May 05, 2017 01:36 UTC
  • Ijumaa tarehe 5 Mei, 2017

Leo Ijumaa tarehe 8 Shaaban 1438 Hijria sawa na 5 Mei, 2017.

Siku kama hii ya leo miaka 877 iliyopita sawa na tarehe 8 Shaaban mwaka 561 Hijria alizaliwa  Ibn al-Rumiyyah mpokeaji wa hadithi, mtaalamu wa mitishamba na madawa mengineyo wa Kiislamu wa karne ya sita Hjria. Alizaliwa huko Andalusia yaani Uhispania ya leo.  Ibn al-Rumiyyah aliweza kujifunza hadithi kutoka kwa wasomi na wapokeaji hadithi wakubwa wa zama hizo baada ya kuhitimu masomo yake ya awali na kuanza kufanya utafiti katika elimu ya mitishamba pia sambamba na kujifunza masomo ya kidini. Akiwa huko Andalusia  Ibn al-Rumiyyah awali alianza kutwalii na kutambua aina mbalimbali za mitishamba na baadaye akaanza safari katika nchi mbalimbali kama vile Misri, Iraq na Hijaz. Akiwa huko msomi  Ibn al-Rumiyyah alijishughulisha na masuala ya utafiti wa mitishamba bila kusahau kujifunza masuala ya hadithi.  Ibn al-Rumiyyah aliandika vitabu vingi kuhusu masuala ya mitishamba, fiqhi na hadithi lakini kwa bahati mbaya baadhi ya vitabu vyake vimepotea.

Siku kama ya leo miaka 199 iliyopita, alizaliwa Karl Heinrich Marx mwanafalsafa wa Kijerumani na mwasisi wa nadharia ya Umaksi. Karl Marx awali alianza kusomea taaluma ya sheria na baadaye historia na falsafa. Mwanafalsafa huyo wa Kijerumani kwa muda fulani alikuwa mkuu wa jarida moja na mwaka 1848 alishirikiana na mwanafalsafa mwenzake wa Kijerumani na kubainisha imani, maoni na mitazamo yake katika kitabu alichokipa jina la "Manifesto ya Ukomonisti." Miaka miwili baadaye Marx alibaidishwa kutokana na kujishughulisha na harakati za kisiasa na hadi mwishoni mwa maisha yake makazi yake yalikuwa nchini Uingereza.

Karl Heinrich Marx

Siku kama ya leo miaka 196 iliyopita, alifariki dunia Napoleon Bonaparte mfalme aliyekuwa na nguvu wa Ufaransa, akiwa uhamishoni. Napoleon alizaliwa mwaka 1769 na kuchukua madaraka makubwa ya uongozi baada ya mapinduzi ya Ufaransa mwaka 1789, ambapo aliifanya nchi hiyo ishinde vita na nchi nyingi za Ulaya. Baada ya kuwa mfalme wa Ufaransa, Napeleon alibadilika na kuwa mtawala aliyependa kujitanua na kuzivamia nchi nyingine katika maeneo mbalimbali duniani. Kwa ajili hiyo katika kipindi cha utawala wake alipigana vita kadhaa na nchi nyingine na kukalia kwa mabavu maeneo mengi ya bara Ulaya.

Napoleon Bonaparte

Na miaka 73 iliyopita katika siku kama hii ya leo hayati Imam Ruhullah Khomeini akiwa na umri wa miaka 42, alitoa taarifa yake ya kwanza ya kisiasa akiwataka wananchi kusimama na kuanza harakati kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Katika taarifa hiyo Imam Khomeini alichunguza hali ya miaka ya nyuma, ya kipindi hicho na mustakbali wa wananchi wa Iran na Waislamu wkwa ujumla na kusema: Kuanza harakati na mapambano kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ndiyo njia pekee ya kurekebisha hali ya dunia. Alisema suala hilo ndiyo falsafa ya kutumwa Manabii wote wa Mwenyezi Mungu. Imam pia alieleza sababu za hali mbaya ya Waislamu na wananchi wa Iran na kukumbusha majukumu mazito ya wanazuoni wa dini na athari mbaya za tabaka hilo kughafilika na masuala ya kisiasa. Katika taarifa hiyo Imam Khomeini alipiga kengele ya hatari na kuwaamsha Waislamu husuan wanafunzi wa vyuo vya kidini kuhusu umuhimu wa kusimama na kuanza mapambano ya kurekebisha umma.

Imam Ruhullah Khomeini