Apr 18, 2017 10:36 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (74)

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami tena juma hili katika sehemu nyingine ya mfululizo wa kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.

Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia suala la kujiweka mbali na dhambi na pamoja na mambo machafu na tulikunukulieni hadithi kadhaa zinazosisitiza juu ya umuhimu wa kujiweka mbali na dhambi na madhara ya kufanya dhambi.

Kipindi chetu cha leo kitazungumzia makundi mawili ya dhambi ndogo na kubwa na kukunukulieni hadithi zinazohusiana na maudhui hii. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki ili muweze kunufaika na yale niliyokuandalieni kwa juma hili; hii ikiwa ni sehemu ya 74 ya mfululizo huu. Karibuni.

Hadithi ya Uongofu

 

Mwenyezi Mungu anasema katika katika aya ya 31 ya Surat Nisaai kwamba:

Mkiyaepuka makubwa mnayo katazwa, tutakufutieni makosa yenu madogo, na tutakuingizeni mahali patukufu.

Aidha anasema katika aya ya 49 ya Surat al-Kahf kwamba:

Na kitawekwa kitabu. Basi utawaona wakosefu wanavyo ogopa kwa yale yaliomo humo. Na watasema: Ole wetu! Kitabu hichi kina nini! Hakiachi dogo wala kubwa ila huliandika? Na watayakuta yote waliyo yatenda yamehudhuria hapo. Na Mola wako Mlezi hamdhulumu yeyote

Kupitia aya hizi inafahamika kuwa, madhambi yamegawanyika katika makundi mawili. Dhambi kubwa na ndogo.

Dhambi maana yake ni kwenda kinyume na amri za Mwenyezi Mungu. Moja ya sababu ambazo humtumbukiza mwanadamu katika dhambi ni kudharau dhambi na kuzifanya kuwa ndogo. Kupingana na amri za Mwenyezi Mungu kwa kiwango chochote kile hata kidogo, mbele ya Mwenyezi Mungu hatua hiyo inahesabiwa kuwa ni jambo kubwa.

Ukweli ni kuwa, kama katika aya na hadithi baadhi ya dhambi zinahesabiwa kuwa ni ndogo ni kutokana na kuwa mbaya na kubwa baadhi ya dhambi ambazo ni kubwa. Kwa msingi huo, hakuna dhambi na kupinga amri ya Mwenyezi Mungu ambako kunaweza kuhesabiwa kuwa ni kudogo.

Mtume saw amenukuliwa akisema kuwa: Usiangalie udogo wa dhambi bali angalia ukubwa wa yule uliyemtendea ujeuri.

Imam Ali bin Abi Twalib as anasema kuwa: Dhambi kubwa kabisa ni yale maasi ambayo mtenda dhambi anayahesabu kuwa ni madogo.

Aidha Imam Ja’afar Swadiq as amenukuliwa akisema kuwa:

“Kitu ambacho ni shari na kibaya usikione na kukihesabu kuwa ni kidogo hata kama kwa macho yako (mtazamo wako) kitakuwa ni kidogo; na kitu cha kheri na amali njema usiihesabu kuwa ni kubwa hata kama kwa macho yako (mtazamo wako) itakuwa ni kubwa. Kwa hakika dhambi kubwa kwa kufanya istighfari sio kubwa na dhambi ndogo kwa kuendelea kuifanya sio ndogo.”

 

Kwa msingi huo basi, kuikariri dhambi ndogo, huibadilisha dhambi hiyo na kuwa kubwa. Kwa maneno mengine ni kuwa, dhambi ndogo ni mithili ya uzi mwembamba ambao kwa kuukariri na kuurejejea rejea katika kuusuka, huwa kamba ngumu na imara ambapo kuikata huwa ni jambo gumu.

