Jumapili, Oktoba 22, 2017
Leo ni Jumapili tarehe pili Swafar Mfungo tano 1439 Hijria, mwafaka na tarehe 22 Oktoba 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1318 iliyopita, aliuawa shahidi Zaid bin Ali bin Hussein mwana wa Imam Sajjad (as) na mjukuu wa Mtume Muhammad (saw). Zaid bin Ali alisimama kupambana na dhulma za Banii Umayyah na kulinda matunda ya mapambano ya babu yake, Imam Hussein bin Ali (as). Baada ya mapambano ya kishujaa, Zaid bin Ali aliuawa shahidi katika mji wa Kufa nchini Iraq. Harakati ya mapambano ya Zaid ni miongoni mwa matunda ya mapambano ya Imam Hussein (as) katika medani ya Karbala hapo mwaka 61 Hijria kwani baada ya mapambano ya siku ya Ashuraa kulijitokeza harakati nyingi baina ya Waislamu zilizopigana jihadi kwa lengo la kuuondoa madarakani utawala dhalimu wa Banii Umayyah.

Siku kama yale leo miaka 1169 iliyopita, sawa na tarehe pili Swafar mwaka 270 Hijiria, harakati za mapambano za Wazangian (Mazangi) zilifeli baada ya kuuawa kiongozi wa harakati hiyo kwa jina la 'Swahib al-Zanj'. Ali Bin Muhammad maarufu kwa jina la Swahib al-Zanj ambaye pia alikuwa ni mmoja wa wajukuu wa bwana Mtume Muhammad (saw) na Imam Ali (as) alianzisha harakati za mapambano mwaka 255 Hijiria akisaidiwa na wafuasi wake pamoja na watumwa weusi ambao walikuwa wakiitwa Wazangi, dhidi ya utawala wa kidhalimu wa Bani Abbas huko kusini mwa Iraq. Swahib al-Zanj aliwaahidi watumwa hao weusi kuwaachilia huru kutoka katika minyororo ya utumwa na kuwapatia haki sawa katika jamii kama watu wengine suala ambalo liliwafanya watu wa jamii ya watu hao kuvutiwa na harakati ya shakhsia huyo. Mwaka 257 Swahib al-Zanj aliweza kudhibiti mji muhimu wa Basra, Iraq na taratibu akaanza kutwaa maeneo mengine ya karibu na mji huo. Katika kipindi hicho majeshi ya utawala wa Abasi yalifanya hujuma kadhaa dhidi ya Mazangi lakini hata hivyo hujuma hizo zilikuwa zikifeli kutokana na msimamo imara wa jamii ya watu hao weusi. Hata hivyo kutokana na matatizo ya ndani, hatimaye jamii ya watu hao ilidhoofika sana ambapo kuuawa kiongozi wao ' Swahib al-Zanj ' kukapelekea harakati yao yote kusambaratika baada ya miaka 15.

Siku kama ya leo miaka 694 iliyopita, alifariki dunia nchini Misri, Abu Hayyan Gharnatwi, malenga na fasihi mkubwa wa Waislamu. Alizaliwa mwaka 654 Hijiria huko Andalusia 'Uhispania ya leo' ambapo baadaye alifanya safari katika miji mbalimbali kwa ajili ya kutafuta elimu na kutoka kwa walimu tofauti wa zama zake. Mwaka 679 Abu Hayyan Gharnatwi, alielekea nchini Misri ambapo aliishi hadi mwisho wa maisha yake. Akiwa nchini humo alijishughulisha na ufundishaji na kuandika vitabu. Licha ya kwamba Gharnatwi alikuwa mtaalamu katika elimu ya Qur'an, hadithi na sharia za Kiislamu, nchini Misri alipata umashuhuri mkubwa katika utaalamu wa elimu ya nahaw. Abu Hayyan Gharnatwi ambaye mwishoni mwa uhai wake alikuwa kipofu, ameacha turathi nyingi kama vile kitabu cha 'Al-Idraaku Lilisaanil-Atraak' 'Tadhkiratun-Nuhaat' 'Tafsirul-Bahril-Muhitw' na 'Kitabu cha maisha yake.'

