May 04, 2018 08:10 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (55)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 55.

Kwa wale wanaofuatilia kipindi hiki kwa karibu bila shaka mnakumbuka kuwa katika vipindi kadhaa vilivyopita tulizungumzia chimbuko na malengo ya kuasisiwa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu ikiwa ni moja ya nembo na vielelezo vya kupatikana muelekeo na sauti moja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Tulieleza kwamba kitu ambacho kilikuwa chachu ya kuasisiwa Jumuiya ya OIC ni tukio la kuchomwa moto msikiti mtukufu wa Al Aqsa, kibla cha kwanza cha Waislamu lililotokea mwaka 1969. Tulifafanua kuwa hujuma hiyo iliyofanywa na myahudi mmoja mwenye taasubi iliamsha ghadhabu za Waislamu duniani. Tukaashiria pia kwamba Saudi Arabia na Morocoo zilikuwa miongoni mwa nchi ambazo katika kipindi hicho zilifanya jitihada kubwa za kufanikisha kufanyika mkutano wa kujadili kadhia hiyo ambapo hatimaye mnamo mwezi Septemba mwaka 1969, mkutano huo ukafanyika katika mji mkuu wa Morocco, Rabat. Katika mkutano huo uliohudhuriwa na viongozi wa nchi 25 za Kiislamu zilijadiliwa ajenda tatu kuu ambazo ni hujuma ya kuchomwa moto msikiti wa Al Aqsa, kukaliwa kwa mabavu ardhi za Waarabu na Israel na hali ya mji wa Baitul Muqaddas. Kama nilivyokuahidini katika sehemu ya 54 ya kipindi hiki, leo na katika vipindi vyengine kadhaa vijavyo tutazungumzia hatua muhimu zaidi zilizochukuliwa na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu, ambayo sasa ni Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, katika kuleta umoja na mshikamano kati ya nchi za Kiislamu.

Wapenzi wasikilizaji, hivi sasa ni takriban nusu karne imepita tangu kuasisiwa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu. Katika kuifanyia tathmini jumla na yenye kuzingatia malengo makuu ya kuasisiwa kwake, ambayo ni kupatikana sauti moja na umoja kati ya nchi za Kiislamu, tunaweza kuugawanya umri wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu katika vipindi vinne tofauti. Kipindi cha kwanza ni cha muongo wa kwanza wa kuasisiwa jumuiya hiyo. Sifa muhimu zaidi iliyokuwa nayo Jumuiya ya Nchi za Kiislamu katika kipindi hicho ilikuwa ni kujengeka utambulisho wake kwa kujikita kwenye lengo tukufu la Palestina. Awamu ya pili ya umri wa jumuiya ya OIC ni ya kipindi cha chini kidogo ya miongo miwili cha baina ya wakati ulipofanyika mkutano wa tatu hadi ulipofanyika mkutano wa nane wa jumuiya hiyo hapa mjini Tehran ambapo kitu cha msingi zaidi kilichoshuhudiwa katika kipindi hicho ni kuhuika hamu ya uchukuaji misimamo ya pamoja na kuwa na sauti moja nchi wanachama.

 

Kipindi cha tatu katika umri wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu kinaanzia pale ulipofanyika mkutano wa Tehran mwaka 1997, na kuendelea hadi lilipoibuka vuguvugu la umma wa Waislamu katika nchi nyingi za Kiarabu katika miaka ya 2011 na 2012. Katika kipindi hicho, muelekeo wa kuwa na sauti moja nchi za Kiislamu ulipata nguvu na kuongezeka kwa kiwango cha kuridhisha. Na kipindi cha nne kinahusiana na wakati nchi nyingi zenye tawala za kiimla na kidikteta zilipochukua hatua ya kukabiliana na matukio yaliyojulikana kama Mwamko wa Kiislamu, ambapo mifarakano na utengano ulishamiri katika Ulimwengu wa Kiislamu na baina ya nchi wanachama wa OIC. Taarifa ya mwishoni mwa mkutano uliofanyika Istanbul, Uturuki inadhihirisha kufikia upeo wa juu kiwango cha hitilafu hizo.

