Mar 25, 2017 02:23 UTC
  • Jumamosi, Machi 25, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe 26 Jamad Thani 1438 Hijria mwafaka na tarehe 25 Machi 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1430 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, vita vya Dhatus Salasil vilimalizika kwa Waislamu kujipatia ushindi. Vita hivyo vilianza baada habari kusambaa kuwa kikundi cha washirikina kilitaka kushambulia mji wa Madina. Baada ya habari hiyo kumfikia Mtume Mtukufu (saw), aliwaamuru baadhi ya Waislamu waenda kukabiliana na washirikina hao wakiongozwa na kamanda mmoja aliyetoka upande wa Muhajirina. Hata hivyo baada ya kujua uwezo mkubwa waliokuwa nao maadui, kundi hilo la Waislamu lilirejea. Mtume alimtuma kamanda mwingine lakini naye pia alirejea na ndipo Mtume Mtukufu (s.a.w) alipomteua Ali bin Abi Twalib (a.s) aongoze Waislamu katika mapigano hayo. Imam Ali (as) aliwashambulia maadui kwa umahiri mkubwa na kurejea Madina na ushindi.***

Vita vya Dhatus Salasil

Katika siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, mkataba wa kuasisi Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya au kwa jina jingine Soko la Pamoja la Ulaya ulisainiwa huko Roma mji mkuu wa Italia kati ya wawakilishi wa nchi mbalimbali za bara hilo. Jumuiya hiyo iliundwa kwa lengo la kuasisi umoja wa forodha kati ya nchi wanachama ili kufuta ushuru wa bidhaa na baada ya hapo, ubadilishanaji wa bidhaa, nguvu kazi, vitega uchumi na huduma nyinginezo pia ukawa huru kati ya nchi wanachama. Jumuiya hiyo ilikuwa utangulizi wa kuundwa Umoja wa Ulaya mwaka 1992.

Bendera ya Umoja wa Ulaya

Miaka 42 iliyopita katika siku kama ya leo, Mfalme wa wakati huo wa Saudi Arabia, Faisal bin Abdulaziz, aliuawa na mwana wa ndugu yake mwenyewe, Faisal bin Saaid bin Abdulaziz. Faisal bin Saaid alifanya mauaji hayo akilalamikia kupunguzwa kwa mshahara wake. Japokuwa hitilafu katika kizazi cha wafalme wa Saudi Arabia zimekuwepo siku zote na zimekuwa zikipamba moto mara kwa mara lakini mauaji ya Mfalme Faisal yalikuwa ya kwanza ya mfalme wa nchi hiyo kutokana na hitilafu kama hizo. Muuaji wa Mfalme Faisal pia alikatwa kichwa mbele ya umati wa watu tarehe 18 Juni mwaka 1975. Baada ya Faisal, Khalid mwana mwingine wa Abdulaziz alishika kiti cha ufalme wa Saudi Arabia.***

Faisal bin Abdulaziz,

Na katika siku kama ya leo miaka 22 iliyopita, vikosi vamizi vya Marekani ambavyo mwezi Disemba 1992 viliwasili nchini Somalia kwa kisingizio eti cha kukomesha uasi nchini humo, hatimaye vililazimika kuondoka katika nchi hiyo baada ya kushindwa vibaya bila ya kutarajia. Mwaka 1991 makundi mbalimbali ya Somalia yalimpindua dikteta wa nchi hiyo Muhammad Siad Barre. Hata hivyo makundi hayo yalishindwa kufikia makubaliano ya kuunda serikali ya mseto na mkwamo huo wa kisiasa ukapelekea kuzuka vita vya ndani nchini humo. Marekani ilituma wanajeshi wake huko Somalia katika fremu ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa ili kulinda maslahi yake nchini humo, kutokana na nafasi muhimu ya Somalia katika eneo la Pembe ya Afrika. Askari wa Marekani walikabiliwa na mapambano makali ya Wasomali na kupoteza askari karibu 100.***

Somalia ilipo kijiografia