Siku kama ya leo miaka 677 iliyopita, alifariki dunia, Ibn Doraihe, mwanahisabati na mtaalamu mkubwa wa nyonta katika ulimwengu wa Kiislamu. Alifanya juhudi kubwa katika kutafuta elimu za Qur'an Tukufu, sharia za Kiislamu 'fiqhi' na hesabu. Baadaye Ibn Doraihem alielekea nchini Misri kwa ajili ya kusoma elimu ya hadithi ambapo alifanikiwa kufikia vilele vya elimu huku kwa muda Fulani akielekea pia Sham 'Syria ya leo'. Akiwa Sham alijishughulisha na kazi ya uhadhiri katika msikiti mkuu wa Umayyad 'Jamiul-Umawi.' Alikuwa mahiri katika elimu za visomo vya Qur'an, hadithi, fiqhi, usulu fiqhi, theolojia, tafsiri ya Qur'an, fasihi na lugha ya Kiarabu. Katika lugha ya Kiarabu Ibn Doraihem, alikuwa na nadharia tofauti ambao zimefafanuliwa na baadhi ya wasomi wakubwa wa lugha hiyo. Moja ya athari zake nyingi ni pamoja na kitabu kinachoitwa 'Qaswidatu fii Mad'hi al-Rasuul saw.'

Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita yaani tarehe 30 Mehr mwaka 1331 Hijria Shamsiya Dakta Hussein Fatemi Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran katika serikali ya wakati huo ya Musaddiq, alitangaza kukatwa uhusiano wa kisiasa wa Iran na Uingereza. Uamuzi huo uliopasishwa na Baraza la Mawaziri ulikabidhiwa kwa balozi mdogo wa Uingereza hapa mjini Tehran. Sababu ya kukatwa uhusiano huo wa kisiasa na Uingereza, ilikuwa ni hatua ya serikali ya London ya kupuuza matakwa ya wananchi wa Iran.

Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, Mawaziri Wakuu wa Ufaransa, Uingereza na utawala haramu wa Israel walikutana katika kikao cha siri nchini Ufaransa kujadili mpango wa kuishambulia kijeshi Misri. Uingereza na Ufaransa zilizokuwa na mpango wa kuikalia kwa mabavu Kanali ya Suez, zilipoteza maslahi yao baada ya Gamal Abdul Nasser Rais wa wakati huo wa Misri kuitaifisha na kuitangaza kanali hiyo kuwa ya kitaifa. Israel ambayo ilikuwa ikiihesabu Misri kuwa adui yake mkubwa ilikusudia kuitumia fursa hiyo kuitia hasara serikali Misri. Wiki moja baada baadaye majeshi ya tawala hizo yakaanza kuishambulia Misri.

Siku kama ya leo miaka 523 iliyopita Christopher Columbus baharia wa Kiitalia alianza safari yake ya pili ya kiuvumbuzi. Columbus aligundua visiwa vya Antil katika bahari ya Atlantic huko mashariki mwa Amerika ya Kati. Christopher Columbus aligundua Marekani katika safari yake ya kwanza ya kiuvumbuzi aliyoianza mwezi Agosti hadi Oktoba mwaka 1492.

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, aliaga dunia Toynbee, mwanahistoria wa Uingereza. Toynbee alizaliwa mwaka 1889. Alikuwa muhadhiri katika chuo kikuu cha mjini London, Uingereza katika kitengo cha historia ya kimataifa. Aliandika vitabu mbalimbali katika fani ya historia, muhimu Zaidi kikiwa ni kitabu cha 'Uchunguzi katika Historia.' Katika kitabu hicho Toynbee alijikita katika kuchunguza masuala mbalimbali ya Ustaarabu wa kipindi cha karne za kati.

Na siku kama ya leo miaka 99 iliyopita, yaani tarehe 22 Oktoba mwaka 1918, duru ya mwisho ya mlolongo wa Vita vya Kwanza vya Dunia ilianza kaskazini magharibi mwa Ulaya kwa waitifaki kuyashambulia majeshi ya Ujerumani. Awali majeshi ya Ujerumani yalionyesha upinzani mkubwa, ingawa hata hivyo baada ya muda yalishindwa vibaya na kwa utaratibu huo, Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia vikafikia tamati.