Jumatano tarehe 13 Juni, 2018
Leo ni Jumatano tarehe 28 Ramadhani 1439 Hijria sawa na Juni 13, 2018.
Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, inayosadifiana na 23 Khordad 1359 Hijria Shamsia, Imam Ruhullah Khomeini mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akiwa na lengo la kufanya mabadiliko katika vyuo vikuu hapa nchini, alitoa amri ya kuasisiwa Baraza la Mapinduzi ya Kiutamaduni. Katika ujumbe wake, Imam Khomeini MA aliwataka wajumbe wa baraza hilo kuratibu na kuandaa mipango na mitalaa katika kozi mbalimbali za vyuo vikuu inayokwenda sambamba na mafunzo ya utamaduni tajiri wa Kiislamu.
Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 23 Khordad 1362 Hijria Shamsia, Bi. Nusrat Amin, faqihi na mfasiri mkubwa wa Qurani Tukufu alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 97 katika mji wa Esfahan ulioko katikati mwa Iran. Bi. Nusrat Amin aliutumia muda wake wote katika kuishughulikia Qurani Tukufu, na hata kufanikiwa kufasiri juzuu 15 za Qurani na kuandika vitabu kadhaa kama vile 'Njia ya Kufikia Saada' na 'Nafahat Ar-Rahmania'.
Katika siku kama ya leo miaka 97 iliyopita, inayosadifiana na 13 Juni 1921 katika miaka ya mwanzo ya usimamizi wa Uingereza huko Palestina, kulianzishwa harakati kubwa katika ardhi yote ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na maghasibu wa Kizayuni. Harakati hiyo ilikuwa dhidi ya Wazayuni. Harakati ya wananchi hao ilibainisha upinzani wao dhidi ya siasa za kikoloni za Uingereza pamoja na uungaji mkono wa nchi hiyo kwa Wazayuni waliokuwa wameiteka ardhi ya Palestina. Siasa za kikoloni za Uingereza zilijumuisha kuwashajiisha Wazayuni kutoka sehemu zote duniani waelekee Palestina ili kwa mujibu wa Azimio la Balfour, serikali ya Kizayuni iundwe ndani ya ardhi ya Palestina. Sera hiyo ya kikoloni ilitekelezwa mwaka 1948 wakati dola bandia la Israel lilipoundwa.
Na siku kama ya leo miaka 1167 iliyopita aliaga dunia Abu Ma'ashar Balkhi mmoja wa wanajimu na wasomi wakubwa wa elimu ya hadithi wa Kiirani. Alielekea Baghdad mwanzoni mwa karne ya tatu Hijria na kuanza kusoma elimu ya nujumu. Katika zama zake Abu Ma'ashar Balkhi alikuwa mnajimu mashuhuri kabisa wa Kiislamu. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni al-Madkhal al-Kabir na al-Mawalid as-Saghirah.
