May 28, 2017 11:23 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya saba ya makala yanayozungumzia jinai na ukatili wa kutisha unaofanywa na Mabudha wenye kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia wimbi la uhajiri wa jamii ya Waislamu wa Rohingya kwenda mataifa ya jirani na Myanmar kwa ajili ya kupata maisha mazuri. Uhajiri ambao hata hivyo huambatana na matatizo mbalimbali ikiwemo kupoteza maisha baharini. Leo pia tuendelea kubainisha suala hilo. Kwa mujibu wa ripo za Umoja wa Mataifa, tangu mwaka 1978 jamii ya wachache wa Rohingya imekuwa inakabiliwa na ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu chini ya utawala wa kidikteta na kijeshi wa Burma ambapo matokeo yake ni kwamba akthari ya Waislamu hao wamelazimika kukimbilia mataifa ya jirani na nchi hiyo hususan Bangladesh.

Sababu kuu ya Waislamu hao kuhajiri kwenda Bangladesh ni mazingira mabaya yanayotawala nchini Myanmar ambayo yanasababishwa na viongozi wa serikali ya nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo mazungumzo ya pande mbili baina ya Bangladesh na Myanmar yangeweza kwa kiasi fulani kupunguza machungu yanayowakabili Waislamu hao wa nchini Myanmar. Kuwa na historia yenye kufanana kama vile rangi, ukaumu na utamaduni kuliopo kati ya watu wa Bangladesh na Burma kungeweza kuwashawishi viongozi wa serikali ya Dhaka kufanya juhudi zaidi kwa lengo la kumaliza tatizo hilo la Waislamu wa Myanmar. Kamiesheni ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa kupitia ripoti ya kurasa 43 na kwa mujibu wa mahojiano iliyoyafanya na wakimbizi wa Rohingya wanaoishi nchini Bangladesh, ilieleza kwa namna ya uwazi sana vitendo visivyo vya kibinaadamu vya Mabudha na askari wa serikali ya Myanmar dhidi ya watu wa jamii hiyo.

Jamii ya Waislamu wa Rohingya wakijaribu kukimbia

Ripoti hiyo ambayo iliandaliwa kwa kuzingatia mahojiano yaliyofanywa na wakimbizi 220 wa Rohingya, ilikusanywa kutoka kwa Waislamu wa maeneo manane tofauti. Kamisheni hiyo ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa ilijiridhisha kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa kujiri jinai zaidi dhidi ya binaadamu nchini Burma. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, miongoni mwa Waislamu waliouawa, ni watoto wadogo wasio na hatia akiwemo mtoto mwenye miezi sita aliyeuawa kwa kukatwa shingo na Mabudha, huku mama wa mtoto huyo naye akinajisiwa na askari watano wa serikali ya nchi hiyo ya kidikteta.

Zeid Ra'ad Zeid Al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu

Zeid Ra'ad Zeid Al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu sambamba na kulaani jinai hizo amesema: "...Ni jeshi gani duniani ambalo linaweza kufanya vitendo vilivyo dhidi ya ubinaadamu aina hiyo? Ni aina gani ya maangamizi haya?" Mwisho wa kunukuu. Baada ya kuorodhesha jinai za kutisha za Mabudha wenye misimamo ya kigaidi na ubaguzi kwa kushirikiana na jeshi la serikali, Zeid Ra'ad Zeid Al-Hussein alisema: "Ni aina gani ya chuki ambayo mtu anaweza kumuua hata mtoto mdogo anayelilia maziwa ya mama yake na kisha kumbaka kwa aina ya kutisha zaidi mama yake?" Mwisho wa kunukuu.

****************************************

Ndugu wasikilizaji ni vyema mkafahamu kwamba, mwaka huu wa 2017 ni mwaka ambao kumeshuhudiwa aina mpya ya biashara ya utumwa. Suala ambalo linakumbushia historia ya kutisha ya Marekani katika kuwafanya watu wengine kuwa watumwa kipindi cha mwaka 1700.

Watumwa hao sio mateka wanaotoka barani Afrika, bali ni mabinti, wanawake, watoto na wanaume wa kabila la Rohingya wa jamii ya wachache ya Waislamu ambao kutokana na kukabiliwa na ubaguzi wa hali ya juu wa serikali ya Myanmar, wamelazimika kukimbia nchi yao. Hii ni kusema kuwa, watu wa jamii hiyo wanaishi katika mazingira magumu sana nchini Myanmar huku kila siku wakikumbwa na mashambulizi ya kutisha ya Mabudha na askari wa serikali ya taifa hilo, ambapo ili kuokoa nafsi zao hulazimika kukimbia ardhi zao na kwenda nchi nyingine za ughaibuni. Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, na kutokana na kushtadi vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya watu wa jamii hiyo na kwa kuzingatia mazingira magumu yaliyopo katika kambi za wakimbizi wanazoishi nchini Burma, zaidi ya watu laki moja na elfu 20 miongoni mwao walilazimika kukimbia kutoka nchi hiyo. Hii ikiwa na maana kwamba, kila Warohingya 10 mmoja wao amekuwa mkimbizi nje ya nchi.

