Aug 06, 2018 01:19 UTC
  • Jumatatu tarehe 06 Agosti 2018

Leo ni Jumatatu tarehe 23 Dhulqaada 1439 Hijria sawa na Agosti 06, 2018.

Miaka 73 iliyopita katika siku kama ya leo, kwa mara ya kwanza kabisa duniani Marekani iliushambulia vikali kwa mabomu ya nyuklia na kuusambaratisha mji wa Hiroshima huko Japan mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia. Mabomu hayo yalikuwa na nguvu kubwa ya uharibifu iliyokuwa sawa na tani elfu 20 ya mada za milipuko za TNT. Katika mashambulizi hayo watu zaidi ya elfu 90 waliuawa na wengine 75 elfu kujeruhiwa. Athari mbaya za mabomu hayo ya nyuklia zingali zinashuhudiwa hadi hii leo huko Hiroshima licha ya kupita miaka mingi sasa tangu kufanyike mashambulizi hayo ya nyuklia ya Marekani. Muda mfupi baada ya kuushambulia mji wa Hiroshima, Marekani iliushambulia pia kwa mabomu ya nyuklia mji wa Nagasaki huko huko Japan na kuilazimisha nchi hiyo kusalimu amri. Maafa hayo ya kutisha na kusikitisha yaliyofanywa na Marekani katika miji miwili ya Japan ambayo yanahesabiwa kuwa jinai kubwa zaidi ya kivita katika historia, yanaonyesha kuwa silaha za nyuklia ni wenzo hatari sana katika mikono ya nchi zinazopenda kujitanua duniani kama Marekani na ndiyo maana kuna udharura wa kusimamiwa na kudhibitiwa silaha hizo na taasisi husika, na hatimaye kutokomezwa kabisa kwa ajili ya usalama wa dunia.

Hiroshima baada ya mashambulizi ya Marekani

Siku kama ya leo miaka 137 iliyopita, alizaliwa Alexander Fleming tabibu, mwanabiolojia na mtaalamu wa madawa wa Scotland. Wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, tabibu huyo pamoja na wasomi wenzake wawili Chain na Florey, waligundua dawa ya antibiotic ya Penicillin. Mwaka 1945, wasomi hao watatu kwa pamoja walitunukiwa tuzo ya Nobel katika elimu ya tiba kutokana na ugunduzi wao huo muhimu. Penicillin inatumika sana hivi sasa katika elimu ya tiba.

Alexander Fleming

Tarehe 15 Mordad miaka 30 iliyopita dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein alilazimika kukubali usitishaji vita na Iran. Baada ya Iran kukubali azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo tarehe 27 Tir mwaka 1367 Hijria Shamsia ambalo lilijumuisha usitishaji vita baina ya pande mbili, ilitarajiwa kuwa mapigano ya kijeshi baina ya nchi hizo mbili pia yangekomeshwa. Hata hivyo siku kadhaa baadaye Saddam Hussein alifanya mashambulizi makubwa dhidi ya ardhi ya Iran ambayo yalifeli kutokana na ushujaa wa wapiganaji wa Kiirani. Hatimaye Saddam Hussein ambaye aliilazimisha Iran kuingia katika vita vya miaka 8 vilivyosababisha hasara kubwa ya hali na mali na hakuweza kufikia malengo yake, alikubali kusitisha mapigano katika siku kama hii ya leo na kutekeleza makubaliano hayo wiki mbili baadaye.

Azimio nambari 598

Na miaka 23 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani Agosti 6, 1995, Profesa Kighoma Ali Malima aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama cha upinzani cha NRA katika uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi nchini Tanzania aliaga dunia. Malima alizaliwa mwaka 1938 katika wilaya ya Kisarawe mkoa wa Pwani. Akiwa kijana mdogo mwenye umri wa miaka 19 na mwanafunzi hodari alikatisha masomo yake ya sekondari ili ajiunge na TANU katika harakati za kuikomboa Tanganyika kutoka katika utumwa wa Waingereza. Hayati Profesa Malima, atakumbukwa na wapenda haki wengi nchini Tanzania kutokana na kupinga kwake dhulma. Profesa Kigoma Ali Malima aliaga dunia ghafla kwa njia ya kutatanisha huko mjini London Uingereza alikopitia kutoka Makka alikokwenda kufanya Umra, zikiwa zimepita siku chache tu tangu alipotangaza uamuzi wake wa kukihama chama tawala cha CCM kufuatia kujiuzulu wadhifa wa uwaziri katika serikali ya chama hicho. Suala hilo lilimfanya akasirikiwe sana na chama hicho cha CCM.

Kighoma Malima