Katika awamu ya kwanza, yaani kipindi cha kati ya mkutano wa kwanza na wa pili wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu, iliyochukua takribani muda wa muongo mmoja, mikutano miwili katika ngazi ya viongozi wakuu wa nchi wanachama ilifanyika katika mji wa Rabat, Morocco na Lahore, Pakistan. Katika kipindi hicho, jumuiya ya OIC ilijitahidi kujenga utambulisho wake mkuu ambao unatokana na misingi na malengo yaliyobainishwa kwenye hati ya jumuiya hiyo. Katika mkutano wa kwanza, mbali na kutiliwa mkazo kuimarishwa mshikamano wa nchi za Kiislamu kwa kuzingatia thamani za Kiislamu, kutangaza kufungamana kwao na Hati ya Umoja wa Mataifa na Tangazo la Haki za Binadamu, pamoja na kufanya juhudi za kudumisha amani na usalama kwa madhumuni ya kupanua ushirikiano baina yao, nchi washiriki zilitangaza kughadhibishwa na tukio la kuchomwa moto msikiti wa Al Aqsa. Viongozi wa nchi 25 waliohudhuria mkutano huo walitaka mji wa Baitul Muqaddas urejeshwe kwenye hali yake ya kabla ya mwezi Juni mwaka 1967.

Katika mkutano huo, nchi wanachama wa OIC zilitoa wito kwa nchi zote duniani na hasa Ufaransa, Uingereza, Shirikisho la Kisovieti la Urusi pamoja na Marekani wa kuzitaka zisipuuze mfungamano mkubwa walionao wafuasi wa dini ya Uislamu kwa mji wa Baitul Muqaddas na uamuzi wa serikali za nchi za Kiislamu wa kutaka kukombolewa mji huo. Lakini zaidi ya hayo watangaze rasmi kwamba kuendelea kukaliwa kijeshi na Israel ardhi za nchi za Kiarabu kuanzia Juni 1967 kumezidi kuwatia wasiwasi wananchi na serikali za nchi za Kiislamu na kwa hivyo wachukue hatua zinazotakiwa kuhakikisha askari wote wa Israel wanaondoka haraka katika ardhi hizo. Viongozi wa nchi za Kiislamu waliohudhuria mkutano huo vilevile walitangaza kwamba wanawaunga mkono kikamilifu wananchi wa ardhi ya Palestina na mapambano yao ya kuikomboa ardhi yao na kurejeshewa haki zao.

 

Mkutano wa pili wa viongozi wa nchi wanachama wa OIC ambao ulifanyika katika mji wa Lahore nchini Pakistan ulichukua maamuzi kadhaa katika uga wa kisiasa na kiuchumi. Katika uga wa kisiasa, Jumuiya ya Nchi za Kiislamu iliunga mkono kikamilifu hatua halali kisheria za watu wa Misri, Jordan, Syria na Palestina za kupigania kukomboa ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu na Israel na ikazitaka nchi wanachama zichukue hatua za kila upande kuushinikiza utawala wa Kizayuni wa Israel uondoke bila masharti yoyote katika ardhi zote unazozikalia kwa mabavu. Lakini pia ikazitolea wito, hasa nchi zenye uhusiano na Israel, kuvunja uhusiano wao na utawala huo haramu ili kutoa msukumo kwa umoja wa Kiislamu. Katika uga wa kiuchumi pia, nchi washiriki zilipitisha mpango maalumu na kukubaliana kuunda kamati ya kuratibu ushirikiano na mataifa mengine ya Waislamu ili kuweza kufikia malengo ya kiuchumi na ya masuala yenye manufaa kwa mataifa hayo yote.

Katika mkutano huo iliamuliwa uanzishwe mfuko utakaopewa jina la Mfuko wa Umoja wa Kiislamu kwa madhumuni ya kuinua kiwango cha mshikamano, kuzipa nafasi ya juu thamani na utamaduni wa Kiislamu na kuongeza idadi ya vyuo vikuu vya nchi za Kiislamu; na ikaafikiwa kwamba kila nchi mwanachama ichangie kusaidia mfuko huo kulingana na uwezo wake kifedha.

Wapenzi wasikilizaji, muda uliotengwa kwa ajili ya sehemu ya 55 ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu umefikia tamati. Hivyo sina budi kuishia hapa kwa leo nikitumai kuwa mumefaidika na kunufaika na yale mliyoyasikia katika kipindi chetu cha leo. Basi hadi wiki ijayo inshaallah tutapokutana tena katika sehemu ya 56 ya mfululizo huu nakuageni huku nikikutakieni heri na fanaka maishani.

Tags