Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (150)
Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran.
Ni wiki nyingine tunapokutana tena kwenye kipindi hiki kinachojadili maswali mbalimbali yanayohusiana na itikadi ya Kiislamu. Katika kipindi cha juma hili tutaendelea kujadili suala ambalo tumekuwa tukilijadili katika vipindi sita vilivyopita nalo ni kuhusiana na wajibu wa Umma wa Kiislamu kuhusiana na kizazi cha Mtume Mtukufu (saw) na haki walizonazo kwa umma huu. Katika vipindi hivyo tulifahamu wajibu sita kati ya wajibu hizo kwa msingi wa mafundisho matakatifu, wajibu ambao ni pamoja na: Wajibu wa kutiiwa kikamilifu na kufuata mafundisho yao katika shughuli zote za maisha yetu, wajibu wa kurejea kwao ili kupata hukumu sahihi ya Qur’ani kuhusiana na matuklio tofauti na hitilafu zote zinazotokea miongoni mwetu, wajibu wa kuwaswalia pamoja na bwana wao mtukufu al-Mustafa na kuepuka kumswalia swala ya mkato ambayo Mtume Mtukufu mwenyewe (saw) ameikataza, tunapokuwa kwenye swala na nje ya swala. Wajibu wa wanne ni kuwapenda na kufadhilisha mahaba yao juu ya mahaba ya watu wengine kwa sababu mahaba hayo hufungamana na mahaba ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw).
Wajibu wa tano ni kuwatukuza na kuwaenzi kutokana na nafasi aali waliyonayo mbele ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw), pamoja na kujitoilea kwao katika kulinda dini ya haki inayowaongoza wanadamu na kuwahudumia waja wote wa Mwenyezi Mungu. Na haki ya sita ni kuwabai, kuwanusuru na kuwasaidia katika kufanikisha haki na uongofu pamoja na kutetea njia yao safi ya Mtume Mtukufu (saw). Baada ya kujua haki hizo, tunajiuliza kwamba je, haki ya saba ni ipi?
Wapenzi wasikilizaji tulijadili katika kipindi maalumu na kupata kufahamu haki alizonazo Mtume Mtukufu (saw) kwa Umma wa Kiislamu. Tulifahamu kwamba kati ya haki hizo za Mtume ambazo zimesisitizwa na aya kadhaa za Qur’ani Tukufu ni haki ya kumzuru na kuomba maghfira na kutawasili naye kwa Mwenyezi Mungu. Hii pia ni haki ya makhalifa wake kumi na wawili katika Maimamu watoharifu wa Nyumba ya Mtume (saw). Mwenyezi Mungu amewajaalia thawabu nyingi mno wale wanaotekeleza wajibu huu wa kimaadili ambao unabainisha utiifu kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw) na wema na mfungamano kwa kizazi cha Mtume, kama inavyosema riwaya ambayo imepokelewa kutoka kwa Amir al-Mu’mineen Ali (as) katika kitabu cha Kamil az-Ziyaraat anaposema kwamba siku moja Mtume (saw) aliwatembelea nyumbani kwao ambapo walimkaribisha kwa chakula na baada ya kula alinawa mikono kwa maji aliyomwagiwa na Imam Ali (as). Baada ya kunawa alipangusa uso na ndevu zake kwa unyevunyevu uliokuwa umesalia mikononi kisha akaondoka kwenda kuswali kwenye msikiti uliokuwa nyuma ya nyumba hiyo. Aliswali na kuendelea kusuju kwa muda mrefu huku akiwa analia. Kisha aliinua kichwa chake na kila mmoja akawa amekaa kimya bila kuuliza swali. Baada ya muda Hussein alimwendelea na taratibu kumkalia miguuni. Hussein aliweka kidevu chake kwenye kifua cha Mtume na kisha kumuuliza ni kwa nini alikuwa akiilia. Mtume (saw) alimjibu kwa kumwambia kwamba siku hiyo alikuwa amewatazama na kufurahishwa sana nao furaha ambayo alikuwa hajawahi kuishuhudia maishani. Ghafla akateremka Malaika Jibril na kumpasha habari kwamba wanawe hao wangeuliwa na maadui. Baada ya kupata habari hiyo Mtume alimshukuru Mwenyezi Mungu na kuwaombea heri. Hapo Hussein akamuuliza Mtume ni nani angewazuru baada ya wao kuuawa, naye Mtume (saw) akamjibu kwa kumwambia kwamba ni kundi moja kutoka kwenye Umma wake, kundi ambalo litafanya hivyo kwa ajili ya kutaka radhi na mfungamano na Mtume ambapo Siku ya Kiama Mtume huyo naye atawalipa wema huo kwa kuwaepusha na moto mkali wa Jahannam.