Katika harakati hizo kwa kawaida watu hao hulazimika kutoa kiasi cha Dola 200 hadi 300 kwa wafanya magendo ya binaadamu ili kwa njia hiyo wafanya magendo hayo waweze kuwasaidia kuwatorosha kutoka Myanmar kwenda nchini Thailand na kisha kupitia nchi hiyo kwenda Malaysia na hata Indonesia. Kwa kawaida baada ya watu wa jamii hiyo kuingia Thailand huishi katika kambi za siri za wafanya magendo hao katikati ya misiti mikubwa ya nchi hiyo, wakisubiria kusafirishwa kwenda nchi nyingine. Tunaweza kusema kuwa, Thailand ni njia kuu ya usafirishaji inayotumiwa na wafanya magendo wanaowasafirisha watu wa jamii ya Rohingya kwenda Malaysia.

******************************

Gazeti la Hindu, linalochapishwa nchini India limeandika katika ripoti yake kwa kumnukuu mmoja wa wakazi wanaoishi katika mji wa Shah Peoria Duwap ulio mpakani na Bangladesh akisema kuwa kwa miaka yote iliyopita na kutokana na kukithiri mashambulizi ya Mabudha wenye kufurutu mipaka dhidi ya jamii ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar  na pia kuongezeka wimbi la wahajiri wanaoelekea katika maeneo  hayo ya mpakani kunakoenda sambamba na kuenezwa propaganda za wafanya magendo ya binaadamu kwa ajili ya kuwapeleka watu wa jamii hiyo kwenda nchi za Asia ya kusini mashariki kwa madai eti ya kupata maisha mazuri, ni mambo yaliyosababisha kuongezeka kwa biashara ya magendo hayo hatari.

Aidha katika miaka ya hivi karibuni, harakati za magendo katika mji huo mdogo wa mpakani, sambamba na mashinikizo mengi kuwalenga Waislamu na pia propaganda zinazofanywa na wafanya magendo hayo ya binaadamu kwamba wanaweza kuyaboreshea maisha watu wa jamiiya Rohingya kwa kuwavusha kwenda mataifa hayo ya kusini mashariki mwa Asia, zimeubadili muundo wa eneo hilo kutokana na taathira yake kwenye maisha ya kawaida ya wakazi wake. Uzingatiaji wa jamii ya dunia kuhusiana na magendo ya binaadamu katika eneo hilo la mpakani ulichukua nafasi yake baada ya tukio la kuzama baharini kwa boti moja ambalo kidhahiri lilionekana kuwa la wavuvi huku miili mingi ya wahanga ikiokotwa wakati ikielea juu ya maji. Kwa mujibu wa serikali ya Bangladesh karibu wahajiri elfu 32 wa Rohingya bado wanaishi katika kambi ndogo ya wakimbizi kusini mashariki mwa nchi hiyo, katika mpaka na nchi ya Burma. Katika sehemu nyingine ya ripoti ya gazeti la Hindu linalochapishwa nchini India imeelezwa kuwa, awali magendo ya binaadamu katika mji huo wa Shah Peoria Duwap yalianza baada ya watu kuingiwa na dhana kwamba, kupata maisha bora au kazi inawabidi kufanya safari katika nchi zilizoendelea kama vile Malaysia, Thailand na Singapore.