Imam Ja’afar Swadiq as anasema kuwa: Katika moja ya safari za Bwana Mtume saw alishukia katika ardhi kavu isiyo na maji wala majani kisha akawaambia Maswahaba zake: Leteni kuni ili tuwashe moto ili tuweze kupika chakula. Maswaha wakamwambia Bwana Mtume saw kwamba: Hapa ni sehemu kavu na jagwa na hakuna kuni kabisa. Mtume akawaambia: Nendeni na kila mmoja atafute na kuleta kiwango chochote cha kuni atakachoweza.

Maswahaba wakatawanyika na kila mmoja akaenda upande wake na baada ya muda kila mmoja akaja akiwa na kiwango kidogo cha kuni na kisha wakazikudanya zote mbele ya Mtume na zikaonekana ni nyingi. Mtume saw akasema:  Dhambi hukusanyika namna hii. Kisha akasema: Jiepusheni na dhambi ndogo kwani zote hizo hukusanywa na kusajiliwa.

Katika sehemu nyingine Imam Swadiq as amenukuliwa akisema kuwa: Endapo dhambi itakaririwa basi huwa haihesabiwi tena kuwa ni dhambi ndogo.

Kufanya dhambi na kisha kuiona dhambi uliyoifanya ni ndogo ni mithili ya mtu ambaye anampiga mtu mwingine kwa vijiwe vidogo vidogo na kisha anayepigwa akilalamika, yeye aje na kumwambia,  vijiwe alivyompiga navyo ni vidogo na wala havikuwa na umuhimu kiasi hicho.

Kwa hakika mtu kama huyu hawezi kusamehewa, kwani maneno yake hayo yanaonyesha moyo wa ujeuri na kiburi alichonacho, kiburi ambacho kimeambatana na hali ya kujiona.

Imam Hassan Askary as, Imamu wa 11 katika mlolomgo wa Maimamu watoharifu 12 kutoka katika kizazi cha Bwana Mtume saw anasema: Miongoni mwa dhambi zisizosamejewa ni mtu kusema, yalaiti nisingeadhibiwa kwa dhambi kama hii; yaani anaiona dhambi hiyo kuwa ni ndogo.

 

Kwa hakika kuburudika kwa dhambi na kufurahia wakati mtu anapofanya dhambi hiyo, hata kama kidhahiri ni ndogo na isiyo na umuhimu ni miongoni mwa mambo yanayoifanya dhambi kuwa kubwa na kupelekea aliyetenda kupata adhabu.

Imam Ali as anasema kuwa, mtu mbaya kabisa ni yule anayefanya amali mbaya na kisha kufurahia kitendo chake hicho.

Aidha amenukuliwa katika sehemu nyingine akisema kuwa: Mtu ambaye anastaladhi na kuburudika kwa kufanya dhambi, basi Mwenyezi Mungu atampatia madhila badala ya ladha.

Kwa hakika katika mafundisho ya Kiislamu kumekatazwa na kuusiwa waumini wajiepushe na suala la kufurahia kutenda dhambi na jambo hilo kutajwa kuwa ni mbaya kuliko hata kutenda dhambi yenyewe. Imam Sajjad as anasema kuwa, jiepushe na kufurahia kutenda dhambi, kwani kitendo hicho ni kikubwa na kibaya zaidi kuliko hata kutenda dhambi yenyewe.

Kudhihirisha dhambi nayo ni hatua nyingine ambayo huibadilisha dhambi ndogo na kuifanya kuwa kubwa. Hii ni kutokana na kuwa, kudhihirisha dhambi kunapunguza adhama na ubaya wa dhambi baina ya watu na huichafua jamii na suala hilo hupelekea dhambi hiyo kuzoeleweka baina ya watu.

Imam Ali bin Abi Twalib as anasema kuwa, jiepushe na kudhihirisha dhambi kwani hatua hiyo ni dhambi kubwa kabisa.

Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia tamati ya kipindi chetu kwa juma hili. Ninakuageni nikitaraji kwamba, mtajiunga nami wiki ijayo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu wa Hadithi ya Uongofu.

Ninakuageni nikimuomba Mwenyezi Mungu atujaalie kuwa miongoni mwa wanaoogopa kutenda dhambi iwe kubwa au ndogo.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.