May 04, 2018 08:12 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (56)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 56.

Kwa wale mnaofuatilia kwa karibu kipindi hiki bila shaka mnakumbuka kuwa katika vipindi kadhaa vilivyopita tumeanza kuzungumzia Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC, ambayo sasa inajulikana kama Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu. Tumesema kuwa mkutano wa pili wa viongozi wa nchi wanachama wa OIC ambao ulifanyika katika mji wa Lahore nchini Pakistan ulichukua maamuzi kadhaa katika uga wa kisiasa na kiuchumi. Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa katika kipindi hicho utambulisho asili wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu wa kufungamana na kadhia ya Palestina ulijengeka, na miche ya mmea wa umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu ilichipua na kujitokeza japokuwa baadhi ya mambo yalichangiana pamoja kuhakikisha umoja na mshikamano huo hauthibiti kivitendo.

Moja ya sababu hizo ni kutotekeleza nchi wanachama yale yaliyopitishwa kwenye vikao vya OIC. Kwa kutoa mfano ni kwamba licha ya nchi wanachama kukubaliana kwa kauli moja kuhusu kuwahami na kuwaunga mkono wananchi wa Palestina na kupigania kukomboa ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu, suala ambalo linakwenda sambamba na manufaa na maslahi ya nchi za Kiarabu, nchi ya Misri ilijiamulia peke yake kuchukua uamuzi wa kufanya mapatano na Israel; na hatua hiyo ikapelekea nchi hiyo kufukuzwa kwenye Jumuiya ya Nchi za Kiislamu.

Kipindi cha pili cha umri wa Jumuiya ya OIC, yaani kuanzia pale kilipofanyika kikao cha tatu hadi wakati Iran ilipokuwa mwenyeji wa mkutano wa viongozi wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo katika kikao kilichofanyika mjini Tehran mwaka 1997, kinajumuisha vipindi kadhaa vilivyoshuhudia mabadiliko katika Ulimwengu wa Kiislamu ambapo kutokana na mizozo na migogoro iliyozuka baina ya nchi wanachama, hali fulani ya mgawanyiko na utengano ilijitokeza ndani ya jumuiya ya OIC na kufifisha nuru ya mwanga wa matumaini ya kupatikana umoja iliyokuwa imejitokeza hapo kabla. Kwa hakika tunaweza kusema kuwa hitilafu na tofauti kati ya nchi za Kiislamu zilishtadi na kupamba moto katika kipindi hicho na katika baadhi ya matukio kupelekea kuzuka mizozo na mapigano kati ya nchi hizo. Mbali na mizozo ya kisiasa na kijeshi, kulijitokeza pia namna fulani ya makabiliano ya kifikra na kiitikadi baina ya mirengo ya ndani ya Ulimwengu wa Kiislamu, ambapo Jumuiya ya OIC sio tu haikufanikiwa kuyazima lakini wakati mwengine, yenyewe ilisababisha pia kushadidi kwa mizozo hiyo.

 

Uvamizi wa kijeshi uliofanywa na Iraq mwaka 1980 dhidi ya Iran ulikuwa moja ya vielelezo na mifano hai ya hali hiyo. Uvamizi huo uliopelekea kutokea vita vya miaka minane vya umwagaji mkubwa wa damu na uharibifu mkubwa kwa nchi zote mbili za Kiislamu uliifanya Jumuiya ya Nchi za Kiislamu, malengo na makusudio yake matukufu yakabiliwe na changamoto kali za namna kadhaa.

Kwanza kabisa ni kwamba kinyume na misingi iliyokubaliwa na nchi wanachama, hitilafu na mgogoro uliojitokeza kati ya nchi mbili juu ya umiliki wa Mto Arvand haukutafutiwa ufumbuzi wa njia za amani na kufikiwa suluhu; na badala yake Iraq ikachukua hatua ya kuishambulia kijeshi nchi nyingine mwanachama wa OIC; pili ni kuwa jumuiya hiyo haikuweza kuchukua hatua ya usuluhishi ili kuuhitimisha uhasama huo; na tatu ni kwamba, kutokana na kuathiriwa na ushawishi wa baadhi ya nchi zenye satua, jumuiya ya OIC ilichukua misimamo ambayo ilisababisha kushadidi mgogoro uliokuwepo na kuvifanya vita viendelee kwa muda mrefu zaidi. Katika mkutano wa tatu wa viongozi wa nchi wanachama wa OIC uliofanyika mjini Jeddah, Saudi Arabia, vita vya Iran na Iraq ilikuwa moja ya ajenda za mkutano huo ambapo jumuiya hiyo ilipitisha azimio la kutaka kuhitimishwa vita hivyo, ilhali Iraq ilikuwa tayari imeshakiuka misingi ya wazi kabisa ya OIC. Lakini mbali na azimio hilo kutilia mkazo kusimamishwa vita pasi na kuyataka majeshi vamizi ya Iraq yaondoke katika ardhi ya Iran, kwa njia isiyo ya moja kwa moja lilionyesha uungaji mkono pia kwa Iraq. Jumuiya ya Nchi za Kiislamu iliendelea na msimamo wake huo hadi pale Iran ilipokubali azimio nambari 598 la Umoja wa Mataifa. Na kwa sababu hiyo, sio tu mzozo na vita vya umwagaji damu kati ya nchi mbili havikumalizika lakini vilishtadi na kupamba moto pia.

