Aya na Hadithi (3)
Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran na karibuni kusikiliza sehemu ya tatu ya kipindi hiki kipya cha Aya na Hadithi.
Ndugu wasikilizaji, Hadithi tukufu zinashauri na kuwasihi waumini kusoma kwa wingi na kuzingatia kwa makini maana ya Aya Tukufu ya Kursiy ambayo inajadili na kuzungumzia madhumuni aali ya Tauhidi na upwekeshaji wa Mweyezi Mungu. Sisitizo hilo bila shaka linatokana na athari muhimu za Aya hiyo tukufu katika kumshinda shetani na vishawishi vyake kama tilivyoona katika kipindi kilichopita, na hivyo kutoa fursa kwa mwanadamu kufanya ibada halisi na ya ikhalsi kwa Muumba wake. Imepokelewa Hadithi katika kitabu cha Uyun Akhbar ar-Ridha (as) kutoka kwa Mtume Mtukufu (saw) ambayo inasema: 'Mtu anayesoma Aya ya Kursiy mara 100 ni kama kwamba amemwabudu Mwenyezi Mungu maisha yake yote.' Na Imam wetu Ja'ffar as-Swadiq (as) anasema kama ilivyopokelewa katika tafsiri ya al-Ayashi na tafsiri nyinginezo: 'Mtu anayesoma Aya ya Kursiy mara moja Mwenyezi Mungu humuondolea makuruhu (udhia) elfu moja kati ya makuruhu za dunia na makuruhu elfu moja kati ya makuruhu za Akhera, ambapo makuruhu rahisi zaidi kati ya makuruhu za dunia ni umasikini na makuruhu rahisi zaidi kati ya makuruhu za Akhera ni adhabu ya kaburi, na hakika mimi huisoma kwa matumaini ya kupandishiwa daraja na cheo.'

Ndugu wasikilizaji, kile kinachokusudiwa na Hadithi hii tukufu ni kutanabahisha kwamba uimarishwaji wa itikadi inayozungumziwa na Aya ya Kursiy, humuwezesha mja kuingia kwenye kinga imara ya Mwenyezi Mungu ambapo huitumia kinga hiyo kudhamini mahitaji yake yote ya humu duniani na huko Akhera. Akiwa katika hali hiyo, hutegemea kinga na ngao hiyo imara ya Mwenyezi Mungu katika utekelezaji wa majukumu na kufikia mahitaji yake yote muhimu yakiwemo madogo madogo kama vile ya kupandishwa cheo na daraja kama ilivyopokelewa katika Hadithi tuliyotangulia kuisoma kutoka kwa Imam Ja'ffar as-Swadiq (as). Katika hilo kuna ukamilifu wa ibada ya mwanadamu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, katika maisha yake yote.
*********
Wapenzi wasikilizaji, Hadithi Tukufu zinatuongoza na kutuelekeza kwenye nukta moja ya kuvutia na muhimu sana katika Aya nyingine mbili zinazoikamilisha Aya hii ya Kursiy, ambapo Aya hizo zinaunda mjumuiko wa kuvutia sana kuhusiana na Tauhidi halisi ya Mwenyezi Mungu. Hii ni kutokana na kuwa mjumuiko huo unatuelekeza kwenye uongozi wa Maumamu wa Haki (as) kama sharti muhimu la kuingia kwenye ngome imara ya neno la Tauhidi kama inavyoashiria ukweli huo Hadithi mashuhuri ya Silisila ya Dhahabu na hadithi nyinginezo sahihi na za kuaminika. Hebu na tusikilize kwa makini Aya mbili hizi kabla ya kukunukulieni Hadithi hiyo Tukufu ambayo itakubainishieni hakika muhimu ya Wilaya ya Tauhidi. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika aya hizo za 256 na 257 za Surat al-Baqarah: Hakuna kulazimisha katika Dini. Kwani Uwongofu umekwisha pambanuka na upotofu. Basi anayemkataa taghuti na akamuamini Mwenyezi Mungu bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti, kisichovunjika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua. Mwenyezi Mungu ni mtawala wa walioamini. Huwatoa gizani na kuwaingiza mwangazani. Lakini waliokufuru, watawala wao ni mataghuti. Huwatoa kwenye mwangaza na kuwaingiza gizani. Hao ndio watu wa Motoni, na humo watadumu.
Imepokelewa katika vitabu vya al-Kafi, Aamali cha Sheikh Tusi, Tafisr al-Ayashi na vinginevyo kutoka kwa Imam wetu, Mueneza wa Sunna ya Mtume (saw) al- Imam as-Swadiq (as), kwamba alisema katika Hadithi: 'Hana dini mtu anayemfuata imamu dhalimu asiyechaguliwa na Mwenyezi Mungu na wala halaumiwi mtu anayemfuata Imamu muadilifu aliyechaguliwa na Mwenyezi Mungu.' Mpokezi wa Hadithi akasema: 'Nikasema: 'Ewe mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu! Wao hawana dini na wala hawa hawalaumiwi?!' Akasema: 'Nam, wao hawana dini na wala hawa hawalaumiwi.' Kisha akasema (as): 'Kwani hausikii kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema: Mwenyezi Mungu ni mtawala wa walioamini. Huwatoa gizani na kuwaingiza mwangazani? Huwaondoa kwenye giza la madhambi na kuwaingiza kwenye mwangaza wa toba na maghfira kutokana na kufuata kwao kila Imam muadilifu aliyechaguliwa na Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anasema: Lakini waliokufuru, watawala wao ni mataghuti. Huwatoa kwenye mwangaza na kuwaingiza gizani. Akasema: 'Nikasema, je, Mwenyezi Mungu hakukusudia kwa hilo makafiri aliposema: Lakini waliokufuru?' Akasema: 'Kisha akasema: Na kafiri ana mwangaza gani hali yeye ni kafiri, hadi atolewe kwenye mwangaza huo na kupelekwa gizani? Bali Mwenyezi Mungu alikusudia kwa hilo kwamba, wao walikuwa kwenye nuru (mwangaza) ya Uislamu lakini walipoamua kufuata kila imamu dhalimu ambaye hakuchaguliwa na Mwenyezi Mungu, walitoka kwenye nuru ya Uislamu na kuingia kwenye giza la ukafiri kutokana na ufuasi wao huo wa maimamu dhalimu na waovu. Kutokana na hilo Mwenyezi Mungu aliwawajibishia moto pamoja na makafiri wengine, na hapo akasema: ' Hao ndio watu wa Motoni, na humo watadumu.'

Mwenyezi Mungu atujalie sote, wapenzi wasikilizaji, ukamilifu wa Taihidi na ibada Yake kwa baraka za kufuata na kushikamana na minara miwili ya wongofu wa walimwengu, yaani kitabu chake kitakatifu Qur'ani Tukufu na Ahlul Beit wa Mtume Wake mpendwa, Bwana wa Mitume Wake wote al-Habib al-Mustafa (saw), Allahumma Amin.
Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu cha Aya na Hadithi kwa juma hili. Msikose kujiunga nasi tena Juma lijalo, Inshaalah, kusikiliza kipindi kingine katika mfululizo wa vipindi hivi ambavyo tunatumai vitatunufaisha sote kwa pamoja. Kipindi hiki kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tunakushukuruni nyote kwa kuwa pamoja nasi hadi mwisho wa kipindi hiki. Basi hadi juma lijalo la zida hatuna isipokuwa kukutakieni nyote kila la kheri maishani, kwaherini.