Wanawake wa Rohingya wakiwa katika mitumbwi kuokoa nafsi zao

Hivi sasa biashara hiyo imegeuka na kuwa moja ya kazi kubwa ya magenge ya wafanya magendo. Magenge hayo  yanatumia vibaya mashinikizo na mashambulizi ya Mabudha na askari wa serikali ya Burma dhidi ya Waislamu, kuwapakia wahajiri hususan Waislamu wa Rohingya ambao wanakimbia hali mbaya ya maisha na kuokoa nafsi zao kutokana na kuuawa katika boti zisizokuwa na viwango vya kubeba idadi kubwa ya watu. Hata wakati mwingine wafanya magendo hao huwashawishi watu wa familia ambazo ndugu zao waliwahi kufanikiwa kufika nchi hizo ili nao waweze kujiunga na safari hizo ambazo aghlabu hukatisha maisha yao baharini kutokana na kuzama maji. Ukweli ni kwamba uhajiri wa umati wa Waislamu wa Rohingya umegeuka na kuwa mgogoro mkubwa wa kibinaadamu katika eneo la kusini mwa Asia. Kugunduliwa kwa makaburi ya umati katika kambi za magenge yanayoendesha magendo ya binaadamu huko nchini Thailand baina ya mpaka wa taifa hilo na Malaysia na kadhalika vitendo visivyo vya kibinaadamu vya wafanya magendo hao ikiwa ni pamoja na kuwanyima maji na chakula wahajiri waliowachukua kutoka Myanmar na Bangladesh, kimevutia hisia za jamii ya walimwengu kwa lengo la kutaka kuzuia mwenendo huo.

Wakiwa katika boti huku wakilia njaa

Hata hivyo hali ikiwa hivyo, wimbi la magendo hayo ya binaadamu linaonekana kushika kasi siku hadi siku. Hii inatokana kwamba, ili kuwasafirisha wahajiri hao masikini kuwapeleka katika nchi za kusini mashariki mwa Asia, wahajiri hao hulazimika kuwapatia wafanya magendo hao kiasi cha Dola 200-300. Hata hivyo na licha ya wahajiri hao kutoa kiasi chote hicho cha fedha, wafanya magendo hao huwatelekeza baharini peke yao bila kuwapa chakula wala maji ya kunya na kuwafanya akthari yao kupoteza maisha.

*************************************

Baadaye wafanya magendo hao ya binaadamu huzifuata tena familia za wahajiri na kuomba kiasi kikubwa cha fedha kinachokadiriwa kati ya Dola 2000-3000 na kuzihadaa familia hizo kwamba endapo zitatoa kiasi hicho basi wataweza kuwafikisha ndugu zao nchini Malaysia, Thailand au Singapore. Aidha wakati mwingine wafanya magendo hao, huwaomba pesa zaidi wahajiri hao katikati ya safari.

Bibi wa jamii ya Rohingya akiomba dua ili Allah awapunguzie machungu

Na kwa kuzingatia kuwa aghlabu ya familia za jamii ya Rohingya ni masikini zisizoweza kudhamini kiasi hicho cha fedha, huamua kuwaozesha kwa lazima watoto wao wa kike kwa wafanya magendo mkabala na kulipa fedha hizo, hususan kwa wasichana wahajiri. Wasichana hao hulazimika kukubali ndoa hizo kinyume na matakwa yao kwa kuwa ndugu zao hawana uwezo wa kudhamini kiasi hicho cha fedha ili kuwafikisha mahala wanapokusudia kwenda. Na wakati mwingine wasichana hao hugeuzwa na kuwa watumwa wa ngono na watu wa magenge hayo hatari. Ni kwa ajili hiyo ndio maana wasichana hao wa Rohingya hufadhilisha kufunga ndoa kinyume na irada yao na watu hao wakatili ili tu kujiepusha na kukumbwa na hatma mbaya zaidi ya kufanywa watumwa wa ngono.

Wakiwa wametiwa jela

Kuhusiana na suala hilo, Ambiya Khatou, binti wa Rohingya anasimulia kwa kusema: “Wafanya magendo ya binaadamu walitupeleka Thailand. Hata hivyo kwa kuwa hatukuwa na pesa za kutosha za kuwapatia, walituweka katika mnada ili kutuuza kama bidhaa. Alijitokeza mwanamume mmoja raia wa Malaysia ambaye alikuwa tayari kutulipia fedha tulizokuwa tunadaiwa na wafanya magendo wale. Licha ya kwamba mwanamume huyo alikuwa mzee, mama yangu aliridhia niolewe kwa nguvu na mwanamume huyo kwani hatukuwa na mtu mwengine ambaye angeendelea kutuhudumia huko ugenini. Inapotokea mtu mwenye uwezo wa kifedha kwa ajili ya kuwaachilia huru wasichana hao kutoka mikononi mwa wafanya magendo hao, basi huweza kununua idadi kadhaa ya wasichana awatakao na kuwatumia. Hata hivyo hivyo vinafanyika mbele ya kimya cha jamii na asasi zinazojinadi kuwa watetezi wa haki za binaadamu.” Mwisho wa kunukuu.

Ndugu wasikilizaji sehemu ya saba ya makala haya yanayozungumzia jinai na ukatili wa kutisha unaofanywa na Mabudha wenye kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar inakomea hapa. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./

 

 

 

 

Tags