Wasudani elfu 343 wamekimbia makazi yao, 503 wameuawa huko Al-Hilalia
(last modified Sat, 16 Nov 2024 02:52:37 GMT )
Nov 16, 2024 02:52 UTC
  • Wasudani elfu 343 wamekimbia makazi yao, 503 wameuawa huko Al-Hilalia

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limetangaza kuwa mamia kwa maelfu ya watu wamekimbia kutoka Jimbo la Aljazira katikati mwa Sudan na kuhamia maeneo mengine, tangu Oktoba 20, huku idadi ya vifo katika mji wa Hilaliya katika jimbo hilo ikiongezeka hadi watu 503 kutokana na mashambulizi ya Vikosi vya Msaada wa Haraka, (RSF).

Shirika hilo lilisema katika taarifa yake kwamba zaidi ya watu 343,000, wanaojumuisha familia zipatazo 68,000, wamehamishwa kutoka maeneo mbalimbali ya Jimbo la Aljazira na kuelekea majimbo ya Kassala na Gedaref upande wa mashariki, na Mto Nile kaskazini, kutokana na kuongezeka kwa ukosefu wa usalama na mashambulizi ya Vikosi vya Msaada wa Haraka.

Wapiganaji wa RSF wamezidisha mashambulizi yao katika Jimbo la Aljazira tangu Oktoba 20, baada ya mmoja wa viongozi wa kundi hilo aliyejulikana kwa jina la Abu Aqla Keikel, mkazi wa jimbo hilo, kujitenga na RSF na kujiunga na jeshi la taifa la Sudan.

Desemba 2023, Vikosi vya Msaada wa Haraka - vikiongozwa na Keikel- vilidhibiti miji kadhaa kwenye Jimbo la Aljazira, ikiwa ni pamoja na Wad Madani, katikati mwa jimbo hilo.

Wakimbizi Sudan

Katika muktadha huu, "Central SD Call", taasisi ya kiraia inayojumuisha wanaharakati, ilitangaza katika taarifa yake ya Alkhamisi, kwamba idadi ya wahanga katika mji wa Al-Hilalia jimboni humo imeongezeka hadi 503 waliouawa kutokana na mashambulizi na mzingiro wa siku 21 wa wapiganaji wa RSF.

Wanaharakati hao wametoa wito "kwa pande zote husika kuingilia kati mara moja ili kuondoa mzingiro usio wa haki katika mji wa Hilaliya."