Mar 07, 2018 11:51 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (16)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipita hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 16.

Katika kipindi kilichopita tulianza kumzungumzia mwanamagaeuzi na mrekebishaji umma mwengine wa Ulimwengu wa Kiislamu Rashid Ridha. Miongoni mwa tuliyoeleza kuhusu mwanafikra huyo ni kwamba, Rashid Ridha, ambaye kwa upande wa sha’ar na misingi ya urekebishaji wa dini alikuwa akiwafuata Sayyid Jamaluddin Asad Aabadi na Sheikh Muhammad 'Abduh, kinyume na mwalimu wake 'Abduh, alikuwa akitilia mkazo sana umoja wa Kiislamu sambamba na kuendelezwa Ukhalifa. Alikuwa akitaka kurejeshwa Ukhalifa katika muundo uleule wa zama za mwanzoni mwa Uislamu sambamba na kufanyiwa marekebisho na kuondolewa kasoro ulizokuwa nazo. Tukabainisha kuwa kiini cha fikra kuu za Rashid Ridha kuhusu Ukhalifa, badala ya kukita zaidi katika kumzingatia Khalifa mwenyewe, kinatilia mkazo kwenye "Ahlul-Halli wal-Aqd", yaani jopo la wawakilishi wa umma ambalo ndiyo msingi mkuu unaojenga utawala wa Kiislamu unaozungumziwa na mwanafikra huyo.

Huenda mtazamo wa Rashid Ridha wa kutojikita zaidi juu ya suala la "Khalifa" mwenyewe au hata "Mji wa Ukhalifa" ukawa umetokana na sababu za kisiasa, kwa sababu katika zama zake mtu aliyekuwa akipigania mno kushika wadhifa wa ukhalifa, yaani Sharif Hussein hakuwa mtu wa kuaminika na mwenye kutazamwa kwa jicho zuri na Rashid Ridha kutokana na tabia za kiimla alizokuwa nazo, kutokuwa na elimu na ujuzi wa masuala ya dini, kulijali na kulipendelea dola la kikoloni la Uingereza na vilevile upinzani wake dhidi ya harakati ya kuleta mageuzi ya kidini. Rashid Ridha alikuwa na shaka kubwa pia, kama Khalifa atakuwa wa Kishia ataweza kukubaliwa na Masuni; kwa sababu hiyo aliibua hoja kwamba hakuna ”Mgombea mwenye sifa kamilifu zinazotakiwa kwa Ukhalifa”; na kwa upande wa mahala, Hijaz na Istanbul hamukuwa mahala mwafaka mwa kuwa makao ya Khalifa; kwa hivyo akaibuka na wazo kwamba Ukhalifa unapasa kuhuishwa kwa njia ya mashirikiano baina ya Waturuki na Waaraabu wa Bara Arabu kwa kuangalia ni yupi baina yao mwenye sifa na masharti yanayotakiwa kwa ajili ya kuuhuisha Uislamu.

 

Rashid Ridha alizingatia uhalisia wa mambo na hivyo akakiri kuwa Waarabu na Waturuki hawajafikia kiwango kinachotakiwa cha maendeleo kuweza kuonyesha ushirikiano baina yao juu ya suala hilo; kwa sababu hiyo akapendekeza kwamba Ukhalifa inapasa uasisiwe katika eneo baina ya upande huu na ule yaani kati ya Bara Arabu na Anatolia ambako Waarabu, Waturuki na Wakurdi wanaishi pamoja. Rashid Ridha aliutaja mji wa Mosul na kueleza matumaini aliyonayo kwamba wakati eneo hilo lisiloelemea upande wowote litakapofanywa makao makuu ya Ukhalifa, nchi hizo za Kiislamu hazitozozania tena suala hilo; na Mosul, kama jina lake linavyoonekana ni “mahala pa kuunganisha”, kuleta maridhiano na kujenga mawasiliano na mafungamano ya kimaanawi. Mpango na ramani aliyochora Rashid Ridha kuhusu umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu ilikuwa inafanana katika mambo mengi na fikra ya kimageuzi ya Sayyid Jamaluddin Aabad Abadi na Muhammad Abdou, lakini pia fikra yake ilikuwa na nukta nyengine mpya kuhusu kuunganisha mfumo mkuu wa Ukhalifa na utawala wa Kiislamu pamoja na nchi tofauti na zinazojitawala za Kiislamu.

