May 28, 2017 11:15 UTC

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya sita ya makala yanayozungumzia jinai na ukatili wa kutisha unaofanywa na Mabudha wenye kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar.

Kuna ushahidi na nyaraka nyingi zinazothibitisha jinai na ukatili wa kijinsia unaofanywa kila uchao na askari na Mabudha wenye kufurutu mpaka nchini Myanmar dhidi ya wanawake na mabinti wa Kiislamu wa Rohingya, nyaraka ambazo zimetokana na mahojiano na Waislamu hao ambao sasa wamekimbilia nchini Bangladesh. Kwa mujibu wa ripoti hizo, askari na polisi wa Myanmar wametekeleza jinai hizo za ukatili na ubakaji katika zaidi ya vijiji tisa vya jamii ya watu hao.

Watu wa jamii ya Rohingya

Kufuatia hali hiyo, shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch limeitaka serikali ya Myanmar kuwachukulia hatua kali makamanda wa jeshi waliotoa amri ya kubakwa na kudhalilishwa kijinsia wanawake na mabinti wa Kiislamu wa Rohingya. Kwa mujibu wa chanzo kimoja cha habari kilicholinukuu shirika hilo la kutetea haki za binaadamu, jinai hizo za ubakaji hazikutokea ghafla tu, bali ni katika sehemu ya mashambulizi ya kimfumo na yaliyoratibiwa kikamilifu dhidi ya jamii ya wachache ya Rohingya, hujuma ambazo zinasukumwa na mirengo ya kidini. Hata hivyo kile ambacho kimewashangaza wengi ni kimya cha jamii ya kimataifa hususan Umoja wa Mataifa na kadhalika mashirika yanayojinadi kuwa watetezi wa haki za wanawake duniani.

Wakimbizi wa jamii ya Rohingya wakijaribu kuokoa nafsi zao

Katika hilo asasi hizo hazijasikika zikitoa tamko lolote dhidi ya jinai hizo za kutisha zilizowakumba wanawake wa Kiislamu na wasio na hatia wa nchini Myanmar kutoka kwa watawala wa serikali ya nchi hiyo ya kibaguzi. Kuna faida gani ya kuwepo mashirika kama hayo yanayodai kutetea haki za binaadamu na wanawake, katika hali ambayo jinai kubwa kama hizo dhidi ya wanawake wa Kiislamu huko Myanmar haziakisiwi wala kulaaniwa na asasi hizo?

***********************************

Ndugu wasikilizaji tunapaswa kufahamu kwamba, mateso yanayowakabiliwa Waislamu wa jamii ya Rohingya hayakutekelezwa siku, wiki na miezi ya hivi karibuni pekee, bali ni ya muda mrefu ambayo yanarejea nyuma kwa miongo kadhaa iliyopita tangu kulipoibuka wimbi la ubaguzi na mauaji ya kimbari dhidi ya wafuasi wa dini hii ya mbinguni.

Wanawake wa Kiislamu wa Rohingya wakiwa wamehifadhiwa

Licha ya Waislamu wa Myanmar kuundwa na jamii ya mamilioni ya watu wanaokadiriwa kuwa zaidi ya milioni 15, lakini serikali ya Myanmar imekataa kabisa kuwatambua watu wa jamii hiyo ya wachache kuwa raia wazalendo wa nchi hiyo. Mwaka 1982 serikali ya Myanmar ilifuta uraia wa watu wa jamii hiyo, suala ambalo lilienda sambamba na kuwanyima haki zao za kimsingi za kiraia. Sheria hiyo iliwazuia watoto wa jamii hiyo kwenda shule, kuzuiliwa huduma za kijamii kama vile mahospitali na kuwapokonya mali zao zikiwemo fedha zilizokuwa zimewekwa kwenye mabenki ya nchi hiyo. Ni kwa msingi huo ndio maana hata Umoja wa Mataifa ukaitaja jamii ya Waislamu wa Rohingya kuwa jamii iliyodhulumiwa na kubaguliwa zaidi duniani. Hii ni kusema kuwa, tangu kulipopitishwa sheria mpya ya uraia nchini Burma mwaka 1982 hadi sasa watu wa jamii hiyo wamenyimwa kabisa haki za uraia na katika kipindi chote hicho, wamekuwa wakishambuliwa na kuuawa na askari wa serikali pamoja na Mabudha.

