Feb 11, 2018 05:30 UTC
  • Jumapili, Februari 11, 2018

Leo ni Jumapili tarehe 24 Mfunguo Nane, Jamadil-Awwal 1439 Hijiria, inayosadiafiana na tarehe 11 Februari 2018 Miladia.

Miaka 2678 iliyopita katika siku kama ya leo, mfalme wa kwanza wa Japan maarufu kwa jina la Jimmu alishika madaraka ya nchi. Kwa utaratibu huo mfumo wa kale zaidi na uliobakia kwa kipindi kirefu wa kifalme duniani ambao ungali unaendelea hadi sasa, ulianzishwa. Wafalme wa Japan huwa na cheo cha heshima tu na Waziri Mkuu ndiye anayeendesha masuala ya nchi.

Bendera ya Japan

Siku kama ya leo miakka 401 iliyopita, alifariki dunia mjini Behshahr, Mazandaran moja ya miji ya Iran Shāh Abbās, mmoja wa wafalme wa silsila ya utawala wa Safavi. Katika utawala wa Shah Abbas, uliofahamika kwa jina la utawala wa Safavi, wasomi na maulama wakubwa walipewa nafasi kubwa kutokana na umuhimu wa nafasi yao. Kujengwa misikiti, mnara wa Naqsh-e Jahan wa mjini Isfahan, njia za chini ya ardhi za Kuhrang mjini Isfahan kwa ajili ya kupitishia maji, kuasisiwa kituo cha biashara ya hariri, kuanzishwa njia za misafara ya biashara ya hariri kutoka Isfahan na misafara mingine ya kibiashara sambamba na kuanzishwa sarafu mpya iliyotumiwa kote Iran kote, ni miongoni mwa hatua zilizotekelezwa na utawala huo. Baada ya kutawala kwa miaka 42 Shāh Abbās alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 59.

Shāh Abbās, mmoja wa wafalme wa silsila ya utawala wa Safavi

Siku kama ya leo miaka 368 iliyopita alifariki dunia René Descartes, mwanafalsafa na mtaalamu wa hisabati wa nchini Ufaransa. Alizaliwa tarehe 31 Machi 1596 Miladia na baada ya masomo yake ya msingi alianza kusomea hisabati na tiba. Baadaye Descartes alibobea katika fani ya hisabati na uhandisi huku muda mfupi baadaye akianzisha utafiti pia katika uga wa falsafa. Aidha msomi huyo wa Kifaransa alifanya safari kwa kipindi fulani katika nchi mbalimbali na baadaye aliishi Uholanzi na kuanza kufanya utafiti. Rene Descartes aliitambua hisabati kuwa elimu kamili miongoni mwa elimu nyinginezo na kutaka kutumiwa elimu hiyo katika fani nyinginezo za kielimu. Miongoni mwa vitabu vya mwanafalsafa huyo ni Principles Of Philosophy, The Passions of the Soul na Discourse on the Method.

René Descartes

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, serikali ya mpito ya Mapinduzi ya Kiislamu ilianza rasmi kazi zake katika siku za mwanzo kabisa za umri wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Wakati huo huo wananchi waliendeleza mapambano ya kuangamiza kikamilifu mabaki ya utawala wa Shah. Baadhi ya makundi ya wananchi yalichukua jukumu la kulinda taasisi muhimu za serikali katika miji mbalimbali. Wakati huo ulidhihiri udharura wa kuwepo chombo cha kushughulikia kadhia hiyo na kukabiliana na vibaraka na mabaki ya utawala wa Shah. Kwa msingi huo Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu hayati Imam Khomeini alitoa amri ya kuundwa Kamati ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran

Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita sawa na tarehe 11 Februari 1990, Mzee Nelson Mandela kiongozi wa harakati ya kupambana na ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini aliachiwa huru baada ya kufungwa jela kwa miaka 27. Mandela alikamatwa na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela mwaka 1963 kwa sababu ya mapambano yake dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini. Lakini baada ya miaka kadhaa aliachiliwa huru kutokana na msimamo wake thabiti akiwa jela, mapambano ya wananchi wa nchi hiyo pamoja na mashinikizo yaliyotokana na fikra za waliowengi duniani.

Mzee Nelson Mandela

Na siku kama ya leo miaka 7 iliyopita, Dikteta Hosni Mubaraka wa Misri ambaye alijitangaza kuwa rais wa maisha wa nchi hiyo aling'olewa madarakani kufuatia harakati za mapinduzi za wananchi. Hosni Mubarak ambaye alikuwa Makamu wa Rais Anwar Sadat wa Misri aliingia madarakani mwaka 1981 baada ya kuuawa kiongozi huyo. Anwar Sadat aliuawa na Khalid Islambuli afisa wa jeshi la Misri baada ya kusaini makubaliano ya Camp David na Israel. Mubarak naye baada ya kuingia madarakani aliendeleza mwenendo huo huo wa kuwatetea Wazayuni na kutekeleza siasa za Marekani na Israel katika eneo la Mashariki ya Kati. Ndani ya nchi pia Mubarak sambamba na kutangaza hali ya hatari ya muda mrefu alitekeleza siasa za kuwakandamiza wananchi hasa wanaharakati wa Kiislamu. Hayo na mengine mengi hatimaye yalipelekea Misri kuwa nchi ya kwanza kuathiriwa na vuguvugu la mwamko wa Kiislamu na wimbi la kukabiliana na udikteta lililoanzia nchini Tunisia na kuanguka utawala wa muda mrefu wa dikteta huyo wa Misri katika siku kama ya leo.

Dikteta Hosni Mubarak

Tags