Ili kufanikisha na kufikia lengo la umoja na kuunda mfumo mmoja wa utawala wa Kiislamu, Rashid Ridha alipendekeza kubuniwa majimui ya kanuni zinazoendana na mataifa ya Waislamu katika zama hizo. Katika kubuni na kupanga majimui ya kanuni na taratibu hizo Rashid Ridha alikuwa akiitakidi kuwa kuna udharura wa kuzungumza na kushauriana na baadhi ya watu weledi, waelewa na wastahiki katika mataifa mbalimbali ya Kiislamu na akiamini kwamba watu hao wanapaswa kuoanisha hukumu na sheria za kifiqhi za madhehebu nne na Qur’ani na Sunna na kualifu kitabu cha majimui ya sheria na kanuni ambazo kabla ya kitu chochote zitokane na sheria za dini ya Mwenyezi Mungu na kuzingatia misingi mbalimbali ya hukumu za dini ikiwemo maslahi ya jamii, manufaa, kheri, saada na ustawi wa jamii wa Waislamu na baada ya hapo kuyatafutia majibu mahitaji ya zama hizo. Rashid Ridha alikuwa akiitakidi kuwa baada ya kupanga sheria hizo, Khalifa atapaswa kuzitekeleza yeye mwenyewe na kutoa miongozo pia inayohitajika kwa Maliwali katika ardhi zote za Kiislamu pamoja na kusimamia kwa umakini utekelezaji wake.

wahda

Mkutano wa Wahda mjini Tehran

 

Kwa muhtasari tunaweza kusema kuwa umoja, ushirikiano na kuwaamsha Waislamu na nchi za Kiislamu ni miongoni mwa daghadagha na mambo yaliyoishughulisha zaidi akili ya Rashid Ridha na kuchukua muda mwingi wa harakati zake. Harakati zake kuhusiana na masuala hayo zilijiakisi kupitia njia tatu. Ya kwanza ni makala alizokuwa akiandika katika jarida la Al-Manar na kuakisi habari na harakati za Waislamu ulimwengu mzima katika muelekeo wa kuleta ushirikiano na kuzikurubisha madhehebu za Kiislamu na umoja baina yao. Njia ya pili ni kupitia utoaji hotuba na indhari mbalimbali katika hafla za Kiislamu na maeneo ya elimu na mafunzo. Na njia ya tatu ni kuandika na kualifu vitabu kikiwemo cha Al-Wahdatul-Islamiyyah. Katika jarida la Al-Manar ambalo lilikuwa na wigo mpana wa kuakisi masuala ya maeneo mengi ya Ulimwengu wa Kiislamu, Rashid Ridha alikuwa akiandika makala mbalimbali kwa nia na madhumuni ya kuwakurubisha pamoja Waislamu. Alikuwa akitoa wito kwa maulamaa wa Ulimwengu wa Kiislamu kuchukua hatua za kujenga maelewano zaidi baina ya Waislamu kwa kubainisha mitazamo yao kwa ajili ya kuleta umoja baina yao. Aidha kupitia wito huo kuwawezesha Waislamu kueleza mishkili na matatizo yao pamoja na mas-ala ya kifiqhi yanayohitaji fatua za maulamaa hao. Kwa kulitumia jarida la Al-Manar, Rashid Ridha aliweza kujenga mtandao huo wa mawasiliano na maelewano baina ya Waislamu kuanzia Morocco na Tunisia za bara la Afrika mpaka India na Indonesia katika bara la Asia.

Mwanamageuzi na mwanafikra huyo wa kupigania umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu alikuwa akitoa indhari na kuwatahadharisha pia Waislamu na Waarabu juu ya hatari ya Uzayuni na njama za wakoloni dhidi yao na akawa anasisitiza kwa kutaka kuwepo umoja wa Kiislamu wa kukabiliana na Uzayuni na Ukoloni. Katika sehemu nyengine ya makala na maandiko yake katika jarida la Al-Manar, Rashid Ridha alikuwa akizihakiki na kuzikosoa hadithi za kutunga za Israiliyyat na kutokana na jitihada na idili kubwa aliyofanya ya kuzizuia zisienee katika mfumo wa kifikra wa Ulimwengu wa Kiislamu, aliweza kupunguza mifarakano na ukereketwa hasi wa kimadhehebu katika Ulimwengu wa Kiislamu. Katika zama ambapo wanamageuzi na wanafikra wapya wa Ulimwengu wa Kiarabu walikuwa wakipigia upatu fikra kama ya Umajimui wa Kiarabu, yaani Pan-Arabism, Uzalendo wa Kiarabu, yaani Arab-Patriotism na Vuguvugu la Kiarabu, Rashid Ridha alikuwa akisisitiza kwamba, njia pekee ya kujiondoa kwenye hali ya kulemaa na kubaki nyuma kimaendeleo na kufikia ustawi ni kupatikana umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu na kuzikurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu.

Wapenzi wasikilizaji, sehemu ya 16 ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu imefikia tamati. Natumai kuwa mumenufaika na kuelimika kutokana na yale mliyoyasikia katika kipindi hiki. Inshallah katika mfululizo ujao wa 17 tutakuja kumzungumzia Abdulrahman Al-Kawakibi, mrekebishaji mwengine wa Ulimwengu wa Kiislamu. Basi hadi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni kila la heri maishani…/