Mar 11, 2017 23:35 UTC
  • Jumapili, Machi 12, 2017

Leo ni Jumapili Jamduth-Thani mwaka 1438 Hijiria, inayosadifiana na tarehe 12 Machi 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1008 iliyopita alifariki dunia Ibn Haytham, mwanafizikia, mwanahisabati na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu katika mji wa Cairo. Ibn Haytham alizaliwa mwaka 354 Hijiria katika mji wa Basra kusini mwa Iraq. Alibobea katika elimu za fizikia, tiba, falsafa na unajimu. Mwanazuoni huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vya hisabati, nujumu na tiba. Moja ya vitabu vyake muhimu ni al-Manadhir ambacho kimetafsiriwa katika lugha ya Kiingereza na kinatumika katika elimu ya nujumu.

Fizikia

Siku kama ya leo miaka 359 iliyopita alizaliwa George Berkeley, mwanafalsafa maarufu wa Ireland. Masomo yake ya msingi aliyakamilisha mjini Dublin, mji mkuu wa Ireland na baadaye akaelekea nchini Marekani ambapo akiwa huko alishiriki katika juhudi za kuasisiwa Chuo Kikuu cha Pennsylvania. Aidha Berkeley aliimba nyimbo mbalimbali katika kuisifia Marekani ambapo kutokana na hali hiyo chuo kikuu na mji mwingine mmoja katika eneo la California viliitwa kwa jina lake. Baada ya hapo Berkeley alirejea Ireland na kuteuliwa kuwa askofu na hapo akaanza kufanya utafiti kuhusiana na falsafa ya dini. Ni kwa ajili hiyo ndio maana akapata umashuhuri mkubwa katika falsafa ya dini. Kadhalika alitabahari katika elimu za jografia, akiolojia na uchumi, huku akifanya safari katika nchi mbalimbali za dunia. George Berkeley alifariki dunia tarehe 14 Januari mwaka 1753 Miladia akiwa na umri wa miaka 68.

Siku kama ya leo miaka 163 iliyopita kulitiwa saini mkataba wa kihistoria wa Constantino huko mjini Istanbul, mji mkuu wa utawala wa Othmania baina ya Ufaransa, Uingereza na utawala huo wa Othmania. Baada ya kutiwa saini mkataba huo nchi hizo zilifikia mafanikio katika kukabiliana na kupenda kujitanua kwa Urusi ya zamani barani Ulaya. Moja ya mafanikio hayo ilikuwa ni kuishinda Urusi katika vita vya eneo la Crimea. 

Siku kama ya leo miaka 154 iliyopita, alizaliwa Gabriele D'Annunzio, mwandishi wa Italia. D'Annunzio alipendelea sana kukemea urembo wa mwili. Kwa mtazamo wake urembo pekee unatakiwa uwe katika nafsi. Hata hivyo maonyesho yake ya uandishi hayakuwa na mafanikio kutokana na kushindwa kuzivutia fikra za walio wengi katika harakati hizo. Hata hivyo aliendeleza juhudi zake kubwa katika uwanja huo na hatimaye kupata umashuhuri na kufariki dunia tarehe 20 Septemba mwaka 1938 Miladia akiwa na umri wa miaka 75. 

Mahatma Gandhi

Siku kama ya leo miaka 87 iliyopita, ilianza harakati kubwa ya uasi iliyoongozwa na kiongozi wa mapambano ya uhuru nchini India Mahatma Gandhi. Harakati hiyo kubwa ambayo iliwashirikisha wazalendo na wapigania uhuru wa India, ilifanyika kwa shabaha ya kukabiliana na maamuzi mapya ya serikali ya kikoloni ya Uingereza kuhusu ongezeko la ushuru wa chumvi. Katika kukabiliana na sheria hiyo ya kidhalimu, Gandhi na wenzake elfu 78 walianza kutayarisha chumvi kutoka maji ya baharini. Wakoloni wa Uingereza walikabiliana na harakati hiyo kwa kukamata makumi ya maelfu ya Wahindi na kuwatia korokoroni. Hali hiyo ilisababisha matatizo katika kusimamia shughuli za serikali. Mapambano hayo ya Mahatma Gandhi yaliilazimisha serikali ya kikoloni ya Uingereza kusalimu amri na kulegeza misimamo yake.

Siku kama ya leo miaka 49 iliyopita nchi ndogo ya Mauritius iliyoko kusini mwa Afrika ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Waholanzi waliingia Mauritius katika karne ya 17 na wakafuatiwa na Wafaransa karne moja baadaye. Mwaka 1814 Waingereza walikivamia kisiwa cha Mauritius na kukiunganisha na makoloni yao. Kisiwa hicho kilipata uhuru mwaka 1968.

Imam Khomeini MA

Na siku kama ya leo miaka 37 iliyopita inayosadifiana na tarahe 22 Esfand 1357 Hijria Shamsia, Imam Khomeini MA mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa amri ya kuundwa taasisi ya kushughulikia masuala ya familia za mashahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini. Taasisi hiyo hadi sasa bado inaendelea kutoa huduma mbalimbali kwa familia za mashahidi wa harakati za mapinduzi vilevile familia za mashahidi wa vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran, katika kuwapatia huduma za kiutamaduni, kijamii na kiuchumi.