Hali mbaya wanayoishi nayo watu wa jamii ya Rohingya

Hii ni kwa sababu serikali ya Myanmar haiwatambui Waislamu hao kama raia wa nchi hiyo sambamba na kuwatuhumu kuwa ni 'wahajiri haramu.' Kwa mujibu wa ripoti ya mtandao wa 'Myanmarmuslims.org' awali ukatili dhidi ya Waislamu wa Rohingya ulianzia huko magharibi mwa nchi na kuenea taratibu katika maeneo mengine ya nchi hiyo.

Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni mbali na Bangladesh, maelfu ya Waislamu hao wamelazimika kukimbilia nchi jirani za Thailand, Malaysia na Indonesia, kutokana na sera za ubaguzi wa kutisha zinazotekelezwa na serikali ya nchi hiyo. Katika harakati hizo za kukimbia, Waislamu hao hutumia usafiri hatari wa mitumbwi isiyo salama, ambayo aghlabu huzama katika maji.

Haya ndio maisha ya wakimbizi wa Myanmar huko Bangladesh

Kwa msingi huo ni idadi ndogo tu ya Waislamu hao waliofanikiwa kufika pwani za mataifa hayo matatu, huku wengi wakipoteza maisha kwa sababu tofauti zikiwemo za kuzama maji, njaa kali na maradhi. Huku hali ikiwa ni hiyo kwa wale waliokimbia, wale waliosalia nchini Myanmar nao hawakusalimika hata kidogo kutokana na ukatili na ukandamizaji wa kuchupa mipaka wa serikali ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa tathmini iliyotolewa na kamisheni ya uchunguzi wa masuala ya wakimbizi ya Umoja wa Mataifa, katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzoni mwa mwaka 2015 zaidi ya watu elfu 25 wa jamii ya Rohingya, walilazimika kutoroka nchi hiyo kwa kutumia mitumbwi, kwenda Bangladesh. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, chanzo cha jamii ya watu hao kuondoka nchini mwao, ni siasa za ukandamizaji na ubaguzi za Mabudha wa kuchupa mipaka. Katika miaka ya hivi karibuni serikali ya nchi hiyo imeshadidisha ukandamizaji dhidi ya Waislamu wa Rohingya kiasi cha kuwafanya walazimike kuihama nchi yao. Aidha tangu mwaka 2012 jamii ya watu wa Rohingya imekuwa ikishuhudia mlolongo wa hujuma na udhalilishaji mkubwa pamoja na mauaji ya umati dhidi yake.

Zeid bin Ra'ad Zeid al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu

Vijiji, shule na misikiti nayo haikusazwa katika mashambulizi ya uchomaji moto wa Mabudha na askari wa serikali ya nchi hiyo. Katika matukio hayo idadi kubwa ya Waislamu waliuawa na wengine karibu laki moja na elfu 40 kusalia bila makazi. Ripoti iliyotolewa mwezi Septemba mwaka jana na shirika la kujitegemea la ‘Taasisi ya Kusimamia Usitishaji Mauaji ya Umati’ ilisema kuwa, ukatili wa hivi karibuni ulivuka kiwango cha mauaji ya umati na kufikia hatua ya maangamizi ya kizazi katika maeneo yote ulikojiri.

*******************************

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako kipindi kilichoko hewani ni Makala ya sita yanayozungumzia jinai za Mabudha makatili wanaowalenga Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar.

