Apr 21, 2018 11:04 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (50)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 50.

Kwa wale mnaofuatilia kwa karibu kipindi hiki bila shaka mnakumbuka kuwa katika sehemu ya 49 ya mfululizo huu tulisema, aliyekuwa rais wa Misri Anwar Saadat alikuwa kiongozi wa kwanza wa nchi ya Kiarabu kuchukua hatua ya kufanya suluhu na Israel na kuutambua rasmi utawala huo haramu wa Kizayuni.   Moja ya matokeo hasi ya mkataba wa Camp David yalikuwa ni kuzuka hitilafu na mgawanyiko kati ya nchi za Kiarabu. Hadi kabla ya kusainiwa mkataba huo, Israel ilikuwa adui wa nchi zote za Kiarabu, lakini nchi hizo ziligawanyika makundi matatu baada ya Misri kujitoa kwenye safu hiyo. Kundi la kwanza lilikuwa la nchi ambazo ziliupinga mkataba huo na likawa maarufu kama "Harakati ya Msimamo Endelevu". Nchi kama Libya, Iraq, Yemen ya Kusini, Syria, Algeria na Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) zilikuwa katika kundi hilo. Kundi la pili lilikuwa la nchi zilizounga mkono hatua ya Misri ya kusaini mkataba wa suluhu na Israel wa Camp David.  Nchi kama Morocco, Sudan na Oman zilikuwa katika kundi hilo. Na kundi la tatu lilijumuisha nchi ambazo hazikuchukua msimamo wa kuunga mkono kundi lolote kati ya hayo mawili kuhusiana na mkataba wa Camp David. Saudi Arabia, Jordan pamoja na nchi nyengine za kandokando ya Ghuba ya Uajemi zilikuwemo kwenye kundi hilo. Miongoni mwa hatua na radiamali muhimu zilizoonyeshwa kuhusiana na mapatano ya Camp David ni msimamo uliochukuliwa na PLO. Mnamo tarehe 19 Septemba mwaka 1978, harakati hiyo ya ukombozi wa Palestina ilitoa taarifa maalumu ya kuulaani na kuushambulia kwa maneno makali mkataba wa Camp David pamoja na rais mwenyewe wa Misri Anwar Saadat na kutamka kwamba mkataba huo umedhihirisha jinsi Saadat alivyosalimu amri kikamilifu mbele ya mpango wa Begin unaotilia nguvu kuendelezwa mwenendo wa ukaliaji wa mabavu wa wazayuni katika ardhi za Palestina, miinuko ya Golan ya Syria na hata baadhi ya sehemu za eneo la Sinai la Misri. Kongamano la kitaifa la Palestina lililofanyika tarehe Mosi Oktoba 1978, nalo pia lilitoa taarifa, ambapo lililaani mazungumzo na makubaliano ya Camp David na kusisitiza kwamba mazungumzo hayo yamepuuza haki ya wananchi wa Palestina ya kuamua juu ya mustakabali wa taifa lao.

Ndani ya ukumbi wa mikutano Waislamu wa kona mbalimbali za dunia wakijadiliana mambo yao mjini Tehran, Iran

 

Huko nchini Syria rais wa nchi hiyo wakati huo Hafidh Al-Assad naye pia aliuzungumzia mkataba wa Camp David, ambapo katika hotuba aliyotoa mjini Damascus kwenye hafla ya ufunguzi wa mkutano wa tatu wa viongozi wa Harakati ya Msimamo Endelevu aliyalaani vikali makubaliano hayo. Azimio lililotolewa mwishoni mwa mkutano huo liliulaani msimamo wa rais Anwar Saadat wa Misri wa kusalimu amri na kufikia mapatano na adui Mzayuni na Ubeberu huko Camp David, kwa kula njama dhidi ya umoja wa Waarabu na kwa kuchukua hatua ambazo zililenga kuipa kisogo na kuipuuza kadhia ya Palestina pamoja na kuvuruga na kuyatibua mafanikio ya kisiasa liliyopata taifa la Palestina. Azimio hilo aidha liliulezea mkataba wa Camp David kuwa ni sehemu ya operesheni kubwa na pana ya ubeberu wa Marekani na Uzayuni ya kujijengea satua na ushawishi wa kuihodhi Misri, Ulimwengu wa Kiarabu na Bara la Afrika. Nchini Libya nako aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddafi aliushambulia vikali na kuulaani mkataba wa Camp David pamoja na Saadat mwenyewe kwa kile alichokitaja kuwa ni kuiondoa Misri kwenye safu ya Waarabu na uwanja wa mapambano na kumtambua rasmi adui ambaye ameighusubu na kuikalia kwa mabavu ardhi ya Waarabu ambayo ni ardhi ya Palestina. Nalo Baraza la Kamandi ya Mapinduzi ya Iraq lilitoa taarifa maalumu ya kulaani njama na uhaini uliofanywa Camp David na kutangaza kuwa Iraq ni sehemu ya medani ya kaskazini ya kijeshi katika kubariziana na adui Mzayuni, hivyo iko tayari kupeleka vikosi vyake vya jeshi upande wa medani ya Syria.

