Jan 16, 2018 10:49 UTC
  • Aya na Hadithi (2)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Hii ni sehemu ya pili ya kipindi chetu kipya ambacho tunakipeperusha hewani chini ya anwani ya Aya na Hadithi za Kiislamu.

Ndugu wasikilizaji, kati ya Aya za kitabu kitakatifu cha Qur'ani ambazo zimebainishwa fadhila zake kupitia Hadithi za Kiislamu na waumini kutakiwa kuzisoma kwa wingi na athari zake kuwekwa wazi na hadithi hizo ni Aya mashuhuri ya Kursiy. Katika kipindi kilichopita tulitaja baadhi ya Hadithi ambazo zinazungumzia suala hilo na katika kipindi cha leo tutazungumzia moja ya athari muhimu za kudumisha usomaji wa Aya hii tukufu na hasa katika kujikinga nayo dhidi ya hila na mitego ya shetani. Mwenyezi Mungu atuepushe sote na hayo kutokana na Baraka zake kwa kuwa Yeye ndiye anayesikia na kujibu maombi ya waja wake, Amin.

 

Wapenzi wasikilizaji, kipenzi na Bwana wetu al-Habib al-Mustafa (saw) amesema kama ilivyopokelewa katika kitabu cha al-Majazaat an-Nabi cha Sharif ar-Radhi na vitabu vinginevyo vya kuaminika kwamba: 'Kila kitu kina nundu (kibyongo) yake - yaani kilele chake – na nundu ya Qur'ani ni Surat al-Baqarah na katika Sura hii kuna bwana wa Aya zote za Qur'ani. Aya hii haisomwi kwenye nyumba yoyote iliyo na shetani ndani yake ila huondoka kwenye nyumba hiyo, nayo ni Aya ya Kursiy.'

Na hii wapenzi wasikilizaji, ndiyo madhumuni ya Riwaya zilizopokelewa kupitia madhehebu nyingine za Kiislamu kama inavyoashiriwa katika Riwaya iliyonukuliwa na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Jarallah az-Zamakhshari katika tafiri yake ya al-Kashhaf. Anasema katika mojawapo ya Hadithi zinazozungumzia fadhila za Aya ya Kursiy kwa kusema: 'Na katika hayo ni kauli ya Mtume (saw) inayosema: Aya hii haisomwi kwenye nyumba yoyote ila mashetani walioko kwenye nyumba hiyo huihama kwa muda wa siku thelathii na wala haingii humo mchawi mwanaume wala mchawi mwanamke kwa muda wa siku arubaini. Ewe Ali! Ifundishe Aya hii kizazi, mke na majirani zako, kwa sababu hakuna Aya yoyote iliyoteremshwa iliyo muhimu zaidi kuliko hii.'

 Naye Imam Ali (as) amenukuliwa akisema: 'Nilimsikia Mtume wenu (saw) akiwa kwenye mimbar akisema: Mtu anayesoma Aya ya Kursiy mwishoni mwa kila swala ya wajibu hakuna chochote kinachomzuia kuingia Peponi isipokuwa mauti, na wala halitekelezi jambo hili isipokuwa swiddiq (mkweli) au mcha-Mungu kweli. Na mtu anayeisoma anapokwenda kulala Mwenyezi Mungu humkinga na shari ya nafsi yake, ya jirani yake, ya jirani ya jirani yake na ya nyumba zinazomzunguka.'

 

Kwa maelezo haya wapenzi wasikilizaji tunafikia natija hii kwamba, kuzingatia na kusoma kwa wingi Aya ya Kursiy ni miongoni mwa ibada muhimu za Kiislamu ambazo humkinga mja na shari anapokuwa anatembea katika njia nyoofu ya kuelekea ukamilifu wa kimaanawi. Na hili ndilo jambo linalotuelekeza katika uazingatiaji wa Hadithi tukufu ifuatayo ambayo ni katika Hadithi Muhimu za Mtume Muhammad (saw). Imepokelewa katika kitabu cha Makarim al-Akhlaq na vitabu vingine muhimu kutoka kwa swahaba mtukufu Abu Dharr al-Ghafari (MA) kwamba alisema: 'Siku moja nilienda kwa Mtume (saw) na kumkuta akiwa ameketi peke yake msikitini. Nilitumia fursa hiyo, naye akasema (saw): Ewe Abudharr! Hakika msikiti una salamu za kutolewa. Nikasema na salamu hizo ni zipi Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Akasema kuswali rakaa mbili. Kisha nilimtazama na kusema:  Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Uliniamuru kuswali, swala ni nini? Akasema (saw): Swala ndiyo maudhui bora Zaidi. Hivyo mtu anayependa huswali kidogo na anayependa hukithirisha (huswali kwa wingi). Nikasema, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ni amali gani inayompendeza zaidi Mwenyezi Mungu Mtukufu? Akasema (saw): Imani juu ya Mwenyezi Mungu, kisha Jihadi katika njia yake. Nikasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ni muumini yupi aliyekamilika zaidi kiimani? Akasema: Yule aliye na tabia nzuri zaidi. Nikasema: Na ni muumini gani aliye bora zaidi? Akasema (saw): Yule ambaye Waislamu wanasalimika na ulimi na mkono wake. Nikasema: Na ni hijra gani iliyo bora Zaidi? Akasema (saw): Mtu anayehijiri kutoka kwenye maovu (anayeepuka maovu). Nikasema: Na ni usiku upi ulio bora zaidi? Akasema (saw): Usiku wa manane unaopita. Nikasema: Ni swala gani bora zaidi? Mtume (saw) akasema: Ni swala iliyo na kunuti ndefu. Nikasema: Ni swaumu gani bora zaidi? Akasema (saw): Ni swaumu ya faradhi na iliyo na malipo (maradufu) mara kadhaa zaidi mbele ya mwenyezi Mungu. Nikasema: Ni sadaka gani bora zaidi? Akasema (saw): Ni kumpa masikini kwa siri na kutoa wakati wa ukata. Nikasema: Na ni Zakaa gani iliyo bora zaidi? Akasema (saw): Ni ile iliyo ghali zaidi kwa bei na iliyo na thamani kubwa zaidi kwa mmiliki wake. Nikasema na ni Jihadi gani iliyo bora zaidi? Akasema (saw): Ni Jihadi ambayo damu ya muumini humwagwa na farasi wake kuchinjwa (kuuawa). Nikasema: Na ni Aya gani aliyokuteremshia Mwenyezi Mungu ambayo ni tukufu zaidi? Akasema (saw): Ni Aya ya Kursiy.'

***********

Wapenzi wasikilizaji, kuna athari nyingi mno ambazo zinatokana na usomaji wa Qur'ani ambazo tutazizungumzia katika kipindi kijacho cha Aya na Hadithi panapo majaliwa yake Allah. Basi hadi wakati huo kutoka Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran la ziada hatuna isipokuwa kukuageni huku tukikutakieni kila la heri maishani, kwaherini.