***********

Mbali na suala hilo, lakini pia wakati kadhia ya Palestina ilikuwa moja ya misingi mikuu ya kuleta umoja na mshikamano katika Ulimwengu wa Kiislamu na fursa mwafaka ya kupatikana umoja wa hali zote baina ya nchi za Kiislamu, katika kipindi hicho umuhimu wa kadhia hiyo ulififia mno kiasi kwamba katika mkutano wa nne wa viongozi wa nchi za Kiislamu uliofanyika mjini Dakar, Senegal Misri iliweza kurudi na kukabidhiwa tena kiti chake cha uwanachama wa OIC. Aidha katika kikao hicho mpango wa amani ya Mashariki ya Kati wa “FEZ” uliwasilishwa na kutiliwa mkazo utekelezaji wake. Kwa mujibu wa mpango huo mkutano wa viongozi wa OIC ulitakiwa kuukubali mpango wa Waarabu wa utatuzi wa kadhia ya Palestina na Mashariki ya Kati ambao ulipitishwa hapo kabla katika kikao cha kumi na mbili cha viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kilichofanyika katika mji wa Fez, nchini Morocco.

Mpango huo ulipendekezwa na Mfalme Fahd wa Saudi Arabia na ukaitambua rasmi haki ya uwepo wa nchi zote za eneo la Mashariki ya Kati katika maeneo ya mipaka yao. Kwa maneno mengine ni kusema kwamba kwa namna isiyo ya moja kwa moja, mpango huo ulitilia mkazo na kukubali kuwa Israel ni nchi huru yenye haki ya kuwepo kama nchi nyinginezo za eneo hili.

 

Kutohudhuria Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kikao hicho ambako kulifanywa ili kulalamikia maamuzi yaliyopitishwa na OIC kuhusiana na vita vya Iran na Iraq, kulidhihirisha ukweli kwamba umoja ulioadhamiriwa, na malengo na misingi iliyokusudiwa kufikiwa na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu inakabiliwa na changamoto kali; na kuna mgongano mkubwa ndani ya Ulimwengu wa Kiislamu hususan baina ya nchi muhimu na zenye nafasi na mchango athirifu katika ulimwengu huo. Maudhui ya kufanya suluhu na Israel kupitia mpango wa amani wa Fez na vilevile kushadidi mashinikizo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mkutano uliofuatia uliofanyika nchini Kuwait kulizidi kuhafifisha na kudhoofisha madhihirisho ya kuleta umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Jambo jengine lililosababisha mfarakno katika Ulimwengu wa Kiislamu na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC katika kipindi hicho ilikuwa ni hatua ya Iraq ya kuivamia kijeshi Kuwait. Uvamizi huo ambao ulifanywa baada ya kumalizika vita kati ya Iran na Iraq ulidhihirisha dhulma iliyokuwa imetendewa Iran na ukaonyesha kuwa OIC haikufanya insafu katika kutatua kadhia hiyo. Katika kipindi hicho, na kwa sababu ya hofu ziliyokuwa nayo nchi za Kiarabu wanachama wa OIC juu ya sera ya Iraq ya kujipanua kieneo, katika mkutano wake wa sita uliofanyika mjini Dakar, Senegal, Jumuiya ya Nchi za Kiislamu ilitoa tamko la kulaani uvamizi wa kijeshi wa Iraq dhidi ya ardhi ya Kuwait.

Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, katika kipindi hicho cha umri wa OIC ukweli uliojificha katika uhusiano wa nchi za Kiislamu ulidhihirika na kuufanya utambulisho wa jumuiya hiyo ukabiliwe na changamoto mpya. Hitilafu hizo zilifikia kiwango cha kuifanya OIC iwe mbali na malengo yake na kuleta hali ya mfarakano baina ya nchi wanachama.  Wapenzi wasikilizaji muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki umemalizika. Nakuageni basi huku nikikutakieni kila la heri maishani.

Tags