Oct 21, 2017 02:25 UTC
  • Jumamosi, Oktoba 21, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe Mosi Mfunguo Tano Safar 1438 Hijria mwafaka na tarehe 21 Oktoba 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1402 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, awamu ya mwisho ya vita kati ya jeshi la Imam Ali bin Abi Twalib (as) na Muawiya bin Abi Sufiyan ilianza katika eneo la Siffin kandokando ya Mto Furati (Euphrates) nchini Iraq. Baada ya Imam Ali bin Abi Twalib (as) kushika hatamu za uongozi Muawiya alikataa kumpa mkono wa utiifu na akaamua kuanzisha vita dhidi ya kiongozi huyo wa Waislamu. Katika kipindi cha utawala wa Khalifa Othman bin Affan, Muawiya alikuwa liwali wa Sham na baada ya kifo cha Othman alikusudia kuwa na udhibiti katika maeneo yote ya ulimwengu wa Kiislamu na kisha airithishe familia yake utawala huo. Vita vya Muawiya dhidi ya Imam Ali as pia vilitokana na jambo hilo.

Nafasi ya kijiografia ya eneo la Siffin

Tarehe Mosi Mfunguo Tano Safar mwaka 61 Hijria yaani miaka 1378 iliyopita, msafara wa familia ya Mtume Muhammad (SAW) ambayo ilichukuliwa mateka katika vita vya Karbala, uliwasili katika mji wa Sham ambao ulikuwa makao makuu ya utawala wa Yazid bin Muawiya. Wakiwa Sham, Ahlul-Baiti wa Mtume (SAW) hususan Bibi Zainab (as) na Imam Sajjad (as) walitoa hutuba tofauti katika msikiti wa Sham wakifichua maovu ya Yazid, kiongozi dhalimu wa Bani Umayyah. Vile vile Ahlul-Bait wa Mtume (SAW) walifikisha kwa watu ujumbe wa harakati ya mashahidi wa Karbala kwa njia nzuri kiasi kwamba watu wa Sham walielewa ukweli kuhusu jinai za jeshi la Yazid na kuzua hasira dhidi ya mtawala huyo. Hali hiyo ilimfanya Yazid aliyetoa amri ya kuuawa Imam Hussein (as) na wafuasi wake, akane uhakika huo na kumtwisha lawama hizo Ubaidullah bin Ziyad, aliyekuwa gavana wa mji wa Kufa, Iraq.

Msafara wa mateka wa Karbala

Katika siku kkama ya leo miaka 227 iliyopita, alizaliwa malenga wa Kifaransa Alphonse de Lamartine.  De Lamartine alitambulika kuwa msanii na mwanafikra mkubwa nchini Ufaransa. Aliwahi pia kusafiri Mashariki na kuishi katika mji mkuu wa Beirut, Lebanon. Aidha miongoni mwa athari za malenga huyu, ni pamoja na "Safari ya Mashariki" na "Kimya cha Malaika".  Alphonse de Lamartine alifariki dunia mwaka 1869. ***

Alphonse de Lamartine

Siku kama ya leo miaka 184 iliyopita, alizaliwa Alfred Nobel mkemia wa Sweden na mvumbuzi wa dynamite. Nobel alikuwa na shauku kubwa ya kujifunza sayansi ya kemia na baadaye akafanya utafiti mkubwa katika uwanja huo na kufanikiwa kuvumbua mada za mlipuko yaani (dynamite). Kinyume na alivyotarajia, majeshi ya nchi mbalimbali yalianza kutumia dynamite vitani na hivyo kusababisha mauaji ya raia wengi. Mkemia Nobel ambaye alikuwa na utajiri mkubwa na hakufikiri kuwa dynamite ingeweza kutumiwa vibaya, aliamua kutoa utajiri wake kama tuzo na zawadi. Alfred Nobel alifanya hivyo kwa lengo kwamba, tuzo hiyo itolewe kila mwaka kwa shakhsiya aliyefanya kazi kubwa ya thamani duniani katika masuala ya sayansi, fasihi na amani. Hata hivyo kinyume na matakwa yake, leo hii tuzo ya amani ya Nobel imechukua sura ya kisiasa na inatumiwa kama wenzo wa kutangaza na kueneza siasa za nchi za Magharibi duniani. ***

Alfred Nobel

Miaka 57 iliyopita katika siku kama ya leo,  nchi ya Kiafrika ya Somalia ilipata uhuru na siku hii inajulikana nchini humo kama Siku ya Taifa. Kijiografia Somalia ipo kaskazini mashariki mwa bara la Afrika katika eneo linalojulikana kama Pembe ya Afrika. Mji mkuu wa Somalia ni Mogadishu na lugha rasmi ya nchi hiyo ni Kisomali na Kiarabu. Asilimia 99 ya wananchi wa Somalia ni Waislamu. Nchi hiyo kwa miaka kadhaa ilikuwa chini ya ukoloni wa Italia na Uingereza mpaka ilipojipatia uhuru mwaka 1960 na katika siku kama ya leo. ***

Somalia ilipo kijiografia

Miaka 39 iliyopita katika siku kama ya leo, vibarua na wafanyakazi wa sekta ya mafuta nchini Iran walianza kufanya mgomo nchi nzima wakati wa kujiri harakati za mapambano ya wananchi dhidi ya utawala dhalimu wa Shah. Kufuatia mgomo huo, usafirishaji mafuta nje ulisimamishwa, jambo ambalo liliukatia utawala wa Shah moja ya vyanzo muhimu vya kipato. Aidha kusimamishwa usafirishaji mafuta ya Iran nje ya nchi, kulipelekea kupanda mno kwa bei ya bidhaa hiyo ulimwenguni. Utawala wa Shah ulitumia vitisho mbalimbali ili kuwafanya wafanyakazi hao warejee kazini, lakini mgomo huo uliendelea hadi utawala huo kibaraka ulipoangushwa. Wananchi wanampinduzi wa Iran licha ya kukabiliwa na matatizo mengi yaliyosababishwa na uhaba wa nishati ya mafuta, lakini walisimama kidete na kuuunga mkono mgomo wa wafanyakazi hao wa sekta wa mafuta.***

Mgomo wa wafanyakazi wa sekta ya mafuta

Na katika siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, kama ya leo miaka 30 iliyopita Brigedia Jenerali Mundhir Abu Ghazala, kamanda Jeshi la Majini la Palestina aliuawa na maajenti wa shirika la ujasusi la utawala ghasibu wa Kizayuni Mossad. Wazayuni walimuuwa kigaidi kamanda huyo wa jeshi la majini la Palestina kwa kutega bomu ndani ya gari lake huko Athens mji mkuu wa Ugiriki. Brigedia Jenerali Abu Ghazala ni miongoni mwa wahanga wa ugaidi wa kiserikali wa utawala wa kibaguzi wa Kizayuni unaoungwa mkono kwa hali na mali na Marekani.***

Brigedia Jenerali Mundhir Abu Ghazala