subira mbele ya mabaa na misiba hupelekea kukwezwa katika njia ya saada na ukamilifu wa mwanadamu.
Mbora wa viumbe Bwana Mtume saw amenukuliwa akisema kuwa, kuna daraja ya mwanadamu kwa Mwenyezi ambayo mja hawezi kuifikia kwa kuifanya kazi yoyote ile, mpaka pale Allah atakapoutia balaa na mtihani mwili wake. Wakati huo mja hufikia daraja hiyo kupitia balaa ile.
Aidha mtu mwenye kuwa na subira dua zake hutakabaliwa na Mola na misiba yake hufidiwa na Mola Jalia.
Katika Qur’ani Tukufu Mwenyezi Mungu amebainisha daraja ya juu mno kwa wenye kusubiri. Aaya za 156 na 157 za Surat al-Baqara zinasema:
Wale ambao ukiwasibu msiba husema: Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye hakika tutarejea. Hao juu yao zitakuwa baraka zitokazo kwa Mola wao Mlezi na rehema. Nao ndio wenye kuongoka.
Aidha Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 10 ya Surat Zumar:
Sema: Enyi waja wangu mlio amini! Mcheni Mola wenu Mlezi. Wale wafanyao wema katika dunia hii watapata wema. Na ardhi ya Mwenyezi Mungu ni kunjufu. Hakika wenye subira watapewa ujira wao bila ya hisabu.
Imenukuliwa kutoka kwa Imam Sadiq as kwamba: Siku ya Kiyama kundi fulani la watu litakuja na kusimama mbele ya mlango wa pepo na kasha kuugonga mlango huo. Wataulizwa, ninyi ni akina nani? Watajibu kwa kusema, sisi ni watu wa subvira. Wataulizwa: Mmesubiri juu ya kitu gani? Watasema: tumesubiri juu ya taa na kumuasi Mwenyezi Mungu. Kisha Mwenyezi Mungu atasema: Wamesema kweli hao, waingizeni peponi. Kisha Imam Sadiq as akasema: hii ndio ile kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:
Hakika wenye subira watapewa ujira wao bila ya hisabu.
Kwa msingi huo basi, kufanya subira mbele ya dhambi, misiba na mabalaa, ni jambo ambalo humrahishia mwanadamu hesabu yake Siku ya Kiyama.
Imekuja katika Hadith al-Qudsi ya kwamba Allah amesema: Kwa kuwa mja mongoni mwa waja wangu alipopata mtihani wa mali au msiba wa kuondokewa na mwanawe alisubiri na kustahamili mtihani huo, ninaona haya na aibu kuweka mizani ya hesabu na kufungua daftari lake kwa ajili ya kuhesabu amali na matendo yake.
Kufanya subira humdhaminia mwanadamu pepo. Bwana Mtume saw amenukuliwa akisema kuwa: Njia ya pepo imejaa mitihani na majaribu na subira na uvuimilivu mkabala wake. Mtu ambaye atakuwa na subira mbele ya matatizo katika njia ya Mwenyezi Mungu na akapambana jihadi na nafsi yake, ataingia peponi. Lakini njia ya motoni imejaa matamanio na starehe. Mtu ambaye atasalimu amri mbele ya nafsi inayoamrisha maovu basi hatima yake ni kuingia katika moto wa Jahanamu.
Wapenzi wasikilizaji kwa hadithi hiyo ya Bwana Mtume saw ndio tunafikia tamati ya kipindi chetu kwa juma hili9. Jiungeni name wiki ijayo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu.
Ahsanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini…