Ijumaa tarehe 3 Agosti 2018
Leo ni Ijumaa tarehe 20 Dhulqaada 1439 Hijria sawa na Agosti 3, 2018.
Miaka 40 iliyopita katika siku kama ya leo, katika hatua yake nyingine ya kigaidi utawala wa Kizayuni wa Israel uliwauwa Izzuddin Qalq mjumbe wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) na naibu wake huko Paris, Ufaransa. Shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel MOSSAD katika miongo miwili ya 70 na 80 liliwauwa kigaidi viongozi wengi wa PLO ili kuidhoofisha harakati hiyo na kuilazimisha kuanzisha mazungumzo eti ya mapatano kati ya Wapalestina na Israel.
Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita, nchi ya Niger iliyoko magharibi mwa Afrika ilijipatia uhuru kutoka kwa Ufaransa. Kuanzia karne ya 18 Niger ilianza kuwa chini ya Ufaransa, na ulipofika mwaka 1922 Paris ilianzisha kambi za kijeshi nchini humo. Niger inapakana na Libya, Chad, Mali na Benin.
Katika siku kama ya leo miaka 104 iliyopita, meli ya kwanza ilipita katika Kanali ya Panama na kwa utaratibu huo, kanali hiyo ikawa imefunguliwa. Wahandisi wa Kifaransa ndio walioanza kujenga mfereji huo wa Panama na baadaye Wamarekani walikamilisha kazi hiyo. Kujengwa mfereji huo wenye kilomita 68, kuliunganisha bahari mbili za Pacifi na Atlantic.
Siku kama ya leo miaka 526 iliyopita, ilianza safari kubwa zaidi ya uvumbuzi ya baharia wa Kiitalia Christopher Columbus. Christopher Columbus alipewa jukumu la kuvumbua njia mpya ya kuelekea India katika makubaliano yaliyofikiwa kati yake na mfalme na malkia wa Uhispania wa wakati huo. Kwa sababu hiyo Christopher Columbus aliondoka katika bandari ya Paulus huko Uhispania akiwa na meli tatu na mabaharia 120 na hatimaye walifika katika nchi kavu baada ya kuwa baharini kwa siku 33. Wakati huo Columbus na wenzake walidhani kuwa wamewasili India lakini walikuwa wamevumbua bara America bila ya wao kujua.
Na miaka 983 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 20 Dhulqaada mwaka 456 alifariki dunia Abu Ali Qirawani, mshairi, mwanafasihi na mkosoaji wa fasihi wa Morocco. Abu Ali alijifunza mashairi, fasihi na elimu nyingi za kipindi hicho akiwa bado mdogo na baada ya hapo alielekea katika mji wa Qirawan nchini Tunisia kwa shabaha ya kushiriki katika vikao na majlisi za wasomi wakubwa. Kipindi hicho mji wa Qirawan ulikuwa kituo kikuu cha ustaarabu wa Kiislamu huko kaskazini mwa Afrika na Andalusia na wasomi wa Kiislamu na wanazuoni wengi mashuhuri walikuwa wakiishi katika mji huo. Mashairi mengi ya malenga huyo yanaakisi vipindi mbalimbali vya naisha yake ya kijamii. Mshairi huyo aligundua mbinu mpya ya kukosoa kazi za fasihi na kuacha athari nyingi katika uwanja huo.