May 24, 2017 12:14 UTC

Sura ya As-Sajdah, aya ya 1-6 (Darsa ya 738)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na Amani zimshukie Mtume wake mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Baada ya kukamilisha tarjumi na maelezo ya Sura ya 31 ya Luqman, katika darsa hii ya 738 tutaanza kuzungumzia sura ya 32 ya As-Sajdah ambayo imeteremshwa Makka. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya mwanzo hadi ya tatu ambazo zinasema:

الم

Alif Lam Mim (A.L.M.)

تَنزِيلُ الْكِتَابِ لَا رَيْبَ فِيهِ مِن رَّبِّ الْعَالَمِينَ 

Ni uteremsho wa Kitabu kisicho na shaka ndani yake kinacho toka kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.

 أَمْ يَقُولُونَ افْتَرَاهُۚ بَلْ هُوَ الْحَقُّ مِن رَّبِّكَ لِتُنذِرَ قَوْمًا مَّا أَتَاهُم مِّن نَّذِيرٍ مِّن قَبْلِكَ لَعَلَّهُمْ يَهْتَدُونَ

Au wanasema: Amekizua? Bali hicho ni Haki itokayo kwa Mola wako Mlezi, ili uwaonye watu wasio fikiwa na mwonyaji kabla yako; huenda wakaongoka.

Sura hii pia ni miongoni mwa sura 29 za Qur’ani zilizoanza kwa herufi za mkato. Kama ilivyo Suratul Baqarah, ambayo imeanza kwa herufi za alif lam mim, aya ya mwanzo ya Suratus Sajdah pia imeanza kwa herufi hizo. Aya inayofuatia inaonyesha kuwa herufi hizi zinahusiana na uteremshwaji wa Qur’ani; na zinabainisha adhama ya Kitabu ambacho kimeandikwa kwa herufi hizi hizi za alfabeti za Kiarabu, lakini upangaji wa maneno na ibara zake umefanywa kwa namna ambayo hakuna mwanaadamu yeyote mwenye uwezo wa kuleta kitabu chengine kilicho mfano wake.

Kitabu ambacho chimbuko lake ni haki na hakuna chochote kilichomo ndani yake isipokuwa haki, hakika na ukweli. Pamoja na hayo bila ya shaka wapinzani na wakanushaji, ambao hawako tayari kukikubali, wanamtuhumu Bwana Mtume Muhammad SAW kuwa aya za Qur’ani ni kitu alichotunga na kujibunia yeye mwenyewe kisha akazinasibisha na Mwenyezi Mungu. Ilhali yeye Mtume hana lengo jengine ghairi ya kuonya na kutoa indhari ili kuwahofisha watu juu ya matokeo mabaya ya amali chafu na matendo maovu wanayofanya, kwamba asaa, huenda wakajiweka mbali na maovu na maasi na kufuata njia iliyonyooka ya uongofu. Baadhi ya mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hizi ni kwamba japokuwa wakanushaji haki wanajaribu kueneza shaka na shubha kuhusiana na Qur’ani lakini hakuna shaka ya aina yeyote  kuhusu ukweli wa Qurani, kwa sababu kitabu hicho kinatoka kwa Muumba na Mola wa walimwengu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Qur’ani ni kitabu cha hukumu za sharia; na mpangaji wa sharia za kitabu hicho ndiye mletaji wa mfumo wa ulimwengu wa maumbile. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kuonya na kutoa indhari ili watu wajihadhari na kujiweka mbali na dhalala na upotofu ni miongoni mwa malengo makuu ya kutumwa Mitume na Manabii.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya nne ambayo inasema:

 اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ مَا لَكُم مِّن دُونِهِ مِن وَلِيٍّ وَلَا شَفِيعٍ أَفَلَا تَتَذَكَّرُونَ

Mwenyezi Mungu ndiye aliyeziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yao kwa siku sita, kisha akatawala kwenye Arshi. Nyinyi hamna walii wala mwombezi isipokuwa Yeye. Basi, je, hamkumbuki? 

Baada aya zilizotangulia zilizozungumzia kuteremshwa Qur’ani na Allah SW, aya hii inaashiria uumbaji wa ulimwengu ambao pia ni kazi yake Mola. Kama ambavyo katika kuiteremsha Qur’ani hakuwa na mshirika yeyote bali aya zote za kitabu hicho ameziteremsha yeye Allah, katika uumbaji wa ulimwengu pia Yeye Mola hakushirikiana na yeyote bali vyote vilivyomo ndani ya ulimwengu wa maumbile mbinguni na ardhini vimeumbwa kwa irada na takdiri yake. Aidha kama ambavyo aya za Qur’ani aliteremshiwa hatua kwa hatua Bwana Mtume Muhammad SAW kwa muda wa miaka 23, uumbaji wa dunia pia umefanyika hatua kwa hatua katika awamu sita ambazo tab’an yamkini kila moja kati ya awamu hizo ilichukua muda mrefu.

