Alkhamisi, 30 Agosti, 2018
Leo ni Alkhamisi tarehe 18 Dhulhija 1439 Hijria sawa na Agosti 30, mwaka 2018.
Siku kama hii ya leo miaka 1429 iliyopita Mtume Muhammad (SAW) akiwa njiani kurejea Madina baada ya kukamilisha Hija yake ya mwisho, kwa amri ya Mwenyezi Mungu alimtangaza Imam Ali bin Abi Twalib AS kuwa kiongozi wa Waislamu wote baada yake. Hatua hiyo ya Mtume Mtukufu ilifanyika katika eneo linalojulikana kwa jina la Ghadir Khum katika makutano ya njia ya Makka na Madina. Siku hiyo Mtume SAW alitoa hotuba mbele ya hadhara kubwa ya Waislamu kisha akashika mkono wa Ali bin Abi Twalib na kusema: "Kila mtu ambaye mimi ni kiongozi wake basi huyu Ali pia ni kiongozi wake. Mwenyezi Mungu ampende atakayempenda, na amfanyie uadui atakayemfanyia uadui." Mtume SAW pia aliwausia Waislamu kushikamana na Qur'ani na Ahlubaiti wake na akasema viwili hivyo havitatengana hadi vitakapomkuta yeye katika hodhi ya Kauthar, Siku ya Kiyama.

Siku kama ya leo miaka 767 iliyopita, alifariki dunia Nasiruddin Tusi, mwanafalsafa, mtaalamu wa hesabati na nujumu na msomi mkubwa wa Kiislamu huko katika mji wa Tus, kaskazini mashariki mwa Iran. Nasiruddin Tusi aliishi katika kipindi cha Hulagu Khan Mongol na aliasisi kituo kikubwa na cha kwanza cha sayansi ya nujumu huko Maraghe kaskazini magharibi mwa Iran. Nasiruddin Tusi ameandika vitabu zaidi ya 80 kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi. Vitabu muhimu zaidi vya msomi huyo ni pamoja na ‘Asasul-Iqtibaas’, ‘Akhlaaq Naaswiri’, ‘Awsaful-Ashraaf’ na ‘Sharhul Ishaarat.
Siku kama ya leo miaka 147 iliyopita, alizaliwa Ernest Rutherford, mtaalamu mkubwa wa fizikia wa nchini Uingereza maarufu kwa jina la baba wa nishati ya nyuklia. Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali eneo alikozaliwa, Ernest alielekea katika mji wa kielimu wa Cambridge na kujiunga na chuo kikuu cha mji huo. Kuanzia mwaka 1919 Rutherford alitokea kuwa mhadhiri mwenye tajriba katika uga wa fizikia chuoni hapo, huku akijiunga na jumuiya ya kifalme ya mjini London hapo mwaka 1903. Mwaka 1904, msomi huyo alisambaza kitabu chake alichokipa jina la ‘Shughuli za Mionzi’. Baadaye Ernest Rutherford aliongoza kundi la utafiti katika chuo kikuu cha Manchester, kundi ambalo haraka liliweza kuandaa nadharia mpya kuhusiana na muundo wa atomiki. Mwaka 1908 Miladia, msomi huyo alitunukiwa zawadi ya Nobel kutokana na shughuli zake hizo na kupata umaarufu mkubwa katika uga huo.
Siku kama ya leo katika kalenda ya Kiirani imepewa jina la Siku ya kupambana na ugaidi. Sababu ya kuitwa jina hilo ni mauaji ya kigaidi dhidi ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu Muhammad Ali Rajai na Waziri wake Mkuu Muhammad Javad Bahonar. Viongozi hao wawili waliuawa shahidi baada ya kutokea mlipuko mkubwa wa bomu katika ofisi ya Waziri Mkuu. Jinai hiyo ya kinyama ilitekelezwa na Kundi la Kigaidi la Munafiqeen (MKO). Rajai alianza kazi ya ualimu sambamba na kushiriki katika harakati za mapambano dhidi ya utawala dhalimu wa Shah na kuendelea katika njia hiyo hadi ulipopatikana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, shahidi Rajai alihudumia nyadhifa za mbunge, Waziri wa Elimu na Malezi, Waziri Mkuu na hatimaye Rais. Wakati wa kipindi cha urais wake, Rajai alimteua Dakta Muhammad Javad Bahonar kushika wadhifa wa Waziri Mkuu. Kutokana na juhudi, bidii na ikhlasi waliyokuwa nayo katika kulihudumia taifa la Iran ili kupeleka mbele malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu, maadui wa mfumo wa Kiislamu hawakufurahishwa na utendaji kazi wao na ndio maana katika tarehe kama ya leo, wakatega bomu katika ofisi ya Waziri Mkuu na kuwauwa shahidi.
Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, Jamhuri ya Azerbaijan ilitangaza uhuru wake kutoka Urusi ya zamani. Ardhi ya Azerbaijan ilitekwa na kukaliwa kwa mabavu na silsila ya Kiirani ya Wasasani tangu mwanzoni mwa karne ya Tatu Miladia na katika kipindi kikubwa cha historia yake ilikuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Vita kati ya Urusi ya zamani na Iran vilijiri mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia, kufuatia kupenda kujitanua kwa utawala wa kifalme wa Tsar huko katika Umoja wa Kisovieti. Iran ilipata pigo katika vita hivyo na kupelekea sehemu moja ya ardhi ya kaskazini ya Azerbaijan kukaliwa kwa mabavu na Urusi ya zamani mwaka 1813 kwa mujibu wa mkataba wa Golestan.
Na siku kama ya leo miaka 19 iliyopita, wananchi wa Timor ya Mashariki huko kusini mashariki mwa bara Asia walishiriki katika kura ya maoni na kuchagua kujitenga nchi hiyo na Indonesia. Kisiwa cha Timor ya Mashariki sambamba na visiwa vingine vya Indonesia kilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na wakoloni wa Kireno mwaka 1511 Miladia. Timor Mashariki iliunganishwa na Indonesia mwaka 1976.