Jun 11, 2017 04:48 UTC
  • Jumapili, Juni 11, 2017

Leo ni Jumapili tarehe 16 Ramadhan mwaka 14384 Hijria, sawa na tarehe 11 Juni 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 711 iliyopita, alifariki dunia Ibn Zamlakani, mtaalamu wa sharia za Kiislamu, hadithi na fasihi mkubwa wa mjini Damascus, Syria. Ibn Zamlakani alisoma elimu mbalimbali kutoka kwa maulama wakubwa wa zama zake huku akiipa umuhimu mkubwa elimu ya dini na hadithi. Miaka 20 baadaye Ibn Zamlakani alifikia daraja ya kutoa fatwa katika masuala ya dini. Alijishughulisha pia na shughuli za ukadhi na ukufunzi katika shule tofauti za mji wa Damascus. Moja ya athari za Ibn Zamlakani ni pamoja na kitabu cha 'Burhanul-Kaashif an I'jaazil-Qur'an.'

Ibn Zamlakani,

Siku kama ya leo miaka 593 iliyopita alifariki dunia Taqiyud-Din Abul-Abbas Maqrizi, msomi na mwanahistoria mkubwa wa Kiislamu. Maqrizi alizaliwa mjini Cairo, Misri na baadaye kusoma elimu ya Kiislamu katika miji tofauti ya nchi hiyo kama ambavyo pia alikuwa na uhodari katika elimu mbalimbali za Kiislamu. Kwa muda fulani alifanya kazi ya ukadhi mjini Cairo. Alipendelea sana historia huku akiandika vitabu tofauti katika uwanja huo. Miongoni mwa athari za Taqiyud-Din Abul-Abbas Maqrizi ni pamoja na kitabu cha 'as-Suluuk Lima'arifatil-Muluuk' ambacho kinazungumzia historia.

Siku kama ya leo miaka 445 iliyopita alizaliwa katika familia masikini Ben Jonson, mwandishi wa michezo ya kuigiza na muigizaji mashuhuri wa Uingereza. Alilazimika kufanya kazi za mikono katika sekta ya ujenzi akiwa na baba yake wa kambo ili kujidhaminia karo ya shule. Baada ya kuhitimu masomo ya juu alijiunga na jeshi la nchi hiyo akiwa na miaka 29 lakini bado jambo hilo halikumpa utulivu wa moyo, na hivyo akalazimika kuondoka jeshini. Aliingia kwenye uwanja wa michezo ya kuigiza kama muigizaji na kisha kuanza kuandika michezo hiyo mwenyewe. Aliishi katika zama za Shakespeare, mwandishi mashuhuri wa michazo ya kuigiza wa Uingereza na kushirikiana naye kwa karibu. Katika michezo yake, Ben Jonson alikuwa akiwakejeli mabwenyenye na viongozi wa makanisa jambo lililowakasirisha sana. Licha ya umashuhuri aliokuwa nao lakini bado umasikini na matatizo mengine yalimwandama Jonson hadi mwishoni mwa maisha yake hapo mwaka 1637.

Ben Jonson

Siku kama ya leo miaka 162 iliyopita, yaani sawa na tarehe 11 Juni 1855, mwanga wa jua ulitambuliwa kwa kutumiwa njia za taaluma ya uchanganuzi na wigo wa rangi. Jaribio hilo lilifanywa kwa mara ya kwanza katika historia ya utafiti mpya wa fizikia na wanasayansi wawili wa Ujerumani walioitwa Kirchhoff na Bunsen. Inafaa kuashiria hapa kwamba, mionzi ya jua katika hewa wakati wa mvua pamoja na kutokea upinde wa mvua wenye rangi mbalimbali, ni tukio la kuvutia ambalo husababishwa na kuchanganuliwa nuru ya jua na matone ya maji mawinguni. Hata hivyo suala hilo mwanzoni lilifafanuliwa na wanasayansi wa Kiislamu kama vile Ibn Sina, Ibn Hisham na Qutbudin Shirazi na baadaye kuthibitishwa na Kirchhoff na Bunsen.

Na siku kama ya leo miaka 43 iliyopita sawa na tarehe 21 Khordad mwaka 1353 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, alifariki dunia Daktari Muhammad Khaz'ali, mwasisi wa Tasisi ya Kuongoza na Kuwasaidia vipofu ya Iran. Dakta Khaz'ali alipokuwa mtoto alipoteza macho yake kutokana na ugonjwa wa ndui, na kupata elimu katika shule maalumu ya vipofu. Kwa kutumia uwezo wake mkubwa wa kuhifadhi mambo, alipata mafanikio makubwa katika masomo yake na kufanikiwa kuhitimu shahada ya uzamili ya sheria katika chuo kikuu cha Tehran. Dakta Khaz'ali alifahamu vyema lugha ya Kiarabu, Kifaransa na Kiingereza na aliandika na kutafsiri vitabu mbalimbali. Miongoni mwa masuala aliyojishughulisha nayo Dakta Khaz'ali ni kupigania kupatiwa huduma muhimu vipofu katika uga wa kimataifa na alikuwa pia mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Mashariki ya Kati katika Baraza la Kitaifa la Kuwahudumia vipofu.

Dakta Khaz'ali