Mar 02, 2017 02:36 UTC
  • Alkhamisi, Pili Machi, 2017

Leo ni Alkhamisi tarehe 3 Jumadithani 1438 Hijria sawa na tarehe Pili Machi, 2017.

Siku kama ya leo miaka 1426 iliyopita alikufa shahidi Bibi Fatima al Zahra, binti mtukufu wa Mtume wetu Muhammad (saw) na mke wa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Alizaliwa miaka mitano baada ya kubaathiwa Nabii Muhammad (saw) na mtukufu huyo akampa jina la Fatima. Alipewa malezi na wazazi wake wawili yaani Bibi Khadija na Mtume wa Mwenyezi Mungu na kupata maarifa aali ya dini kutoka kwa baba yake. Bibi Fatima alifikia daraja za juu za ukamilifu wa kiroho na kimaanawi ndani ya nyumba ya wahyi na ufunuo. Baada ya kuolewa na Imam Ali bin Abi Twalib ambaye alikuwa kielelezo halisi cha takwa na uadilifu, Bibi Fatima alikuwa na nafasi kubwa na alitoa mchango wa aina yake katika jamii ya Kiislamu. Alikuwa dhihirisho la uchamungu, ukarimu, kujitolea, subira, kujipinda katika ibada na kuwasaidia watu wote na alilea watu adhimu kama Imam Hassan na Hussein (as).

Siku kama ya leo miaka 121 iliyopita sawa na tarehe Pili Machi mwaka 1896 mwanafikizia wa Kifaransa Henri Becquerel alivumbua nururishi au Radioactivity baada ya kufanya utafiti katika mada za urani na vitu vinginevyo. Becquerel alikuwa akichunguza urani ndipo alipogundua nururishi. Utafiti wa mwanafikizia huyo wa Kifaransa ulimfanya atunukiwe tuzo ya Nobel mwaka 1903 na miaka mitano baadae aliaga dunia.

Henri Becquerel

Siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, mwafaka na tarehe Pili Machi mwaka 2004, mamia ya watu wasio na hatia waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika miripuko kadhaa mikubwa iliyotokea katika shughuli ya kukumbuka kuuawa shahidi Imam Hussein (AS) huko katika miji mitukufu ya Karbala na Kadhimein nchini Iraq. Katika mwaka huo wananchi Waislamu wa Iraq walifanya maadhimisho hayo kwa hamasa kubwa baada ya utawala wa Saddam Hussein, dikteta wa zamani wa nchi hiyo aliyeng'olewa madarakani, kupiga marufuku kwa miaka kadhaa shughuli zote za aina hiyo. Miripuko hiyo ya kigaidi ya Karbala na Khadhimein ilitokea ikiwa ni muendelezo wa machafuko yaliyoikumba Iraq tangu nchi hiyo ivamiwe kijeshi na kukaliwa kwa mabavu na Marekani na Uingereza mwaka 2003. 

Na Miaka 61 iliyopita katika siku kama hii, nchi ya Morocco ilipata uhuru. Morocco iko kaskazini mwa Afrika katika Ukingo wa Bahari ya Mediterrania na Bahari ya Antlantic na inapakana na Algeria na Sahara Magharibi. Morocco ilikombolewa na Waislamu mwishoni mwa karne ya Saba Miladia na silsila kadhaa za kifalme zilitawala nchini humo. Mapambano ya wananchi Waislamu wa Morocco dhidi ya wakoloni wa Uhispania na Ufaransa yalipelekea nchi hiyo kupata uhuru mwaka 1956.

Bendera ya Morocco

 

Tags