Kwa masikitiko ni kwamba watu wengi, badala ya kuzingatia uumbaji na utawala mutlaki wa Mwenyezi Mungu wanaviendea viumbe vyake na kuvichukulia kuwa ni walinzi au waombezi wao. Hali ya kuwa ghairi ya mawalii wa Allah, ambao wanaombea na kutakia shufaa kwa idhini yake Mola, hakuna kitu wala mtu yeyote mwenye uwezo wa kumuombea na kumshufaia mwanadamu mwenzake na kuwa sababu ya yeye kusamehewa madhambi yake au kuwa wasita na kiunganishi cha kupatia neema za Mola.

 Kutokana na aya hii tunajifunza haya yafuatayo:-

Mosi, tadbiri na uendeshaji wa masuala ya ulimwengu yako mikononi mwa yule yule aliyeumba ulimwengu wenyewe. Kwa maneno mengine, si kwamba baada ya kuumba ulimwengu, Yeye Muumbaji aliamua kuuacha tu kama ulivyo au kukabidhi mamlaka ya uendeshaji wake kwa viumbe wake.

Na pili ni kwamba, mwanaadamu anahitajia mawaidha na ukumbusho juu ya neema za Mwenyezi Mungu, la sivyo atajisahau na kupatwa na mghafala.

 Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya tano na ya sita ambazo zinasema:

يُدَبِّرُ الْأَمْرَ مِنَ السَّمَاءِ إِلَى الْأَرْضِ ثُمَّ يَعْرُجُ إِلَيْهِ فِي يَوْمٍ كَانَ مِقْدَارُهُ أَلْفَ سَنَةٍ مِّمَّا تَعُدُّونَ 

Hulipanga jambo kutoka mbinguni hadi ardhini, kisha linapanda kwake katika siku ambayo kipimo chake ni miaka elfu kwa mnavyo hisabu nyinyi.

ذَٰلِكَ عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ

Huyo ndiye mjuzi wa mambo ya ghaibu na ya dhahiri. Asiyeshindika, Mwenye kurehemu.

Aya hizi zinaendeleza maudhui ya aya iliyotangulia kuhusu tadbiri ya Allah katika mfumo wa ulimwengu na kutilia mkazo tena nukta hiyo kwa kueleza kwamba: Ulimwengu mzima wa uumbaji, kuanzia mbinguni hadi ardhini uko chini ya tadbiri yake na hakuna mwendeshaji mwengine yeyote ghairi yake Yeye. Haendeshi masuala ya ulimwengu huu tu bali mambo yenu na amali zenu zote mnazofanya zitarejea kwake Yeye Mola wenu Siku ya Kiyama; na hakuna kitu chochote kinachoweza kutoka nje ya mamlaka ya nguvu, elimu na ujuzi wake Mola. Makusudio ya siku ambayo katika hisabu ya wanaadamu ni sawa na miaka elfu moja ni Siku ya Kiyama. Chochote kile kitakachojiri hadi mwisho wa dunia kitadhihirishwa siku hiyo katika mahakama ya Mwenyezi Mungu; na Yeye Mola, ambaye ni mwenye ujuzi wa mambo yote ya siri na ya dhahiri, unaotokana na elimu yake isiyo na kikomo, ataamiliana na waja wake kwa msingi wa izza na rehma. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Muumbaji,  Mtawala wa Mwendeshaji wa Ulimwengu mzima ni mmoja tu; na tauhidi halisi ni kuyarejesha mambo yote kwa Allah SW. Kama ambavyo katika uumbaji, kila kitu kinarejea kwake Yeye, uendeshaji wa mambo yote pia uko mikononi mwake na unarejea kwake Yeye Mola. Funzo jengine tunalolipata kutokana na aya hizi ni kuwa tadbiri na uendeshaji mambo ya ulimwengu na kanuni zinazotawala juu yake zinatokana na elimu isiyo na mwisho wala kikomo ya Mwenyezi Mungu: Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba elimu ya Allah ni ya hali moja kuhusiana na mambo yote, yawe yanayoonekana au yaliyofichikana. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 738 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atughufirie madhambi yetu, atukubalie dua zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.