Jul 21, 2018 01:17 UTC
  • Jumamosi, 21 Julai, 2018

Leo ni Jumamosi tarehe 7 Mfunguo Pili Dhul-Qaad 1439 Hijria mwafaka na tarehe 21 Julai 2018.

Leo ni Jumamosi tarehe 7 Mfunguo Pili Dhul-Qaad 1439 Hijria mwafaka na tarehe 21 Julai 2018.

Miaka 723 iliyopita katika siku kama ya leo alifariki dunia Ibn Baswis mtaalamu wa kaligrafia aliyeliwa maarufu kwa jina la Damashqi. Alizaliwa mwaka 651 Hijiria katika mji wa Damascus na kwa muda wa miaka 50 alijishughulisha kufundisha hati na wakaazi wa mji huo walistafidi kwa elimu na sanaa kutoka kwake. Ibn Baswis aliandika hati kwa mitindo tofauti ya kupendeza na katika umri wake wa uzeeni aliandika nakala ya Qur'ani Tukufu kwa kutumia maji ya dhahabu na kwa hati nzuri na za kuvutia. Qur'ani hiyo pamoja na athari nyingine za Ibn Basis bado ziko hadi leo. ***

Ibn Baswis

Miaka 130 iliyopita katika siku kama ya leo, John Boyd Dunlop raia wa Uingereza, alikuwa mvumbuzi wa kwanza wa gurudumu (Pneumatic Tyre). Dunlop alifikia hatua ya kuvumbua gurudumu la magari baada ya kupita miaka kadhaa ya utafiti. Alifariki dunia 1921. ***

John Boyd Dunlop

Tarehe 21 Julai miaka 119 iliyopita alizaliwa mwandishi mtajika wa Kimarekani kwa jina la Ernest Hemingway. Kwa muda fulani Hemingway alikuwa mwandishi huko Uingereza na Ufaransa. Ernest Hemingway alianzisha mbinu ya kuandika riwaya na tungo fupi fupi na alikuwa akitumia lugha nyepesi na inayoeleweka kwa wepesi. Mwaka 1954 mwandishi Ernest Hemingway alitunukukiwa tuzo ya Nobel katika medani ya fasihi. Miongoni mwa vitabu maarufu vya Hemingway ni "The Old Man and The Sea", "A Farewell to Arms" na "For Whom The Bell Tolls". ***

Ernest Hemingway

Miaka 66 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria Shamsiya, kulifanyika maandamano makubwa mjini Tehran na kwenye miji mingine ya Iran baada ya Dakta Musaddiq kujiuzulu cheo cha Waziri Mkuu. Wakati huo Ayatullah Kashani alitoa taarifa ya maneno makali baada ya Dakta Musaddiq aliyekuwa Waziri Mkuu kujizulu na Shah kumteuwa Ahmad Qavam mashuhuri kwa jina la Ghavam Sultaneh kuwa Waziri Mkuu. Ayatullah Kashani alitoa taarifa hiyo akilalamikia vikali agizo la Shah la kumteuwa Ghavam kushika wadhifa huo. Ahmad Qavam ambaye alikuwa na uhusiano na wakoloni na kibaraka wa utawala wa kibeberu wa wakati huo, muda mfupi baada ya kuwa Waziri Mkuu, alianzisha njama za kutenganisha dini na siasa na kuendesha propaganda dhidi ya Ayatullah Kashani na wanaharakati wa Kiislamu nchini Iran. ***

Dakta Musaddiq

Siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 21 Julai 1954 ulitiwa saini mwishoni mwa mkutano wa Geneva mkataba wa kuacha vita kati ya Ufaransa na Vietnam na kukomesha ukoloni wa Ufaransa huko India na China. Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya kuanguka ngome imara ya Wafaransa iliyojulikana kwa jina la Dien Bien Phu nchini Vietnam Mei mwaka 1954. Makubaliano ya mkutano wa kimataifa wa Geneva, yalihudhuriwa na wawakilishi wa ngazi za juu kutoka Ufaransa, Marekani, Uingereza, China, Vietnam na Urusi ya zamani. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, vikosi vya kigeni vilipaswa kuondoka Vietnam, lakini Marekani kinyume na makubaliano ya Geneva, iliamua kutuma majeshi katika eneo hilo kwa lengo la kuzuia kuungana maeneo mawili ya Vietnam ya kaskazini na kusini. ***

Vita vya Dien Bien Phu 

Na katika siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, meli ya kwanza ya biashara ya nyuklia iliyopewa jina la NS Savannah iliwekwa majini huko Marekani. Baada ya kugunduliwa atomu na wasomi kutambua nguvu kubwa na nishati ya atomiki ilijitokeza fikra ya kutumia nishati hiyo katika masuala mbalimabali. Hata hivyo inasikitisha kwamba, nishati hiyo ilitumiwa kwa mara ya kwanza kielimu katika kutengeneza mabomu ya nyuklia. Suala hilo lilichochea mashindano ya kutengeneza silaha na mabomu ya nyuklia kati ya madola makubwa duniani na kuiweka dunia katika ncha ya vita vya nyuklia. Meli ya NS Savannah ilikuwa matokeo ya jitihada za wasomi za kutumia nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani na katika siku kama hii ya leo yaani tarehe 21 Julai mwaka 1958 meli hiyo ya kibiashara iliyokuwa ikitumia nishati hiyo iliwekwa majini na kuanza kufanya kazi. NS Savannah ilikuwa meli ya kwanza iliyotumia nishati ya nyuklia kuvuka habari ya Atlantic. ***