Jul 02, 2017 04:14 UTC
  • Takwimu Jumapili

Leo ni Jumapili tarehe saba Shawwal 1438 Hijria, sawa na tarehe Pili Julai 2017.

Siku kama ya leo miaka 1435 iliyopita kulipiganwa vita vya Uhud kando kando ya mlima wenye jina hilo kaskazini mwa mji wa Madina, kati ya Waislamu na Washirikina. Baada ya washirikina wa Kiquraishi kushindwa vibaya na Waislamu katika vita vya Badr walianzisha vita hivyo vya Uhud kwa kuandaa jeshi la watu 3,000 waliokuwa wamejizatiti kikamilifu kwa ajili ya vita hivyo, huku wapiganaji wa Kiislamu wakiwa 700 tu. Kabla ya kuanza kwa vita hivyo, Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w) aliwashauri masahaba zake namna walivyotakiwa kupambana na Maquraishi na iliamuliwa kuwa vita hivyo vipiganwe nje ya mji wa Madina. mwanzoni mwa vita hivyo, Waislamu walionekana kushinda, hata hivyo kufuatia kughafilika na baadhi yao kuasi amri ya Mtume (saw) aliyewataka kuendelea kubakia mlimani, Waislanu walishuka mlimani kwa tamaa ya kuchukua ngawira hali iliyowafanya washirikina kuwashambulia na kudhoofisha nguvu na uwezo wao. Waislamu 70 waliuawa shahidi katika vita hivyo akiwemo Hamza ami yake Mtume (s.a.w). Hata hivyo washirikina hawakuweza kupata ushindi wa moja kwa moja na hivyo wakalazimika kurejea Makka.

Eneo kulipopiganwa vita vya Uhud

Siku kama ya leo miaka 1132 iliyopita, alifariki dunia Ahmad Bin Jihani, msomi mkubwa wa Kiirani wa zama za Samani. Abu Abdillah Ahmad Bin Jihani, alikuwa mwanasiasa na mtaalamu mashuhuri wa elimu ya jeografia katika ulimwengu wa Kiislamu kutokana na utafiti mwingi alioufanya katika uwanja huo. Athari kubwa ya Ibn Jihani ni pamoja na kitabu cha elimu ya jeografia alichokipa jina la al-Masaalik wal-Mamaalik. Katika kitabu hicho Allamah Ahmad Bin Jihani alibainisha nadharia zake juu ya umbo duara la dunia ikiwa ni katika kufafanua mtazamo wa dini ya Uislamu iliyolitambua suala hilo kabla ya Wamagharibi.

Ahmad Bin Jihani

Siku kama ya leo miaka 451 iliyopita, alifariki dunia Michel de Nostredame maarufu kwa jina la Nostradamus, mtabiri wa nchini Ufaransa. Nostradamus alizaliwa mwaka 1503 Miladia na tangu mwanzoni mwa ujana wake alijifundisha hesabati na elimu ya nyota huku akiamini kwamba angeweza kutabiri matukio ya baadaye kwa kutegemea mwendo wa nyota. Awali Nostradamus alijifundisha elimu ya tiba, lakini taratibu akajiingiza katika elimu ya nyota. Kalenda ya kwanza ya nyota ya Nostradamus alitangazwa mwaka 1550 ambapo miaka mitano baadaye alianza kusoma mashairi katika kutabiri matukio ya baadaye. Kiujumla ni kwamba Nostradamus alidai katika kitabu chake cha 'Tabiri' juu ya kutokea matukio muhimu duniani. Aidha miongoni mwa tabiri zake ni pamoja na kutokea kwa mapinduzi ya nchini Ufaransa, kudhihiri Napoleon Bonaparte, Adolf Hitler  na kadhalika mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Michel de Nostredame

Siku kama ya leo miaka 358 iliyopita alifariki dunia msomi mkubwa wa Kishia kwa jina la Mirza Rafia Naeini. Mirza Rafiud-Din Muhammad bin Haidar Twabatwabai, maarufu kwa jina la  Mirza Rafia Naein alikuwa mmoja wa maulama wakubwa wa Kishia katika karne ya 11 Hijiria. Alitabahari katika elimu ya sharia za Kiislamu, usul fiqhi, theolojia na elimu ya hadithi. Kadhalika Mirza Rafia Naeini alikuwa kati ya walimu wa Allamah Majlisi wa pili na Sheikh Hurr Aamil na mmoja wa walimu wa Sheikh Bahai. Vitabu vya 'Aqsamu Tashkik wa Haqiqtuh' 'Hashiyat Usulul-Kaafi' na 'al-Shajaratul-Ilaahiyyah' ni miongoni mwa athari za msomi huyo. Allamah Mirza Rafia Naeini alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 85 huko mjini Isfahan, Iran.

Kaburi la Mirza Rafia Naeini

Siku kama ya leo miaka 128 iliyopita mfumo wa kisultani ulifutwa huko Brazil na badala yake ukaasisiwa mfumo wa jamhuri bila ya umwagaji damu wowote na katika hali ya utulivu kabisa. Mfalme wa mwisho wa Brazil alikuwa Pedro wa Pili ambaye alifanya jitihada za kufanya mabadiliko nchini humo. Hatua za mfalme huyo hususan ile ya kuondoa biashara ya utumwa mwaka 1888, iliwakasirisha sana wamiliki wa ardhi waliokuwa wakiunga mkono mfumo wake wa kisultani. Pedro wa Pili alienguliwa madarakani bila ya mapambano yoyote na mfumo wa jamhuri ukaasisiwa nchini Brazil.

Pedro wa Pili

Siku kama ya leo miaka 92 iliyopita, alizaliwa Patrice Lumumba mwasisi wa Kongo huru. Lumumba alitoa mchango mkubwa katika juhudi za kukombolewa Kongo wakati wa harakati za ukombozi wa nchi za Kiafrika. Lumumba aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi baada ya kuundwa Jamhuri ya Kongo mwaka 1960. Patrice Lumumba aliuawa mwaka 1961 na vibaraka wa Marekani na Ubelgiji baada ya kuvumilia mateso na unyama mkubwa. Lumumba aliandika vitabu kadhaa wakati wa uhai wake na mashuhuri zaidi ni kile alichokiita "Kongo, Nchi Yangu."

Patrice Lumumba mwasisi wa Kongo huru

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita aliaga dunia mwandishi mtajika wa Kimarekani kwa jina la Ernest Hemingway. Alizaliwa mwaka 1899 na kwa muda fulani alikuwa mwandishi huko Uingereza na Ufaransa. Hemingway alikuwa mwasisi wa riwaya na tungo fupi fupi za hadithi na alitumia lugha nyepesi na inayoeleweka. Mwaka 1954 mwandishi huyo alitunukukiwa tuzo ya Nobel katika medani ya fasihi. Moja kati ya vitabu maarufu vya Hemingway ni vile alivyoviita kwa majina ya "The Old Man and The Sea", "A Farewell to Arms" na For Whom The Bell Tolls".

Ernest Hemingway