Sep 20, 2017 03:51 UTC
  • Jumatano tarehe 20 Septemba, 2017

Leo ni Jumatano tarehe 29 Dhilhija 1438 Hijria sawa na 20 Septemba, 2017.

Siku kama ya leo miaka 186 iliyopita, lilitengenezwa basi la kwanza lililokuwa likitumia nishati ya mvuke. Basi hilo lilikuwa na uwezo wa kubeba abiria 30, huku likienda kwa mwendo mdogo na liligunduliwa na raia wa Uingereza kwa jina la Gordon Branz. Hii leo mabasi bora na ya kisasa yamegeuka kuwa moja ya vyombo muhimu vya usafiri.

Basi la kale zaidi lililokuwa likitumia nishati ya mvuke

Siku kama ya leo miaka 150 iliyopita, nchi ya Hungary iliungana na ardhi ya Austria na Francois Joseph akawa mtawala wa kifalme wa nchini mbili hizo. Hungary ambayo kwa mara kadhaa katika historia ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na nchi zenye nguvu za Ulaya kama vile Austria na utawala wa Othmania, baadaye ilijipatia uhuru wake mnamo mwaka 1918 mwishoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia.

Francois Joseph

Miaka 100 iliyopita katika siku kama hii ya leo aliuawa shahidi Sheikh Muhammad Khiyabani, mwanamapambano na mpigania uhurju na kujitawala wa Iran. Alizaliwa mwaka 1297 Hijria Shamsia katika eneo la Khamene katika mkoa wa Azarbaijan mashariki. Sheikh Khiyabani alianzisha harakati za kupinga dhulma na ukandamizaji zilizokuwa zikifanywa na tawala za silsila ya Qajar hapa nchini. Baada ya kuusambaratisha udikteta wa Muhammad Ali Shah Qajar na kumlazimisha mtawala huyo kukimbia mwaka 1287 Hijria Shamsia, wananchi wa Tabriz walimchagua Sheikh Muhammad Khiyabani kuwa mwakilishi wao katika Bunge la Taifa. Hata hivyo katika siku kama ya leo Sheikh Khiyabani alikamatwa na kuuawa shahidi, wakati alipokuwa akipambana na askari wa serikali ya kifalme.

Sheikh Muhammad Khiyabani

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, Jean-Bedel Bokasa, dikteta wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, aliondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi. Bokasa alizaliwa mnamo mwaka 1922 na kusomea nchini Ufaransa, huku akiwa shabiki mkubwa wa Napoleon Bonaparte na Charles de Gaulle, viongozi wawili wa zamani wa Ufaransa. Alichukua madaraka ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, mwaka 1966 baada ya kufanya mapinduzi dhidi ya binamu yake David Dacko, wakati Bokasa alipokuwa mkuu wa majeshi ya nchi hiyo. Jean-Bedel Bokasa alitawala nchi hiyo kwa mfumo wa kiimla na kwa kipindi cha miaka 13 sanjari na kusimamia moja kwa moja wizara 14 kati ya wizara 16 za taifa hilo la katikati mwa Afrika.

Jean-Bedel Bokasa

Na siku kama ya leo, miaka 6 iliyopita, aliuawa Burhanud-Din Rabbani, Mkuu wa Baraza Kuu la Usalama nchini Afghanistan. Burhanud-Din Rabbani alizaliwa tarehe 20 Septemba mwaka 1940 Miladia. Alikuwa kiongozi wa chama cha Jumuiya ya Kiislamu nchini humo na rais rasmi wa kwanza wa utawala wa mujahidina huko Afghanistan. Hadi mwisho wa maisha yake Burhanud-Din Rabbani, alikuwa mkuu wa Baraza Kuu hilo la Usalama lililoundwa na rais wa zamani wa nchi hiyo Hamid Karzay. Baraza hilo lilikuwa na wadhifa wa kufanya mazungumzo na makundi ya Taleban kwa lengo la kufikiwa amani na kumaliza mgogoro wa taifa hilo kwa njia ya amani. Rabani aliuawa katika siku kama ya leo, na gaidi aliyekuwa ameficha bomu katika kilemba chake, wakati alipoingia ofisini kwa shakhsia huyo kwa madai ya kufanya mazungumzo.

Burhanud-Din Rabbani