Dec 25, 2017 06:36 UTC

Sura ya As-Sabaa, aya ya 18-21 (Darsa ya 765)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 765 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 34 ya Sabaa. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 18 na 19 ambazo zinasema:

 وَجَعَلْنَا بَيْنَهُمْ وَبَيْنَ الْقُرَى الَّتِي بَارَكْنَا فِيهَا قُرًى ظَاهِرَةً وَقَدَّرْنَا فِيهَا السَّيْرَ ۖ سِيرُوا فِيهَا لَيَالِيَ وَأَيَّامًا آمِنِينَ

Na baina yao na miji mingine tuliyo ibariki tuliweka miji iliyo dhaahiri, na tukaweka humo vituo vya safari. Tukawaambia: Nendeni humo usiku na mchana kwa amani.

فَقَالُوا رَبَّنَا بَاعِدْ بَيْنَ أَسْفَارِنَا وَظَلَمُوا أَنفُسَهُمْ فَجَعَلْنَاهُمْ أَحَادِيثَ وَمَزَّقْنَاهُمْ كُلَّ مُمَزَّقٍ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّكُلِّ صَبَّارٍ شَكُورٍ

(Lakini) wakasema: Mola wetu Mlezi! Weka mwendo mrefu baina ya safari zetu. Na wakazidhulumu nafsi zao. Basi tukawafanya ni masimulizi tu, na tukawatawanya tawanya. Hakika katika hayo bila ya shaka zimo Ishara kwa kila mwenye subira sana na mwenye kushukuru.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizoelezea kwa ujumla habari za kaumu ya Sabaa iliyokuwa ikiishi katika ardhi ya Yemen. Aya tulizosoma zinasema: Mwenyezi Mungu alikuwa amewamiminia neema nyingi mno watu wa kaumu hiyo kiasi kwamba katika eneo hilo kubwa vilijengeka vijiji vilivyostawi na kunawiri katika masafa ya karibu mno kutoka kijiji kimoja hadi kingine. Ardhi yake ilikuwa imenawiri kwa kijani kibichi na kufunikwa na anuai za miti na mimea ya maua na mashamba ya mazao kiasi cha kufupisha masafa na kuvifanya vijiji hivyo vikaribiane. Mbali na neema chungu nzima, amani pia ilitawala katika eneo hilo; na kwa ujumla anga ya uneemevu ilitanda katika maisha ya watu. Kila mmoja alishughulika na kazi yake na kufaidika na neema chungu nzima zilizokuwepo. Lakini hali hiyo haikuendelea, kwani mghafala na kuleweshwa na neema kuliwafanya akthari ya watu wamsahau Mwenyezi Mungu. Walikuwa wakijivuna na kujifaharisha na kutekwa na starehe na anasa mpaka ikafika hadi raha na neema zenyewe walizojaaliwa nazo pia zikawachosha na kuwakinaisha wakawa wanatamka kwa ndimi zao: Tunataka hali hii tuliyonayo ibadilike tusiwe tumekaribiana sana na kuwa pamoja kiasi hiki. Bora tuwe mbalimbali zaidi na kila mmoja awe mbali kidogo na mwenzake. Kuzikufuru huko neema walizojaaliwa na kutaka wabadilishiwe ziwe nakama kulipelekea kubomoka bwawa kubwa la eneo hilo lililokuwa mhimili wa ustawi na maendeleo yao. Kilichotokea hasa ni kwamba kwa sababu kadhaa, kuta za bwawa hilo la udongo zilianza kulegalega kwa ndani, na baada ya kutokea mafuriko makubwa, kuta hizo za bwawa zilivunjika na mafuriko mengine makubwa yakatokea. Tukio hilo liliibadilisha mara moja ardhi ya Sabaa ya eneo lililonawiri la kijani kibichi kuwa sehemu iliyozagaa matope na nyumba zilizobomoka na kuporomoka. Ilikuwa hatima yenye kutoa ibra na mazingatio kiasi kwamba kwa muda wa miaka kadhaa, yaliyoisibu ardhi ya Sabaa yalibaki kuwa maudhui ya kuzungumziwa na watu, kwamba vipi eneo lile la kijani kibichi lililonawiri na kustawi lilibadilishwa ghafla kuwa ardhi iliyojaa nyasi na miba. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuzikufuru neema kunaziondosha au kunazibadilisha kuwa nakama na kumsababishia mtu matatizo mbalimbali. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa adhabu za baadhi ya madhambi ikiwemo ya utovu wa shukurani humfika mtu papa hapa duniani na kuyaathiri maisha ya mtu binafsi, familia yake na jamii yake kwa jumla. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba Qur’ani inawausia watu kutalii kuhusu mambo yaliyozisibu kaumu zilizotangulia ili kupata mafunzo na ibra kwa ajili ya maisha yao ya leo.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 20 na 21 ambazo zinasema:

وَلَقَدْ صَدَّقَ عَلَيْهِمْ إِبْلِيسُ ظَنَّهُ فَاتَّبَعُوهُ إِلَّا فَرِيقًا مِّنَ الْمُؤْمِنِينَ

Na hakika Iblisi alihakikisha (imethibiti) ile dhana yake juu yao. Nao walimfuata, isipo kuwa kundi la Waumini.

