Sep 14, 2018 02:25 UTC
  • Ijumaa, Septemba 14, 2018

Leo ni Ijumaa tarehe 4 Mfunguo Nne Muharram 1440 Hijria sawa na Septemba 14, mwaka 2018 Milaadia.

Siku kama ya leo, miaka 1379 iliyopita, Ubaidullah bin Ziyad, mtawala dhalimu na fasiki wa mji wa Kufa, Iraq alitoa hotuba katika msikiti wa mji huo. Katika hotuba hiyo, Ibn Ziyad alitoa vitisho vikali dhidi ya wafuasi wa Imam Hussein (as), mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad (swa) akiwataka kutomsaidia mtukufu huyo katika ardhi ya Karbala na kwamba angemuua mtu yeyote ambaye angefanya hivyo. Kwa kutumia fatwa ya hila iliyotolewa na Shuraihul-Qadhi ya kuhalalisha damu ya Imam Hussein (as), Ibn Ziyad akafunga njia zote za kuingia na kutoka mji wa Kufa huku akitoa fedha kwa wakazi wa mji huo kwa ajili ya kwenda kupambana na mjukuu huyo wa Mtume huko Karbala tukio lililomalizika kwa kuuawa Imam Hussein na watu wa familia ya Mtume (swa).

Siku kama ya leo miaka 955 iliyopita, alifariki dunia Abul-Qasim Muhammad Baghdadi, maarufu kwa jina la Ibn Naqiya, malenga, mwandishi na fasihi mkubwa wa mjini Baghdad, Iraq. Umahiri aliokuwa nao Ibn Naqiya, ndio uliofanya kuwa mashuhuri ambapo hata wataalamu wa mashairi waliyatumia mashairi yake. Kitabu cha ‘Maqaamaat’ ni moja ya athari zinazonasibishwa kwa malenga huyo. Katika kitabu hicho Ibn Naqiya, alizungumzia maovu ya kijamii kupitia hekaya na tenzi. Athari nyingine inayonasibishwa kwa msomi huyo wa Kiislamu, ni kitabu kinachoitwa ‘Al-Jamaan fi Tashbiihaatil-Qur’an’ ambayo ni tafsiri nyepesi ya Qur’an Tukufu. Katika tafsiri hiyo Ibn Naqiya amefafanua aya 226.

Tarehe 14 Septemba miaka 206 iliyopita, moja kati ya ajali kubwa za moto ulimwenguni na uliowashwa makusudi ilitokea katika mji mkuu wa Russia, Moscow. Tukio hilo lilitokea baada ya kupita siku moja tu, tangu mji huo uvamiwe na kukaliwa kwa mabavu na majeshi ya Napoleone Bonaparte, wakati mji huo ulipochomwa moto kwa amri ya mtawala wa wakati huo wa mji huo. Lengo la mtawala huyo lilikuwa ni kuyafanya majeshi ya Bonaparte yashindwe kustafidi na suhula za mji huo. Moto huo mkubwa uliteketeza na kuharibu kabisa robo tatu ya mji mzima wa Moscow.

Moto ulioteketeza mji wa Moscow.

Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita, hati ya Jumuiya ya Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC) ilitiwa saini na nchi za Iran, Saudia, Iraq, Kuwait na Venezuela. Jumuiya hiyo ilianzishwa kwa lengo la kukabiliana na makampuni makubwa ya mafuta ya Magharibi ambayo yalikuwa yakisimamia uvumbuzi, uchimbaji na uuzaji wa bidhaa hiyo kimataifa na kuainisha bei ya bidhaa hiyo muhimu kwa maslahi yao binafsi na kwa madhara ya nchi zalishaji. Licha ya kwamba awali jumuiya hiyo haikuwa na nguvu wala ushawishi wowote, lakini ilikuja kupata nguvu zaidi baada ya nchi kadhaa zikiwemo, Algeria, Libya, Nigeria, Qatar, Imarat, Gabon, Indonesia na Ecuador ambazo ni wazalisha wa mafuta kujiunga nayo.

OPEC

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita yani tarehe 23 Shahrivar mwaka 1357 Hijria Shamsia kulifanyika maandamano makubwa hapa nchini kuwaenzi mashahidi waliokuwa wameuawa na vibaraka wa Shah siku kadhaa kabla yake. Siku hiyo umati mkubwa wa watu ulimiminika katika makaburi ya Behest Zahraa mjini Tehran kuwaenzi mashahidi hao. Askari wa utawala wa Shah walikuwa na nia ya kuzuia maandamano hayo lakini umati mkubwa wa wananchi walioshiriki maandamano ulidumisha malalamiko yao dhidi ya utawala wa kidikteta wa Shah huko wakipiga nara za: “Iran ni nchi yetu na Khomeini na kiongozi wetu.”

Maandamano dhidi ya utawala wa Shah.

 

Tags