*******************

Katika kipindi cha baina ya kufanyika mazungumzo ya Camp David mwaka 1978 hadi kutiwa saini rasmi mkataba huo mwaka 1979 mjini Washington; radiamali na jibu la pili muhimu la Ulimwengu wa Kiarabu lilitolewa baada ya kikao cha nchi za " Harakati ya Msimamo Endelevu". Kikao cha viongozi wa nchi za Kiarabu kilifanyika Novemba mwaka 1978 katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad na ikaamuliwa kwamba ofisi kuu ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) iondolewe Cairo, Misri na kuhamishiwa mji mkuu wa Tunisia, Tunis. Vikwazo kadhaa pia vilipitishwa dhidi ya Misri. Huo ulikuwa ujumbe muhimu wa malalamiko kwa Cairo wa kuishinikiza ikatae kusaini makubaliano rasmi ya mkataba wa udhalilishaji wa Camp David. Hata hivyo Saadat hakuujali wito huo; badala yake akafika Ikulu ya White House akiwa bega kwa bega na Waziri Mkuu wa utawala wa kizayuni Minachem Begin na rais wa Marekani Jimmy Carter na kusaini mkataba huo. Waarabu nao wakaamua kufunga balozi zao mjini Cairo na kuvunja uhusiano wao wa kibiashara na kisiasa na Misri. Baada ya kuiona Misri imesaini mkataba wa Camp David, Israel, ambayo ilijiona sasa imepumua kwa kuepukana na tishio la moja ya kambi kuu ambayo ingeweza kuichachafya, mnamo mwaka 1982 iliishambulia na kuivamia kijeshi Lebanon kwa lengo la kufanikisha malengo yake matatu; ambayo ni kuwatimua wapiganaji wa msituni wa Kipalestina waliokuweko Lebanon, kuviondoa vikosi vya jeshi la Syria vilivyokuweko nchini humo pia, na kuiweka madarakani serikali ya Wakristo wa Kimaroni yenye muelekeo sawa na wake ili kuweza kuutambua rasmi utawala huo wa Kizayuni. Wakati Misri iliporidhia kufikia suluhu ya udhalilishaji na Israel takribani nchi zote za Kiislamu zilipinga suala hilo, hata hivyo haukuhitajika muda wa miaka mingi kabla ya kuongezeka idadi ya waliojiunga na safu ya kufanya mapatano na utawala huo wa Kizayuni kwa kujitokeza pia Jordan na hata Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) chini ya uongozi wa Yasir Arafat.

Mwito wa Umoja

 

Wapenzi wasikilizaji, ni wazi kwamba kadhia ya Palestina ni fursa adhimu na mhimili muhimu wa kuleta umoja katika umma wa Kiislamu wa kukabiliana na adui mkubwa wa Waislamu, yaani utawala wa Kizayuni wa Israel. Kama tulivyotangulia kueleza, umma mzima wa Kiislamu una kauli moja juu ya suala la kurejeshwa haki za Wapalestina; hata hivyo ikiwa nchi za Kiislamu hazitokuwa na uelewa kuhusu dhati ya uadui ilionao Israel kwa Uislamu na maslahi ya Waislamu, haitowezekana kupatikana umoja wa Kiislamu. Kwa takribani miaka 70 sasa Ulimwengu wa Kiislamu unakabiliwa na adui huyo; hata hivyo imetokea kwa nadra uadui huo kuwa sababu ya kuungana Waislamu, kwa sababu bado haujapatikana uelewa kamili wa uadui wenyewe miongoni mwa Waislamu na hasa viongozi wa nchi za Kiislamu. Siku ya Kimataifa ya Quds ni fursa adhimu na mwafaka kabisa kwa umma wa Kiislamu kupaza sauti za kuwazindua na kuwaamsha viongozi wa mataifa ya Kiislamu waliolala au waliohadaika ili kuweza kuwa na umoja wa Kiislamu kwa kushikamana na lengo lao tukufu na la pamoja, yaani kuikomboa Quds tukufu na kupigania haki za wananchi madhulumu wa Palestina kwa kukabiliana na adui wao wa pamoja, yaani Israel.

Hakuna shaka kwamba umma wa Kiislamu umeshazinduka; na Palestina itarejea kwenye nafasi yake katika mwamko wa Kiislamu; na baada ya muda si mrefu mashinikizo ya wananchi kwa viongozi wao yatazihamasisha serikali za mataifa ya Waislamu kuchukua maamuzi kwa lengo la kuimarisha na kudumisha umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu. Na bila ya shaka viongozi ambao hawatoweza au hawatotaka kujiunga na mkondo wa mwamko wa wananchi Waislamu wa eneo watatengwa na kubaki peke yao.

Wasikilizaji wapenzi, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki sina budi kuishia hapa kwa leo nikiwa na matumaini kuwa mtakuja kujiunga nami tena wiki ijayo inshallah katika siku na saa kama ya leo katika sehemu nyengine ya mfululizo huu. Nakuageni basi, huku nikikutakieni kila la heri maishani

Tags