Ijumaa tarehe 21 Septemba 2018
Leo ni Ijumaa tarehe 11 Muharram 1440 Hijria sawa na Septemba 21, 2018.
Siku kama ya leo miaka 1379 iliyopita, yaani tarehe 11 Muharram mwaka 61 Hijiria, msafara wa mateka wa familia ya Bwana Mtume Muhammad (saw), baada ya tukio chungu la mauaji ya siku ya Ashura, ulianza safari ya kelekea Sham, yalikokuwa makao makuu ya utawala wa dhalimu wa Yazidi bin Muawiya. Baada ya majeshi ya Yazidi yaliyokuwa yakiongozwa na Omar bin Sa’ad kumuua shahidi Imam Hussein (as) na masahaba wake, majeshi hayo ambayo hayakuwa na chembe ya ubinadamu moyoni, yalianza kupora vitu vya thamani vya msafara wa watu wa familia ya Mtume (swa). Askari hao sanjari na kuchoma moto mahema ya Imam Hussein (as) na watu wake, waliwanyang’anya pia wanawake mapambo yao na kila walichokuwa nacho. Jioni ya siku kama ya leo msafara wa familia ya Imam Hussein uliokuwa ukiongozwa na Imam Sajjad (as) na Bibi Zainab (as), ulielekea Kufa na baadaye Sham.
Siku kama ya leo miaka 186 iliyopita, inayosadifiana na 21 Septemba 1832, aliaga dunia Sir Walter Scott, mwandishi wa riwaya, mshairi na mwanahistoria mahiri wa Uskochi. Alizaliwa 15 Agosti mwaka 1771 na baada ya kuhitimu masomo yake katika taaluma ya sheria, alifanya kazi ya uwakili kwa muda wa miaka 14. Hata hivyo, Sir Scott alikuwa na shauku na mapenzi makubwa na taaluma ya fasihi ya lugha.
Siku kama ya leo miaka 109 iliyopita, yaani 21 Septemba 1909, alizaliwa Dakta Osagyefo Kwame Nkrumah mwanasiasa na shujaa wa uhuru wa Ghana. Nkurumah alishiriki kikamilifu katika harakati za kupigania uhuru za wananchi wa Ghana dhidi ya mkoloni Muingereza. Baada ya kujipatia uhuru, kulijitokeza na kushuhudiwa njama kadhaa za kutaka kumuondoa madarakani na hata kumuua Nkrumah. Mwaka 1966 wakati Dakta Nkrumah akiwa safarini nchini China, Jenerali Joseph Ankrah alifanya mapinduzi na kuiondoa madarakani serikali Nkrumah. Mwanamapinduzi huyo aliaga dunia mwaka 1972 akiwa uhamishoni nchini Romania. Kwame Nkrumah alikuwa na nafasi muhimu katika kuasisiwa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM pamoja Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika OAU.
Na siku kama ya leo miaka 24 iliyopita Bunge la Taifa la Ufaransa lilipasisha sheria iliyopiga marufuku vazi la staha la mwanamke wa Kiislamu, hijabu katika shule za nchi hiyo. Ufaransa ilipasisha sheria hiyo inayowazuia wanafunzi wa kike Waislamu kwenda mashuleni wakiwa na vazi la hijabu licha ya kudai kuwa ni kitovu cha demokrasia na uhuru. Baadaye sheria hiyo ilipanuliwa zaidi na kupiga marufuku vazi la hijabu katika vyuo vikuu na idara za umma. Wachambuzi wengi walikosoa vikali sheria hiyo wakisema inapingana na Katiba ya Ufaransa na Tangazo la Kimataifa la Haki za Binadamu zinazosisitiza kuwa kila mtu ana uhuru wa kukubali na kutekeleza itikadi zake za kidini maadamu hazina madhara kwa watu wengine.