Jumatatu, Oktoba 8, 2018
Leo ni Jumatatu tarehe 28 Mfunguo Nne Muharram 1440 Hijria sawa na Oktoba 8, mwaka 2018 Milaadia.
Miaka 784 iliyopita katika siku kama hii ya leo mji wa Baghdad uliokuwa makao makuu ya watawala wa Kiabbasi ulitekwa na Hulagu Khan Mongol baada ya kuuawa Mustaasim aliyekuwa mtawala wa mwisho wa utawala wa ukoo wa Abbas. Mauaji ya mtawala huo yalihitimisha utawala wa kizazi hicho uliotawala sehemu kubwa ya ulimwengu wa Kislamu kwa kipindi cha miaka 500. Hulagu Khan Mongol hakusita kufanya mauaji na jinai za aina mbalimbali katika uvamizi wake wa nchi mbalimbali, na baada ya kuteka baadhi ya maeneo ya Iran na kuua watu kwa umati katika maeneo ya mijini na vijijini, aliushambulia mji wa Baghdad na kufanya mauaji ya kinyama dhidi ya maelfu ya wakazi wake. Vilevile aliharibu na kuvunja nyumba na majengo muhimu ya mji wa Baghdad.
Miaka 90 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarehe 16 Mehr mwaka 1307 Hijiria Shamsia kufuatia upinzani wa Sayyid Hassan Mudarres dhidi ya udikteta wa Reza Khan Pahlawi, mtawala huyo aliwaamuru askari wake wavamia nyumba ya Ayatullah Muddares, kumpiga na kumjeruhi na kisha akahamishiwa nje ya mji wa Tehran. Askari hao pia waliwatia nguvuni watu wa familia ya mwanazuoni huyo. Mwishowe Ayatullah Mudarres alibaidishwa katika mji wa Kashmar kaskazini mashariki mwa Iran na kuuawa shahidi na askari wa Reza Khan mwaka 1316 Hijiria Shamsia.
Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita sawa na tarehe 8 Oktoba 1990 , kwa mara nyingine tena utawala haramu wa Israel ulifanya jinai ya kinyama kwa kuwashambulia waumini wa Kipalestina waliokuwa wakiswali ndani ya Msikiti mtukufu wa al-Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Wapalestina 20 waliuawa shahidi na makumi ya wengine kujeruhiwa. Mauaji ya Wapalestina yaliyofanywa na utawala ghasibu wa Israel tena ndani ya Msikiti wa al-Aqsa, kwa mara nyingine tena yalilipua ghadhabu za fikra za walio wengi duniani dhidi ya utawala huo katili. Hata hivyo kama kawaida uungaji mkono wa Marekani kwa Israel ulizuia kuchukuliwa hatua zozote za kivitendo dhidi ya utawala huo.
Miaka 13 iliyopita katika siku kama ya leo, mtetemeko mkubwa wa ardhi uliokuwa na ukubwa wa 7.8 kwa kipimo cha Rishta uliyakumba maeneo ya kaskazini mashariki mwa Pakistan. Kitovu cha mtetemeko huo kilikuwa katika mji wa Muzaffarabad. Watu wapatao 90 elfu walipoteza maisha yao na wengine milioni 3 na laki 6 kubaki bila makazi kufuatia mtetemeko huo.