Alkhamisi tarehe 19 Julai 2018
Leo ni Alkhamisi tarehe 05 Dhulqaada 1439 Hijria sawa na Julai 19, 2018.
Miaka 64 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia msomi mashuhuri wa Kiislamu Muhammad Hussein Kashiful Ghitaa. Ayatullah Kashiful Ghitaa alizaliwa katika mji mtakatifu wa Najaf katika familia ya wasomi na wachamungu na kuanza kutafuta elimu akiwa bado mtoto mdogo. Baada ya kukamilisha elimu ya msingi na ya kati, Ayatullah Kashiful Ghitaa alihudhuria darsa za maulamaa wakubwa wa zama hizo na kukwea daraja za juu za elimu katika kipindi kifupi. Alifanikiwa kulea wasomi na maulamaa wakubwa na kufanya safari katika nchi nyingi za Kiislamu kwa ajili ya kueneza elimu na maarifa. Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu pia alikutambua kushiriki katika masuala ya kisiasa na kutilia maanani masuala ya serikali na utawala kuwa ni katika mambo ya wajibu na alikuwa na mchango mkubwa katika kuanzisha Harakati ya Kitaifa ya Iraq. Ayatullah Kashiful Ghitaa alishiriki vilivyo katika mapigano ya jihadi ya wananchi wa Iraq wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia dhidi ya jeshi vamizi la Uingereza. Mwanazuoni huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi katika nyanja mbalimbali.
Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, Kuwait iliondokana na ukoloni wa Uingereza. Katika kipindi cha utawala wa Achaemenid, Kuwait ilikuwa ikihesabiwa kuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Mwaka 1899 Miladia, Kuwait iliwekeana saini na Uingereza, suala lililoifungulia London mlango wa kuikoloni nchi hiyo. Mwenendo huo uliendelea hadi baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Kuwepo kwa visima vya mafuta kulipanua uingiliaji mkubwa wa mashirika mengi ya Uingereza na Marekani katika taifa hilo. Hatimaye mwaka 1961 Kuwait na Uingereza zilitiliana saini makubaliano yaliyoifanya nchi hiyo kujipatia uhuru wake.
Miaka 39 iliyopita katika siku kama ya leo mapinduzi ya wananchi wa Nicaragua yalipata ushindi dhidi ya dikteta Anastasio Somoza wa nchi hiyo na muitifaki wake mkubwa yaani Marekani. Dikteta huyo kibaraka wa Marekani alichukua hatamu za uongozi wa Nicaragua mwaka 1967 na tangu wakati huo wimbi kubwa la upinzani lilianza kuenea nchini kote na katika America ya Kati dhidi ya kiongozi huyo. Mapambano ya silaha ya wapiganaji wa msituni ya Harakati ya Ukombozi wa Kitaifa ya Sandinista (FSLN) yaliyoanza mwaka 1963 yalipamba moto zaidi katikati ya muongo wa 1970 na kuungwa mkono na wananchi. Hatimaye Somoza alilazimika kukimbia nchi baada ya jeshi la Sandinista kuingia Managua mji mkuu wa Nicaragua katika siku kama ya leo. Karibu watu elfu 40 waliuawa katika mapinduzi ya Nicaragua.
Miaka 125 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa malenga wa Russia kwa jina la Vladimir Mayakovsky. Mashairi ya Mayakovsky yalikuwa na nafasi kuu wakati wa mapinduzi ya Kikomonisti ya Urusi ya zamani mwaka 1917. Vladimir Mayakovsky alikuwa akiamini kuwa fasihi inapasa kuwa lugha ya watu wengi na inayobainisha maisha yao ya kijamii.
Na miaka 775 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo alifariki dunia mtaalamu wa fiqhi, hadithi, historia na mwanafasihi wa Kiislamu Radhiyyud-Din Ali bin Musa, maarufu kwa jina la Sayyid Ibn Tawus. Ibn Tawus alipitia kipindi cha utoto na ujana wake mjini Hillah, Iraq sambamba na kusoma elimu tofauti za dini. Aidha Sayyid Ibn Tawus alifahamika kwa zuhudi na uchaji Mungu na kwa sababu hiyo alikataa vyeo vyote alivyopewa na watawala wa wakati huo.