Watoto wa jamii ya Rogingya wakisomea katika mazingira mabaya sana

Kama tuolivyosema ni kwamba, hadi sasa makumi ya maelfu ya Waislamu wa jamii ya wachache wa Rohingya wamelazimika kuihama nchi yao na kwenda uhamishoni kutokana na ukatili wa kuchupa mipaka wa serikali. Hii ni kusema kuwa, karibu watu elfu 70 miongoni mwa Waislamu hao wamewasili nchini Bangladesh katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni. Hata hivyo Bangladesh kama zilivyo nchi nyingine jirani, haikuwa tayari kuwapokea watu hao wanaodhulumiwa kuingia ardhi yake. Hadi sasa, serikali ya Dhaka, bado inafikiria kuwahamisha Waislamu hao na kuwaweka katika kisiwa cha mbali, licha ya kutolewa tahadhari mbalimbali juu ya hatari ya kisiwa hicho na kutokuwa kwake na mazingira mazuri ya kuishi binaadamu na vilevile kukabiliwa na hatari ya mafuriko ya kila mara. Pia akthari ya Waislamu hao wa Rohingya wanaishi katika kambi za wakimbizi. Hii ni katika hali ambayo kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), kambi hizo hazina nyenzo za msingi kwa ajili ya maisha kama vile chakula, maji na madawa. Kwa kuzingatia kuwa Malaysia ni nchi ya Kiislamu inayohitajia nguvukazi kubwa, hivyo katika kipindi chote hiki, nchi hiyo imekuwa chaguo la kwanza kwa watu wa Rohingya.

Wahajiri wa Rohingya wakilia njaa kali ndani ya boti

Aidha Malaysia ilitangaza kupokea Waislamu hao wa Rohingya elfu 45 na sasa haiko tena tayari kupokea idadi zaidi ya hiyo kutokana na ongezeko kubwa la wakimbizi wa jamii hiyo. Katika wiki za hivi karibuni na baada ya Malaysia kuzuia kuingia nchini humo mitumbwi iliyowabeba wakimbizi hao, Indonesia imekuwa chaguo la pili kwa ajili ya kuelekezwa huko mitumbwi ya wakimbizi hao. Hata hivyo hatua ya serikali ya Indonesia ya kutuma meli za kivita katika maji yake, imeizuia mitumbwi ya wakimbizi hao kuingia nchi hiyo. Ndugu wasikilizaji, Thailand ni nchi nyingine ambayo imeshuhudia kuwasili wakimbizi wa Rohingya wanaojaribu kuokoa maisha yao kutokana na hujuma za serikali ya Myanmar. Hata hivyo haijakuwa rahisi kwa watu hao kuweza kuingia ardhi ya nchi hiyo. Kwani wafanyamagendo ya binadamu ambao wamekuwa wakipewa pesa na Waislamu hao ili waweze kuwafikisha nchini Thailand, wamekuwa wakiwaacha katikati ya maji bila chakula wala maji ya kunywa. Katika hali hiyo, wakimbizi wale wa Rohingya wamekuwa wakichukua wiki kadhaa katika maji baina ya Thailand, Malaysia na Indonesia wasijue pa kwenda.

Mabudha wakatili wanaohusika katika jinai dhidi ya Waislamu wa Rohingya

Kwa mujibu wa ripoti, mamia ya watu wamepoteza maisha yao katika hali hiyo ya kutisha ambapo hata baadhi ya vyombo vya habari vimesambaza picha za wahanga hao.

******************************

Wasikilizaji wapenzi kitendo cha kuwafanya Waislamu wa Rohingya kuwa wakimbizi huko Bangladesh au kwenda kwao nchi nyingine za jirani, kimefanya hali ya maisha ya watu hao kuwa ngumu sana. Ni kwa kuzingatia kuharibika zaidi hali ya Waislamu hao katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, ndio maana maelfu ya Waislamu hao wakajaribu kuelekea nchi nyingine kupitia njia hatari zaidi katika bahari ya Mediterranean.

Ndugu wasikilizaji sehemu ya sita ya makala haya yanayozungumzia jinai na ukatili wa kutisha unaofanywa na Mabudha wenye kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar inamalizikia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, Was-Salaamu Alaykum Warahmatullahi wa Barakaatu…………//

 

Tags