Mar 18, 2018 10:30 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (27)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 27.

Kwa wale mnaofuatilia kwa karibu kipindi chetu hiki bila shaka mngali mnakumbuka kuwa katika sehemu iliyopita ya 26 tulianza kuzungumzia fikra na mitazamo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei kuhusu suala la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu na mazungumzo yetu yaliishia pale tulipoeleza kwamba, mlinganiaji huyo wa umoja wa Kiislamu anaitakidi kwamba hatua za kutusiana na kuvunjiana heshima za baadhi ya makundi ya Kishia na Kisuni zinafanyika kufanikisha malengo ya maadui wa Uislamu; na anayakanya vikali makundi yote mawili kwa kuyataka yajiepushe na mambo hayo. Ayatullah Khamenei anasema: "Suni na Shia kila moja wana hafla zao za kimadhehebu, desturi zao, ada zao na majukumu yao ya kidini wanayotekeleza na inapasa wayatekeleze; lakini mstari mwekundu ni kwamba haifai abadani kusemwa kitu cha kusababisha wao kutengana kwa sababu ya hatua za kuyatusi matukufu ya upande mmojawapo, iwe inayochukuliwa na baadhi ya Mashia kwa sababu ya kujisahau, au inayochukuliwa pia na baadhi ya Masuni kama Masalafi na mfano wao kutokana na kujisahau. Hili ndilo jambo analotaka adui. Hapa pia inapasa kuwepo na umakini".  Wakati alipofutu mas-ala kuhusu kumvunjia heshima Bibi Aisha, mke wa Bwana Mtume SAW, Ayatullah Khamenei alieleza katika fatua yake kwamba kufanya hivyo ni haramu. Amesema: "Kuzitusi nembo za ndugu zetu Ahlu-Sunnah ikiwemo kumzushia tuhuma mke wa Mtume (Aisha) ni haramu. Maudhui hii inajumuisha wake wa Mitume wote hususan Bwana wa Manabii, Mtume mkubwa kabisa Mtukufu Muhammad SAW".

 

Ayatullah Khamenei ameyakosoa vikali baadhi ya matapo ya Kishia yenye mfungamano na maajinabi ambayo yanakoleza moto wa hitilafu kwa kuyatusi na kuyavunjia heshima matukufu ya Masuni na kuyataja makundi hayo kuwa ni walelewa wa vyombo vya usalama vya mkoloni kizee yaani Uingereza. Anasema: "Sisi hatuukubali Ushia ambao kitovu na kituo chake kikuu cha tablighi ni London; huu sio Ushia walioueneza na walioutaka Maimamu (AS). Ushia ambao msingi wake ni kuzusha hitilafu, msingi wake ni kusafisha na kunyoosha njia kwa ajili ya uwepo wa maadui wa Uislamu, huu sio Ushia; huu ni upotofu. Ushia ni dhihirisho lililokamilika la Uislamu halisi, ni dhihirisho la Qur'ani. Sisi tunawaunga mkono watu wanaosaidia kupatikana umoja na tunawapinga watu wanaofanya mambo yaliyo dhidi ya umoja." (Hotuba aliyotoa tarehe 17 Agosti, 2015). Anauelezea pia uundwaji na harakati za mapote ya kitakfiri ya Kisuni kuwa nayo pia lengo lake ni kusababisha ufa na mpasuko katika safu za umma wa Kiislamu na kuyataja mapote hayo kuwa ni matokeo ya kazi ya Marekani. Ayatullah Khamenei anafafanua zaidi kwa kusema: "Ulimwengu wa leo wa Uislamu unahitajia zaidi umoja kuliko wakati mwengine wowote ule. Mfarakano na ukufurishaji ni balaa lililowakumba Waislamu ambao wote wanasali kwa kuelekea Kibla kimoja na wana Kitabu kimoja cha mbinguni. Wanamwabudu Mungu mmoja na nyoyo zao zina mapenzi na Mtume wao wa mwisho. Maadui wa Uislamu wanapiga ngoma ya kuchochea mifarakano baina ya Waislamu wakati huu kuliko walivyowahi kufanya wakati wowote ule na wanachowaza akilini mwao ni kuzidhibiti ardhi za mataifa ya Waislamu. Katika wakati kama huu umoja ndio kinywaji cha dawa ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu anawataka waja wake waumini wajigange nayo. Kuitikia wito huu wa Mwenyezi Mungu kutafungua njia ya saada na izza kwa waumini." (Hotuba ya tarehe 15 Agosti, 2015). Akizungumzia nafasi ya madola ya kikoloni na kiistikbari katika kuzusha na kuchochea moto wa mfarakano baina ya Waislamu, Ayatullah Khamenei anasema: "Bila shaka Waingereza walikuwa ndio wataalamu wa kazi hii; wao wana utaalamu wa kuzusha hitilafu za kimadhehebu; na Wamarekani nao wamejifunza kwao wao, na leo hii wanaifanya kazi hii kwa uwezo wao wote. Haya makundi ya ukufurishaji mnayoyaona, yote haya yameundwa na wao". (Hotuba hiyo hiyo).

