Dec 17, 2017 01:30 UTC
  • Jumapili, Disemba 17, 2017

Leo ni Jumapili tarehe 28 Rabiul Awwal 1439 Hijria sawa na 17 Disemba 2017.

Siku kama ya leo miaka 239 iliyopita, alizaliwa Humphrey Davy mwanakemia na mwanafikizia wa Kiingereza. Katika majaribio yake ya kimaabara, msomi huyo aliweza kutenganisha elementi za Sodium, Potassium, Calcium, Barium, Magnesium na Strontium miongoni mwa elementi nyinginezo na hatua hiyo ilihesabiwa katika zama hizo kuwa mafanikio makubwa katika sayansi ya kemia. Davy mbali na kuwa mwasisi wa elimu inayojulikana kama "electrochemical", aliweza pia kuwasilisha nadharia ambayo iliitaja gesi ya Hydrojen kuwa gesi inayoweza kuzitambua asidi. Mwanakemia huyo wa Kiingereza alifariki dunia mwaka 1829 Miladia.

Humphrey Davy

Siku kama ya leo miaka 114 iliyopita inayosadifiana na tarehe 17 Disemba mwaka 1903, ndege ya kwanza duniani iliyokuwa ikitumia injini ya mota, ilifanikiwa kuruka na kupaa angani kwa dakika moja baada ya kufanyiwa majaribio kadhaa. Ndege hiyo ilitengenezwa na ndugu wawili walioitwa Wilbur na Orville Wrights na kufanyiwa majaribio katika jimbo la North Carolina nchini Marekani. Ndugu hao wawili walikuwa watengeneza baiskeli ambao baadaye walipatwa na shauku kubwa ya kutengeneza ndege yenye kutumia injini ya mota.

Wilbur na Orville Wrights

Miaka 46 iliyopita sawa na tarehe 17 Disemba mwaka 1971 vilimalizika vita vya tatu kati ya Pakistan na India kwa kujitenga eneo la Pakistan Mashariki, ambalo lilitangazwa kuwa nchi ya Bangladesh. Wananchi wa Baghladesh ya leo kwa asilimia 95 ni Wabangali walio na asili ya Pakistan Mashariki, ambao tangu mwanzoni mwa kuundwa Pakistan walikuwa wakipinga kuhodhiwa uongozi wa nchi hiyo na Pakistan Magharibi, na ubaguzi waliokuwa wakikabiliana nao na ndio maana wakaanza harakati za kutaka kujitawala Pakistan Mashariki chini ya uongozi wa Sheikh Mujib al-Rahman.

Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, sawa na tarehe 17 Disemba mwaka 1992 utawala wa Kizayuni wa Israel, kwa kisingizio cha kuuawa polisi wake mmoja wa mpakani, uliwabaidisha kusini mwa Lebanon viongozi 415 wa harakati ya Jihadul Islam na Hamas kutoka Palestina. Baada ya serikali ya Lebanon kupinga hatua hiyo isiyo ya kibinadamu na kukataa kuwapokea Wapalestina hao, hasira na upinzani wa ulimwengu wa Kiislamu ulilifanya Baraza la Usalama kupitisha azimio nambari 977 lililolaani hatua hiyo ya Tel Aviv na kutaka kurejeshwa Wapalestina hao waliobaidishwa nchini kwao.

Wapalestina waliofukuzwa katika makazi yao

Tarehe 17 Disemba miaka 7 iliyopita kijana mmoja wa Kitunisia kwa jina la Tariq Mohamed Bouazizi alijiteketeza kwa moto na kuanzisha harakati ya ukombozi wa wananchi wa nchi hiyo dhidi ya utawala wa kidikteta wa Habib Bourguiba na Zainul Abidin bin Ali uliodumu kwa kipindi cha nusu karne. Kujichoma moto kwa Bouazizi ilikuwa cheche ya harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Tunisia na katika nchi nyingine za Kiarabu kama Misri, Libya, Yemen na Bahrain dhidi ya watawala dhalimu na vibaraka wa Magharibi.

Bouazizi ambaye alikuwa na shahada ya chuo kikuu alikuwa akiuza bidhaa za mkononi mitaani aliponyanganywa bidhaa zake na kudhalilishwa na afisa wa kike wa halmashauri ya mji na ndipo alipoamua kujiteketeza kwa moto, kitendo ambacho kiliamsha hasira za wananchi wa Tunisia na kuwa chachu ya harakati iliyohitimisha utawala wa dikteta Zainul Abidin. Dikteta huyo alikimbia nchi na kwa sasa anapewa hifadhi na watawala wa kifalme wa Saudi Arabia.

Tariq Mohamed Bouazizi