Sep 22, 2018 03:03 UTC
  • Jumamosi, Septemba 22, 2018

Leo ni Jumamosi tarehe 12 Mfunguo Nne Muharram 1440 Hijria inayosadifiana na tarehe 22 Septemba 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1379 iliyopita sawa na tarehe 12 Mfunguo Nne Muharram mwaka 61 Hijria, msafara wa mateka wa Karbalauliojumuisha wanawake na watoto wa mashahidi wa Karbala, uliwasili katika mji wa Kufa, nchini Iraq. Kiongozi wa msafara huo alikuwa Imam Ali bin Hussein Sajjad (as), mtoto wa Imam Hussein (as) na Bibi Zaynab (as) dada wa Imam Hussein bin Ali (as). Licha ya taabu na masaibu waliokutana nayo, wawili hao wakiwa mjini Kufa walifichua kwa ushujaa mkubwa dhulma na jinai za utawala wa wakati huo na kuwalaumu wakazi wa mji huo kumtelekeza Imam Hussein AS na kutomuunga mkono. ***

Msafara wa mateka wa Karbala

 

Katika siku kama ya leo miaka 1379 iliyopita sawa na tarehe 12 Mfunguo Nne Muharram mwaka 61 Hijria, miili ya mashahidi wa Karbala ukiwemo mwili mtukufu wa mjukuu wa Mtume (saw) Imam Hussein AS ilizikwa ikiwa ni siku mbili baada ya kuuawa shahidi na kuachwa jangwani. Mashahidi wa Karbala walizikwa na watu wa kabila la Bani Asad. Mwili wa Imam Hussein na mashahidi wote wa Karbala ilibakia kwa siku mbili bila ya kuzikwa kwani hakuna mtu aliyekuwa na ujasiri wa kuzika miili hiyo kutokana na hofu ya utawala dhalimu wa Bani Umayyah. Hatimaye katika siku kama hii ya leo wanawake wa kabila la Bani Asad waliwahamasisha wanaume wao kuzika miili hiyo mitakatifu ya wajukuu wa Mtume na masahaba wa Imam Hussein (as).***

Kaburi la mashahidi wa Karbala

 

Miaka 1345 iliyopita katika siku kama ya leo,  kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia ya kuaminika, Imam Ali Zainul Abidin maarufu kwa lakabu ya Sajjad mwana wa Imam Hussein (as) na mmoja wa wajukuu wa Mtume Mtukufu S.A.W, aliuawa shahidi. Imam Zainul Abidin alizaliwa mwaka 38 Hijria huko katika mji wa Madina. Mtukufu huyo aliishi katika zama ambapo watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu walikuwa wakikabiliwa na masaibu mengi. Imam Sajjad A.S ambaye alikuwa mgonjwa wakati wa tukio la Karbala, baada ya harakati adhimu ya Imam Hussein, alibeba jukumu kubwa la kueneza ujumbe wa mapambano hayo na kuendeleza njia ya baba yake. ***

Kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Zeonul Abidin AS
 

 

Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita, nchi ya Mali iliyo kaskazini magharibi mwa Afrika ilijipatia uhuru. Karibu miaka elfu mbili iliyopita nchi ya Mali ilikuwa na utamaduni mkubwa. Hata hivyo nchi hiyo tangu karne ya 18 hadi ya 19 Miladia ilikuwa moja ya tawala za ufalme wa Sudan. Baada ya Morocco kutwaa baadhi ya maeneo yaliyokuwa chini ya tawala za ufalme wa Sudan ikiwemo Mali, tawala mbalimbali za kikabila nchini Mali zilifanikiwa kuingia madarakani. Satwa ya Wafaransa nchini Mali ilianza mnamo karne ya 19 na hadi kufikia mwaka 1898 nchi hiyo ilikuwa chini ya usimamizi wa Ufaransa. Hata hivyo Mali ambayo ilikuwa ikiitwa Sudan ya Ufaransa, mwaka 1958 ilianza kujitawala na mwaka 1960 ikajipatia uhuru wake kamili. ***

Bendera ya Mali

 

Na siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, majeshi ya dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein yalianza mashambulio makubwa ya anga na nchi kavu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hivyo kuanzisha vita vya miaka minane dhidi ya Iran. Jeshi la Iraq lilikuwa limefanya uvamizi na mashambulizi kadhaa katika maeneo ya mpakani ya Iran miezi kadhaa nyuma. Magari ya deraya na vikosi 12 vya jeshi la nchi kavu la Iraq viliyashambulia maeneo ya mipaka ya kusini magharibi mwa Iran. Mapambano makali ya wananchi wa Iran yaliwalazimisha askari wa dikteta Saddam kurejea nyuma hadi kwenye mipaka inayotambulika kimataifa.***

Hujuma ya kijeshi ya Saddam Hussein dhidi ya Iran