Kwa mtazamo wa Ayatullah Khamenei, kuna misingi miwili muhimu na yenye udharura wa kufanyiwa kazi katika harakati zenye lengo la kufanikisha kupatikana umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu. Msingi mmoja ni kuondoa hitilafu, migongano, mapigano na vizuizi vinavyokwamisha lengo hilo; na msingi mwengine ni kuzielekeza harakati zote za pamoja kwenye lengo la kuutawalisha Uislamu. Katika kulitolea ufafanuzi suala hilo, Ayatullah Khamenei anasema: "Katika suala la umoja kuna nukta mbili au mielekeo miwili ya msingi ambayo kila mmoja peke yake una umuhimu maalumu. Tunapotoa wito wa shime wa umoja, tunapaswa kuzizingatia nukta hizi mbili za msingi; na nukta hizi ndizo zenye taathira kwa maisha ya kivitendo ya Waislamu. Moja ya nukta hizi mbili ni kuondoa hitilafu, migongano, mapigano na vizuizi ambavyo vimekuwepo tangu karne kadhaa nyuma hadi hii leo baina ya makundi na madhehebu za Waislamu; na kila mara migongano hii imesababisha madhara kwa Waislamu. Nukta ya pili ni kwamba umoja huu utumike na uwe kwa ajili ya kuufanya Uislamu utawale, la kama si hivyo utakuwa kitu kisicho na maana yoyote" (Hadithi ya Wilayat, juzuu ya 5, ukurasa wa 243).

Kongamano la Umoja wa Kiislamu Tehran

 

Wapenzi wasikilizaji, baada ya kubainisha hayo, katika sehemu hii ya kipindi chetu cha leo tutaashiria pendekezo la kivitendo lililotolewa na Ayatullah Khamenei kwa ajili ya kufanikisha lengo la kufikiwa umoja wa Kiislamu, ambalo ni kuasisiwa Jumuiya ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu.

Kwa mtazamo wa Ayatullah Khamenei amali za minasaba mbalimbali ya kidini ni moja ya hazina zenye thamani kubwa kwa ajili ya kufikiwa umoja wa Kiislamu; na amali ya Hija, ambayo ni dhihirisho la umoja wa kiitikadi na kifikra baina ya Waislamu ni njia muhimu zaidi ya kuitumia kwa ajili ya kufanikisha lengo hilo. Kwa mtazamo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mkusanyiko wa Hija ni fursa bora ya kuziunganisha pamoja fikra za Waislamu na kubainishwa madukuduku ya pamoja ya umma wa Kiislamu. Anafafanua zaidi kuhusu nukta hiyo kwa kusema: "Sisi tunaitakidi kuwa Uislamu, umelifanya suala la umoja baina ya Waislamu na kuunganisha pamoja nguvu za wanaomwamini na kumpwekesha Mwenyezi Mungu kuwa moja ya faradhi (za dini). Sisi tunaamini kwamba moja ya malengo makubwa zaidi ya kuhiji Nyumba ya Mwenyezi Mungu ni kuwakurubisha pamoja Waislamu. Ni pale Mwenyezi Mungu aliposema katika aya ya 27 ya Suratul-Haj kwamba: "Na watangazie watu Hija; watakujia kwa miguu na juu ya kila ngamia aliye konda, wakija kutoka katika kila njia ya mbali. Na ni kwa sababu hiyo inawakusanya Waislamu wote duniani katika siku maalumu na katika maeneo mahususi yaliyoainishwa kama Arafa, Mash'ar, Mina na katika Msikiti Mtukufu. Kwa nini hawa wana hofu kiasi hiki ya Waislamu kujuana?! Suala ni kwamba umoja wa Kiislamu na kuwa na muelekeo mmoja, mtazamo mmoja na kauli moja Waislamu ni hatari kwa Uistikbari na hasahasa haini Marekani na kwa nyenzo zake kwenye vyombo vya ubeberu duniani." (Hadithi ya Wilayat, Juzuu ya 4, Ukurasa wa 297).

 Wapenzi wasikilizaji, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki, sina budi kuishia hapa kwa leo nikitumai kuwa mtajiunga nami tena inshaaAllah juma lijalo katika siku na saa kama ya leo katika mfululizo mwengine wa kipindi hiki. Basi hadi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni kila la heri maishani.