Jumapili, Oktoba 14, 2018 Miladia
Leo ni Jumapili tarehe 4 Mfunguo Tano Swafar mwaka 1440 Hijiria, inayosadifiana na tarehe 14 Oktoba mwaka 2018 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 204 iliyopita, mkutano wa kihistoria wa Vienna ulifanyika kwa lengo la kujadili “Ulaya baada ya Napoleon Bonaparte”. Baada ya kujiuzulu na kubaidishwa Bonaparte mwezi Aprili mwaka 1814, mkutano wa kihistoria wa Vienna ulianza kufanyika katika siku kama ya leo katika mji mkuu wa Austria Vienna ili kuchukua maamuzi kuhusu ardhi zilizokaliwa kwa mabavu na Ufaransa katika kipindi cha vita vya Bonaparte. Wakati wa kuendelea mkutano huo, Napoleone Bonaparte alikimbia kutoka mahala alipokuwa amebaidishiwa na mwishoni mwa mwezi Februari mwaka 1815 kwa mara nyingine tena akashika hatamu za uongozi kwa muda mfupi, kipindi ambacho kiliondokea kuwa mashuhuri kwa jina la “Utawala wa Siku 100”. Aliposhika tena hatamu za uongozi alijianda kuwashambulia maadui zake.
Siku kama ya leo miaka 85 iliyopita, kwa amri ya Adolf Hitler Kansela wa wakati huo wa Ujerumani, nchi hiyo ilijitoa katika Jumuiya ya Kimataifa. Kuingia madarakani Adolf Hitler akiwa Kansela wa Ujerumani kulikuwa kumepelekea kuzuka wasiwasi mkubwa katika kila kona ya Ulaya kutokana na mipango yake ya kijeshi. Baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia na kutiwa saini mkataba wa amani wa Warsaw ambao ulidhibiti sana zana za kijeshi za Ujerumani, Hitler na viongozi wengine wa Kinazi walikasirishwa mno na hatua hiyo.
Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, Wazayuni wa Israel walivamia kijiji cha Qibya kilichoko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kufanya jinai kubwa za kutisha. Katika mashambulizi na uvamizi ulioendelea katika kijiji hicho kwa muda wa siku mbili, Wazayuni walitekeleza mauaji na ukatili mkubwa dhidi ya raia wa Kipalestina wasio na hatia. Mbali na Wazayuni hao kuwaua na kuwajeruhi kwa umati raia wa Kipalestina zaidi ya 42, askari wa Israel waliokuwa wakiongozwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Israel, Ariel Sharon, walibomoa makumi ya nyumba na shule za kijiji hicho. Mauaji hayo ya halaiki ni miongoni mwa mifano ya ugaidi wa utawala ghasibu wa Israel hususan wa Waziri Mkuu wa zamani wa utawala huo, Ariel Sharon.
Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, yaani tarehe 14 Oktoba mwaka 1964 Nikita Khrushchev Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomonisti cha Umoja wa Sovieti aliuzuliwa kutoka katika wadhifa wake huo. Nikita Khrushchev alifanikiwa kuwa mwanachama wa ofisi ya kisiasa ya Chama cha Kikomonisti mwaka 1939 na baada ya kufariki dunia Joseph Stalin mwaka 1953, Nikita alijitokeza kuwa shakhsia aliyekuwa na nguvu katika umoja wa Sovieti na kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomonisti na baadaye Waziri Mkuu wa shirikisho hilo.
Siku kama ya leo miaka 23 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 89 Ayatullah Muhammad Baqir Muhsini Malayeri, faqihi mkubwa wa Iran. Ayatullah Malayeri aliyekuwa mashuhuri katika hawza ya kielimu ya mjini Qum, Iran alizaliwa mjini Najaf, Iraq na katika familia ya kielimu, hapo mwaka 1285 Hijiria Shamsia. Akiwa kijana mdogo alielekea mjini Malayer, ambao ni makao makuu ya mkoa wa Hamadan nchini hapa akiwa pamoja na baba yake na baada ya kuhitimu masomo ya msingi alielekea mjini Mash'had kwa ajili ya kuendelea na masomo ya hawza. Wakati wa kuasisiwa hawza ya kielimu ya Qum, Ayatullah Muhammad Baqir Muhsini Malayeri naye alielekea mji huo na kupata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo akiwemo Abdul-Karim Haeri Yazdi na Seyyed Hussein Borujerdi na kufikia daraja za juu za kielimu. Aidha Ayatullah Malayeri alitambuliwa kwa uchaji-Mungu mkubwa katika zama zake.
Na siku kama ya leo miaka 19 iliyopita alifariki dunia kiongozi wa zamani wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anayejuliakana pia kama Baba wa Taifa. Nyerere alizaliwa mjini Butiama mkoani Mara mwaka 1922. Mwaka 1955 aliingia katika ulingo wa siasa akiongoza chama cha Tanganyika Africa Nation Union (TANU). Mwaka 1961 Nyerere alikuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika na mwaka mmoja baadaye akawa Rais wa nchi hiyo. Kutokana na juhudi zake mwaka 1964 Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kuunda nchi moja ya Tanzania. Nyerere aliendelea kuongoza nchi hiyo hadi mwaka 1985 ambapo aliachia hatamu za uongozi. Hata hivyo Nyerere aliendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Tanzania hadi alipofariki dunia. Nyerere analaumiwa kwa siasa yake ya kiujamaa ambayo inalaumiwa kuchelewesha maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania. Pia kuna makundi ya Waislamu Tanzania yanayomtuhumu kwamba, aliendesha kwa siri vita dhidi ya dini yao na kupendelea Wakristo katika utoaji wa elimu na madaraka. Aidha baadhi ya Wazanzibar wanamtuhumu Nyerere kwamba alimhadaa aliyekuwa Rais wa Zanzibar Mzee Abeid Amaan Karume kwa kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar na kuanza kupora taratibu mamlaka ya Zanzibar.