Alkhamisi 8 Juni, 2017
Leo ni Alkhamisi tarehe 13 Ramadhani 1438 Hijria, sawa na 8 Juni, 2017.
Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel, Mossad, lilifanya mauaji ya kigaidi dhidi ya kiongozi mwingine wa Kipalestina katika moja ya nchi za kigeni. Siku hiyo maajenti wa Mossad walimuuwa Atef Bseiso mmoja wa viongozi wa usalama wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) huko Paris, Ufaransa. Licha ya kwamba hakukuwepo shaka juu ya kuhusika utawala wa Kizayuni katika mauaji hayo, lakini utawala huo ghasibu ulikana kufanya jinai hiyo ya kinyama kwa kuhofia hasira za walimwengu. Hata hivyo miaka saba baadaye, polisi ya Ufaransa ilitangaza kwamba shirika hilo la ujasusi la Israel Mossad ndilo lililopanga na kutekeleza mauaji hayo.
Tarehe 8 Juni miaka 122 iliyopita, alizaliwa Said Nafisi, mwandishi na mtarjumi wa kisasa wa nchini Iran hapa mjini Tehran. Nafisi alikuwa mtoto wa Ali Akbar Nafisi, maarufu kwa jina la Nadhim al-Atwibbai, msomi na mwandishi wa kitabu cha ‘Tamaduni ya Thamani’. Baada ya kumaliza masomo yake ya awali, Ustadh Said Nafisi alikamilisha masomo yake katika taaluma za sheria na elimu ya siasa. Nafisi alijishughulisha na ukufunzi katika taaluma za historia na fasihi huku akiwa mmoja wa wanaharakati wa utamaduni nchini Iran. Mbali na Iran, Ustadh Said Nafisi alikuwa na uanachama katika taasisi mbalimbali za kiutamaduni na katika vyuo vikuu vya nchi kadhaa za Ulaya na Asia.
Katika siku kama ya leo miaka 162 iliyopita, mji wa Lisbon ambao ni mji mkuu wa Ureno uliharibika, kutokana na mtetemeko mkubwa wa ardhi na moto uliosababishwa na zilzala hiyo. Karibu wakazi elfu arubaini wa mji huo walipoteza maisha yao na theluthi mbili ya nyumba na taasisi za kiuchumi za mji huo kubomolewa. Mbali na maafa hayo, karibu meli elfu mbili, boti na ngalawa nyingi zilizokuwa katika bandari za Ureno zilizama. Mtetemeko huo ni moja ya mitetemeko mikubwa zaidi kuwahi kuikumba Ureno.
Siku kama ya leo miaka 187 iliyopita kiberiti kilivumbuliwa nchini Ujerumani. Mvumbuzi wa kiberiti hicho alijulikana kwa jina la Camberz. Tofauti kubwa ya kiberiti hicho cha awali na kile kinachotumiwa hivi sasa ni uwakaji wake uliokuwa wa taratibu. Baada ya Camberz walijitokeza watafiti wengine waliofanya utafiti wao kuhusiana na kiberiti, na hatimaye Phillips raia wa Marekani alifanikiwa kutengeneza kiberiti kama kile kinatumika leo hii.
Na siku kama ya leo miaka 1343 iliyopita inayosadifiana na tarehe 13 Ramadhani mwaka 95 Hijria, alifariki dunia Hajjaj bin Yussuf Thaqafi, liwali katili na dhalimu katika kipindi cha utawala wa Bani Umayyah. Hajjaj bin Yussuf Thaqafi aliishi katika kipindi cha Abdul Malik Marwan na Hisham bin Marwan, na alikuwa mashuhuri kwa kuwatesa na kuwauwa wapinzani wa utawala wa Bani Umayyah, hasa wafuasi wa Imam Ali bin Abi Talib AS na watu wa familia ya Mtume Mtukufu Muhammad SAW. Baadhi ya wanahistoria wameandika kuwa, zaidi ya watu 120,000 waliuawa kutokana na amri iliyotolewa moja kwa moja na Hajjaj bin Yussuf Thaqafi. Miongoni mwa jinai zilizowahi kufanywa na Hajjaj Thaqafi ni pamoja na kushambulia mji mtakatifu wa Makka na kuharibu al Kaaba katika mwaka 74 Hijria.