Oct 20, 2018 01:06 UTC
  • Jumamosi, 20 Oktoba, 2018

Leo ni Jumamosi tarehe 10 Mfunguo Tano Safar 1440 Hijria, mwafaka na tarehe 20 Oktoba 2018 Miladia.

Katika siku kama ya leo miaka 191 iliyopita, vita vya majini vya Navarino au The Battle of Navarino vilitokea katika ghuba ndogo ya Navarino kwenye bahari ya Mediterranean. Katika vita hivyo, meli za kivita za Uingereza, Russia na Ufaransa zilizishambulia meli za kivita za utawala wa Othmania kwa lengo la kuihami Ugiriki. Vita hivyo vilifikia tamati kwa kushindwa vibaya utawala wa Othmania.***

vita vya majini vya Navarino

Siku kama ya leo miaka 177 iliyopita, Mulla Jaafar Shariatmadar Tehrani mwandishi na msomi mkubwa wa Kiislamu aliaga dunia mjini Tehran Iran. Shariatmadar Tehrani alizaliwa 1197 Hijria Qamaria na aliitumia sehemu kubwa ya ujana wake kwa ajili ya kusoma na kutafuta elimu. Wakati mji wa Karbala Iraq unazingirwa na Daud Pasha kamanda wa Kiothmaniya, Shariatmadar Tehrani alirejea nchini Iran. Mbali na kuwa mahiri katika taaluma ya ukadhi, Mullah Jaafar Shariatmadar alibobea pia katika fasihi ya lugha ya Kiarabu na utunzi wa mashairi. ***

Mulla Jaafar Shariatmadar Tehrani

Miaka 159 iliyopita, katika siku kama ya leo,  alizaliwa John Dewey, msomi na mwandishi mashuhuri wa Marekani. Dewey alikuwa amebobea mno katika elimu ya malezi na alijifunza mengi alipokuwa katika Chuo Kikuu cha Columbia. John Dewey alifanikiwa kuandika vitabu vingi kuhusiana na malezi na makuzi ya mtoto. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya msomi huyo ni pamoja na "How We Think", "The Public and its Problems" na "Freedom and Culture" John Dewey alifariki dunia mwaka 1962 akiwa na umri wa miaka 92. ***

John Dewey

Siku kama yya leo miaka 71 iliyopita, muundo na rangi ya bendera ya Umoja wa Mataifa ulipasishwa. Baada ya kuasisiwa Umoja wa Mataifa kulizuka mjadala wa namna bendera ya umoja huo itakavyokuwa.  Hatimaye katika siku kama ya leo yaani Oktoba 20 mwaka 1947 uamuzi kuhusiana na jinsi muundo na rangi za bendera ya Umoja wa Mataifa zitakavyokuwa ukapasishwa. ***

Umoja wa Mataifa

Katika siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, Jomo Kenyatta mwanaharakati, mwanasiasa na mpigania uhuru mashuhuri barani Afrika na Rais wa Kwanza wa Kenya alitiwa mbaroni kufuatia amri ya utawala wa kikoloni nchini Kenya. Mzee Kenyatta alikuwa miongoni mwa watu 100 mashuhuri nchini humo waliotiwa mbaroni katika kipindi cha masaa 24 ikiwa ni katika fremu ya mpango wa kuibana Mau Mau, kundi la wapiganaji wa Kenya waliokuwa wakiupinga utawala wa kikoloni wa Waingereza. Wakenya huadhimisha siku hii kama Sikukuu ya Mashujaa na kuwakumbuka wale wote waliopigania uhuru wa taifa hilo. ***

Mzee Jomo Kenyatta

Na katika siku kama ya leo miakka 7 iliyopita, kiongozi wa zamani wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi alikamatwa na wanamapinduzi karibu na mji wa bandari wa Sirte kaskazini mwa nchi hiyo na kuuawa. Gaddafi aliuawa baada ya miezi kadhaa ya mapigano na wanamapinduzi ambapo jeshi lake liliwaua maelfu ya wananchi hususan katika miji ya Benghazi na Tripoli. Gaddafi ambaye aliitawala Libya kwa zaidi ya miaka 42 alizaliwa mwaka 1942. Aliingia madarakani mwaka 1969 kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani mfalme Mohammad Idris al-Sanusi. ***

Kanali Muammar Gaddafi