Alkhamisi, 12 Julai, 2018
Leo ni Alkhamisi tarehe 28 Mfunguo Mosi Shawwal 1439 Hijria inayosadifiana na tarehe 12 Julai 2018.
Siku kama ya leo miaka 12 iliyopita Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mara nyingine tena lilifanya mashambulizi ya anga na bahari huko Lebanon. Utawala wa Kizayuni ulifanya mashambulizi hayo kwa kisingizio cha kukamatwa mateka wanajeshi wake wawili na wapiganaji wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon kupitia oparesheni yake ya kujilinda. Tel Aviv ilifanya mashambulizi hayo ya kijeshi huko Lebanon ikiungwa mkono na Washington lengo lake kuu likiwa ni kuvunja uwezo wa kijeshi wa Hizbullah na kuipokonya silaha harakati hiyo inayohesabiwa kuwa nguvu kuu ya mapambano huko Lebanon mbele ya jeshi ghasibu la utawala wa Kizayuni.
Tarehe 12 Julai 1946, Hoteli ya King David iliyoko katika mji wa Baitul Muqaddas huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, ililipuliwa baada ya kutegwa bomu ndani ya hoteli hiyo na kundi moja la kigaidi la Wazayuni la Irgun. Zaidi ya Wapalestina 200 walipoteza maisha yao huku Mayahudi 15 wakiwa miongoni mwa wahanga wa tukio hilo.
Siku kama ya leo miaka 83 iliyopita, inayosadifiana na 21 Tir 1314 Hijria Shamsia, Waislamu wa mji wa Mash'had ulioko nchini Iran walianzisha harakati ya kusimama kidete kwenye Msikiti wa Gouhar Shad. Wananchi wakiongozwa na wanachuoni wa kidini walipambana dhidi ya utawala wa Mfalme Reza Khan Pahlavi, kutokana na hatua zake za kutaka kutokomeza utamaduni wa Kiislamu nchini Iran, na badala yake kuleta utamaduni wa Magharibi. Miongoni mwa hatua za Reza Khan ni kuondosha kwa nguvu vazi la Kiislamu la hijabu kwa wanawake wa Kiislamu, hatua ambayo ilikabiliwa na upinzani mkubwa wa wananchi, Watu kadhaa waliuawa na wengine kujeruhiwa kwenye machafuko hayo.
Siku kama ya leo miaka 201 iliyopita, alizaliwa Henry David Thoreau, msomi na mwanaharakati wa Kimarekani. David alikuwa akiheshimu mazingira asilia kama viumbe vya Mwenyezi Mungu huku akiwa mwenye akhlaqi njema. Henry David alikuwa akisisitiza kuwa, haifai kuangamiza maisha ya wanadamu kwa tamaa ya kufikia mali na fedha nyingi. Aidha mwanaharakati huyo, aliamini kuwa kama vile ambavyo serikali inavyomuadhibu mtu mkosefu, kadhalika inapotokea serikali hiyo ikashindwa kutekeleza wadhifa wake wa kiuongozi, basi wananchi nao wanatakiwa kuipa adabu serikali hiyo sanjari na kuiondoa madarakani. Miongoni mwa athari muhimu za Henry David Thoreau ni pamoja na kitabu cha 'Uasi wa Kiraia' na alifariki dunia mwaka 1862 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 785 iliyopita inayosadifiana na tarehe 12 Julai 1233 bandari ya kihistoria ya Alexandria nchini Misri ilizingirwa na meli za kivita za wapiganaji wa Msalaba. Katika zama hizo Salahuddin Ayubi shujaa wa vita vya msalaba alikuwa kamanda wa majeshi ya Alexandria, lakini hakuweko wakati wa mashambulio dhidi ya bandari hiyo. Hata hivyo wapiganaji wa Kiislamu walisimama kidete na kukabiliana na mashambulio ya maadui hao hadi alipowasili Salahuddin Ayubi. Hata hivyo wapiganaji wa Kiislamu waliyashinda vibaya majeshi vamizi ya Uholanzi, ambao yalikuwa mstari wa mbele na kuyalazimisha kurudi nyuma.
Siku kama ya leo miaka 1307 iliyopita, kwa mara ya kwanza katika historia ya mapambano ya Waislamu, akiwa na jeshi kubwa la Kiislamu Twariq bin Ziyad aliweza kuingia Uhispania. Ushindi huo ulikuwa mwanzo wa maendeleo ya Waislamu barani Ulaya ambapo umeendelea hadi leo kufikia Ufaransa. Twariq bin Ziyad aliwasili Uhispania baada ya kuvuka lango bahari kati ya Morocco na Uhispania linalojulikana kwa jina lake mwenyewe yaani "Jabal Tariq." Mlango bahari huo unatumika kama njia ya mawasiliano kati ya Bahari za Atlantic na Mediterranean. Waislamu walitawala kwa karne nane huko Uhispania na kueneza mafunzo na utamaduni wa Kiislamu barani Ulaya baada ya kutekwa Andalusia, moja ya sehemu za Uhispania ya leo.