Kama ambavyo katika wajibu huu kuna kuunga uhusiano na kumfanyia wema Mtume (saw) pia kuna kutangaza utiifu kwa agano la wilaya ya Imamu wa haki. Kwa mfano Sheikh Swaduq anasema katika vitabu vyake vya Man La Yahdharuhu al-Faqih, Uyun Akhbar ar-Ridha na Ilal as-Sharai,’ Mufid katika kitabu cha al-Muqnia,’ Kuleini katika kitabu cha al-Kafi na wengineo wakimnukuu Imam Rridha (as) akisema: ‘Hakika kila Imam ana agano kwenye shingo za mawalii na wafauasi wake. Hakika mfano bora zaidi wa kutekeleza agano ni kuzuru makaburi yao – yaani Maimamu (as) – hivyo mtu atakayewazuru kwa hamu ya kuwazuru na kuthibitisha yale waliyoyahimiza, bila shaka Maimamu wao hao watakuwa wanaowaombea shufaa Siku ya Kiama.’
Kuna hadithi nyingi sana zinzazozungumzia fadhila za kuwazuru Ahlu Beit wa Mtume Mtukufu (saw). Hadithi hizo zinasisitiza wazi kuwa wajibu huu wa kuwazuru unathibiti katika uhai wao na vilevile baada ya wao kuaga dunia, kwa kuyatembelea makaburi yao.
Ziara ya Mtume (SAW) imesisitizwa sana katika uhai wake na baada ya kuaga kwake dunia na hasa baada ya kukamilika ibada tukufu ya Hija. Ziara hiyo hukamilisha ibada hiyo na kuacha kulizuru kaburi lake baada au kabla ya kufanya Hija ni katika mifano ya wazi ya kumtelekeza na kumpuuza kama ilivyopokelewa kutoka kwake mwenyewe kupitia madhebeu zote mbili. Na suala hilo pia linawahusu mawalii na makhalifa wake watoharifu (as). Hivyo ukamilifu wa Hija hutimia kwa kuwazuru watukufu hao katika uhai wao na makaburi yao baada ya kuaga kwao dunia kama ilivyosisitizwa katika hadithi nyingi ambazo tutakusomeeni baadhi hivi punde. Endeleeni kuwa pamoja nasi.
Thiqatul Islam al-Kulein amenukuu katika kitabu chake cha al-Kafi na as-Swaduq katika vitabu vyake vya as-Sharai’ na Uyun al-Akhbar kutoka kwa Imam Muhammad al-Baqir (as) kuwa: ‘Watu waliamrishwa wafike kwenye mawe haya na kuyazunguka na kisha waje kwetu na kutupasha habari za ufuasi wao kwetu na kutufahamisha nusura (msaada) wao.’ Imam huyo mtukufu (as) amenukuliwa katika hadithi nyingine akisema: ‘Anzieni Makka na kisha mkamilishe kwa kutuzuru.’
Hadithi ya tatu kutoka kwa Imam huyo (as) katika kufasiri maneno ya Mwenyezi Mungu yanayosema: ( ثُمَّ لْيَقْضُوا تَفَثَهُمْ) Kisha wajisafishe taka zao, Imam anasema neno تَفَثَْ hapa ni kukutana na Imam. Na katika hadithi nyingine Imam Swadiq (as) amenukuliwa akisema: ‘Mmoja wenu anapohiji, basi na ahitimishe Hija yake kwa kutuzuru kwa sababu hilo ni katika kukamilisha Hija.
Tunahitimisha kipindi hiki kwa kunukuu hadithi iliyonukuliwa na as-Swaduq katika kitabu cha al-Khiswal kutoka kwa Imam Ali (as) kwamba alisema: ‘Mzuruni Mtume (saw) katika Hija yenu mnapotoka kwa ajili ya Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu. Hii ni kwa sababu kutomzuru ni kumtelekeza ilihali mmeamrishwa kutekeleza wajibu huo. Na yazuruni makaburi ambayo Mwenyezi Mungu amekuamrisheni kuyapa haki zake na kuyazuru, na tafuteni riziki kando ya makaburi hayo.’
Na kufikia hapa ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho mmekitegea sikio kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo majaaliwa tunakuageni nyote wapenzi wasikiliza kwa kusema, Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.