Feb 12, 2018 23:25 UTC
  • Jumanne, tarehe 13 Februari, 2018

Leo ni Jumanne 26 Jamadil Awwal 1439 Hijria sawa na 13 Februari 2018.

Siku kama ya leo miaka 84 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Allamah Mirza Muhammad Hussein Naini, marjaa na faqihi mkubwa na mmoja wa wahakiki wa elimu ya usulu fiq’h. Allamah Naini alizaliwa mwaka 1276 Hijiria Qamaria mkoani Nain, ambao ni moja ya mikoa ya katikati mwa Iran katika familia ya kidini. Allamah Naini alisoma na kuhitimu masomo yake ya awali nyumbani kwao na kuendelea na masomo ya juu huko mjini Najaf, Iraq. Akiwa mjini hapo, alipata kusoma kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kama vile Allamah Mirza Shirazi na kufikia daraja ya juu ya elimu za hesabu, falsafa ya sayansi, falsafa, irfan na fiq’hi. Miongoni mwa athari za Allamah Naini ni pamoja na vitabu vya “Wasiilatun-Najjat” na “Tanbiihul-Ummah wa Tanziihul-Millah” kitabu ambacho kilitoa mchango mkubwa katika kuathiri mapambano dhidi ya viongozi dhalimu wa zama hizo.

Ayatullah Allamah Mirza Muhammad Hussein Naini

Tarehe 13 Februari miaka 760 iliyopita mji wa Baghdad uliokuwa makao makuu ya watawala wa Kiabbasi, ulitekwa na Hulagu Khan. Hulagu alimuua mtawala al Muutasimu Billah na kukomesha kabisa utawala wa kizazi cha Bani Abbasi uliotawala maeneo mengi ya ulimwengu wa Kiislamu kwa kipindi cha miaka 37. Katika unyama huo mkubwa, Hulagu Khan alifanya ukatili mkubwa na kuua nusu ya watu wasiokuwa na hatia wa mji wa Baghdad. Hulagu Khan pia alichoma moto nyumba na majengo mengi ya kihistoria ikiwemo maktaba kubwa ya Baghdad na idadi kubwa ya vitabu vyenye thamani kubwa vya maktaba hiyo viliteketea au kutumbukizwa katika mto Tigris.

Na siku kama hii ya leo miaka 1159 iliyopita alifariki dunia mshairi na mwandishi mashuhuri aliyekuwa na asili ya Iran, Ibn Abi Tahir Tayfur. Alizaliwa mwaka 204 Hijria huko Baghdad na baada ya kupata elimu ya msingi alijishughulisha na uandishi. Akiwa Baghdad alifahamiana na magwiji wa fasihi na lugha ya Kiarabu na kutokana na kipawa chake kikubwa alianza kutunga na kuandika mashairi. Alipata umashuhri kubwa katika uwanja huo. Msomi huyo alitoa mchango mkubwa katika fasihi ya lugha ya Kiarabu na ameandika vitabu kadhaa ikiwemo diwani yake ya mashairi.