Jumamosi, Julai Mosi, 2017
Leo Jumamosi tarehe 6 Mfunguo Mosi Shawwal 1438 Hijria sawa na tarehe Mosi Julai mwaka 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 652 iliyopita, alifariki dunia Ibn Bardes, malenga na mpokezi wa hadithi wa Kiislamu. Ibn Bardes alizaliwa huko Baalbek moja kati ya miji ya Lebanon na kuelekea katika mji wa Damascus Syria baada ya kukamilisha masomo yake ya awali, ambapo alinufaika na elimu ya maulamaa maarufu wa zama hizo. Msomi huyo wa Kiislamu alisafiri katika nchi mbalimbali za Kiislamu na akaanza kufundisha baada ya kukamilisha masomo yake. Alikuwa mashuhuri baina ya watu kwa kushikamana na dini, kutakasa nafsi na maadili mema. Miongoni mwa vitabu vya Ibn Bardes ni al Iilamu fii Wafayatil Aalam. ***

Miaka 57 iliyopita katika siku kama ya leo, sehemu mbili za Somalia ya Uingereza na ya Italia ziliungana na kuunda nchi moja ya Somalia yenye kujitawala. Karne kadhaa nyuma, Somalia iliwahi kujitawala kwa kipindi kifupi. Mwaka 1884 Uingereza iliiweka katika himaya yake sehemu ya ardhi ya nchi hiyo. Miaka mitano baadaye Italia nayo ikakoloni baadhi ya sehemu za Somalia. Harakati za mapambano za Muhammad Abdullah Hassan dhidi ya Waingereza kuanzia mwaka 1901 hadi 1920 hazikusaidia kitu. Mwaka 1950 Umoja wa Mataifa uliitaka Italia iandae mazingira ya kujitawala na kuwa huru Somalia. ***
Katika siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, nchi ndogo ya Burundi ilijitangazia uhuru wake. Ardhi ya Burundi pamoja na Rwanda ilikuwa sehemu ya makoloni ya Mjerumani huko Afrika Mashariki kuanzia mwaka 1899 hadi 1917. Baada ya Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na kushindwa Ujerumani katika vita hivyo, Umoja wa Mataifa uliikabidhi Ubelgiji ardhi ya Burundi na mwaka 1946, yakatambuliwa rasmi mamlaka na utawala wa Ubelgiji kwa nchi hiyo. Mwaka 1962 Burundi ilipata uhuru ikiwa na mfumo wa utawala wa Kifalme. Hata hivyo miaka minne baadaye wapigania jamhuri walimuondoa madarakani mfalme na kuanzisha mfumo wa serikali ya jamhuri. ***
Na siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, Rwanda ilipata uhuru. Rwanda ina historia inayofanana na jirani yake wa kusini yaani Burundi ambapo kabla ya nchi hizo kujitangazia uhuru zilikuwa zikikoloniwa na Ubelgiji. Baada ya mapambano mtawalia ya wapigania uhuru wa Rwanda, hatimaye mnamo mwaka 1962, nchi hiyo ilipata uhuru na kabila kubwa la Wahutu likashika hatamu za uongozi wa nchi. Mwaka 1973, Meja-Jenerali Juvenal Habyarimana alichukua madarakani baada ya kufanya mapinduzi yasiyo na umwagaji damu. Hata hivyo mwaka 1994 kulitokea mauaji ya kimbari ambapo zaidi ya watu laki 8 waliuawa wengi wao wakiwa ni wa kabila la Kitutsi.***