 وَمَا كَانَ لَهُ عَلَيْهِم مِّن سُلْطَانٍ إِلَّا لِنَعْلَمَ مَن يُؤْمِنُ بِالْآخِرَةِ مِمَّنْ هُوَ مِنْهَا فِي شَكٍّ ۗ وَرَبُّكَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ حَفِيظٌ

Naye hakuwa na mamlaka yoyote juu yao, ila ni kwa sababu (ya kuwajaribu) tujue ni nani mwenye kuamini Akhera, na nani anaye tilia shaka. Na Mola wako Mlezi ni Mwenye kuhifadhi kila kitu.

Baada ya Iblisi kuwaghilibu Adam na Hawa alilaaniwa na Allah kwa kubaidishwa na kuwekwa mbali na rehma zake. Kwa sababu hiyo akaapa kuwa atahakikisha anawaghilibu na kuwapotosha wana wa Adam huku akiamini kuwa atafaulu katika njama yake hiyo. Aya hizi tulizosoma zinasema: kuhusu watu wa kaumu ya Sabaa, shetani alihisi amepata matarajio aliyokuwa nayo kwa kuthibiti alilotaka kwa sababu akthari ya watu walitekeleza matakwa yake ghairi ya wachache tu wenye imani ya kweli ambao hawakutekwa na ushawishi wake. Kisha Allah SW anatukumbusha kwa kutueleza kwamba msidhani kuwa shetani ana uwezo wa kuwateza nguvu watu na kuwalazimisha waasi na kufanya madhambi. Hasha! Anachofanya ni kutia wasiwasi; na ikiwa Mwenyezi Mungu amemwezesha yeye kufanya hivyo, ni kwa ajili ya kuwatahini watu. Yaani iweze kubainika nani kati yao wana imani ya kweli ya akhera na kwa hivyo hawatokubali kuathiriwa na wasiwasi wa shetani; na nani miongoni mwao wana shaka juu ya hilo na hivyo wapatwapo na wasiwasi mdogo tu wa shetani wanatumbukia kwenye lindi la madhambi. Kwa kawaida, watu wenye irada nyepesi na imani dhaifu huathiriwa kirahisi na matamanio ya nafsi au kuchochewa na vishawishi vya nje na huwa hawana istiqama na uwezo wa kukabiliana na vishawishi hivyo. Hakuna shaka yoyote kuwa Allah SW ni mjuzi na mwelewa wa amali zote za waja wake lakini halipi malipo ya thawabu au adhabu kwa kutegemea elimu yake. Kwa sababu haitoleta maana kumlipa mja wake malipo yoyote yale kabla ya kufanya amali ya kumstahikisha thawabu au iqabu. Ni sawa na mwalimu ambaye anajua kama mwanafunzi fulani ni hodari na anadurusu ipasavyo masomo yake, lakini hawezi kumtilia maksi nzuri ya kufaulu bila kwanza kumfanyia mtihani na kumsahihishia karatasi ya majibu yake. Ni wazi kuwa utambuzi tu na uelewa alionao mwalimu hautoshi kuwa kipimo cha uadilifu cha kutoa maksi kwa wanafunzi wake bali inapasa wao wenyewe waonyeshe kivitendo kwanza kiwango cha elimu na uhodari wao. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuzikufuru neema za Mwenyezi Mungu ni moja ya mambo yanayomfanya mtu aathiriwe kirahisi na ushawishi wa shetani. Watu wa kaumu ya Sabaa waliathiriwa na ushawishi wa shetani kwa sababu ya kuzikufuru neema za Mola. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kwa upande mmoja Mwenyezi Mungu amemfanya mwanadamu awe na hiyari ya kufanya au kutofanya atakalo, na kwa upande mwengine amempa akili na kumteremshia Wahyi wa kumuonyesha njia sahihi na isiyo sahihi ya kufuata. Mitume na mawalii wa Allah wanawaita watu kwenye mema na ya kheri shetani na watu wenye sifa za kishetani wakiwaelekeza kwenye maovu na mabaya. Katika hali hiyo mtu mwenyewe inampasa kwa irada na hiyari yake achague njia ya kufuata. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 765 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiqi ya kuifuata, na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh…/