Jan 27, 2018 04:15 UTC
  • Jumamosi, 27 Januari 2018

Leo ni Jumamosi tarehe 9 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1439 Hijria mwafaka na tarehe 27 Januari mwaka 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 653 iliyopita sawa na tarehe 9 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 786 Hijria, aliuawa shahidi faqihi na mtaalamu mkubwa wa hadithi Muhammad bin Jamaluddin Makki Amili, mashuhuri kwa jina la "Shahidi wa Kwanza." Alizaliwa mwaka 734 Hijria katika mojawapo ya vijiji vya Jabal Amil nchini Lebanon. Alijifunza elimu mbalimbali kutoka kwa walimu wakubwa wa zama zake kama vile Allama Hilli. Mbali na elimu ya dini, Muhammad bin Jamaluddin pia alikuwa hodari katika taaluma za mashairi na fasihi. Katika miaka 52 ya umri wake uliojaa baraka, Shahidi wa Kwanza aliandika vitabu vingi, ikiwa ni pamoja na "Albaqiyatus-Swalihat" na "al Lumuatu Dimashqiyya." Aliuawa na wapinzani wenye taasubi katika siku kama ya leo. ***

Shahidi wa Kwanza

 

Katika siku kama ya leo miaka 459 iliyopita alizaliwa katika mji wa Shiraz kusini mwa Iran Ṣadr al-Din, Muḥammad bin Ibrahim al-Shirazi maarufu kwa jina la Ṣadr al-Muta'allihīn na Mulla Sadra, mwanafalsafa na arif mkubwa. Awali alielekea katika mji wa Qazwin uliokuwa katika zama hizo mji mkuu wa utawala wa Safavi na kuhudhuria darsa na masomo ya walimu wakubwa kama Sheikh Bahai. Alisoma Fikihi, Usul, hadithi na hisabati kwa Sheikh Bahai na kusoma mantiki, falsafa na Irfan kwa Mirdamad. Baada ya Isfahan kufanywa mji mkuu, Mulla Sadra naye alihamia katika mji huo na kuanza kufundisha. Hata hivyo kutokana na mitazamo yake kupingana na maulama kadhaa, Mulla Sadra alilazimika kuuhama mji huo na kuanza kuishi katika kijiji cha karibu na mji wa Qum. Baada ya muda alianza tena kujishughulisha na kazi ya kufundisha na kualifu vitabu. al Mabdau Wal-Maad, Zaadul Musafir na Mutashabbihaat al-Qur'an ni baadhi tu ya vitabu vya Ṣadr al-Muta'allihīn au Mulla Sadra kama anavyojulikana pia.***

Mulla Sadra,

 

Miaka 127 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Ilya Ehrenburg mwandishi wa Umoja wa Kisovieti yaani Urusi ya zamani. Ilya alifanya kazi ya uandishi habari kwa miaka kadhaa huko Uhispania na kuanza kujishughulisha na utunzi wa mashairi pia. Ehrenburg alifahamika vyema nchini humo kama mwandishi wa hadithi na mwanahabari, khususan pale alipokuwa akiripoti matukio katika Vita vya Kwanza vya Dunia, vya Pili na vile vya ndani vya Uhispania. Mwandishi huyo wa Kirusi aliandika vitabu visivyopungua 100 ambapo miongoni mwake ni hivi alivyovipa majina ya "tufani" na "kuanguka Paris". Ilya alifariki dunia mwaka 1967. ***

Ilya Ehrenburg

Siku kama ya leo miaka 93 iliyopita sawa na tarehe 9 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1346 Hijria, Ayatullahil Udhma Sayyid Abu Turab Khonsari aliaga dunia. Khonsari alikuwa mmoja wa wasomi na maulama wakubwa na mashuhuri wa Iran. Alizaliwa huko Khonsar moja ya miji ya katikati mwa Iran na baada ya kumaliza masomo yake ya awali ya kidini alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini mjini Isfahan na baadaye huko Najaf Iraq. Ayatullah Khonsari alikuwa ametabahari pia katika uga wa uandishi wa vitabu na vitabu vya Misbahus Swalihiin na Qasdus Sabiil ni baadhi tu vitabu vyake mashuhuri. ***

Sayyid Abu Turab Khonsari

 

Na katika siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, makubaliano ya kusitisha vita kati ya Marekani na Vietnam Kaskazini yalitiwa saini mjini Paris, Ufaransa baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa kipindi cha miaka minne. Kwa mujibu wa makubaliano hayo ya Paris, Marekani ilikubali kuondoa majeshi yake huko Vietnam Kusini. Japokuwa baada ya kutiwa saini makubaliano hayo vita kati ya Marekani na Vietnam Kaskazini havikusitishwa, lakini serikali ya Washington ililazimika kuondoa majeshi yake huko Vietnam Kusini baada ya kupata hasara kubwa za hali na mali. Makubaliano ya Paris yalikuwa pigo kubwa kwa siasa za uingiliaji kati na za kibeberu za Marekani nchini Vietnam ambazo zilianza kutekelezwa mwaka 1964. 

Vita vya Vietnam