Jumanne tarehe 23 Oktoba 2018
Leo ni Jumanne tarehe 13 Safar 1440 Hijria sawa na tarehe 23 Oktoba 2018.
Siku kama ya leo miaka 1137 iliyopita alifariki dunia mtaalamu wa hadithi wa Kiislamu Abu Abdulrahman Ahmad bin Shuaib Nasai, maarufu kwa jina la Sheikhul Islam. Nasai alizaliwa mwaka 220 Hijria katika mojawapo ya vijiji vya Khorasan huko kaskazini mwa Iran na akaelea nchini Misri akiwa kijana. Huko alipata elimu ya fiqhi na hadithi na akaanza kufunza taaluma hizo. Baadaye Sheikhul Islam Nasai aliekele Damascus, Syria ambako alibainisha sifa na maadili ya watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Aali zake) na kupigwa mara kadhaa na wapinzani wa Ahlul Bait. Hatimaye alielekea Hijaz na kuishi mjini Makka. Nasai ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha "Khasaisu Amirul Muuminina Ali" na kile cha "Sunanun Nasai" ambacho ni miongoni mwa vitabu mashuhuri vya hadithi vya Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 1070 iliyopita alifariki dunia mtaalamu wa fasihi, fiqhi na tafsiri ya Qurani Muhammad Azhari Harawi. Alizaliwa mwaka 282 Hijria katika eneo la Harat nchini Afghanistan. Harawi alitekwa nyara na Waarabu wa jangwani akiwa safarini kuelekea Makka kwa ajili ya ibada ya hija na huko alijifunza lahaja asilia ya lugha ya Kiarabu ambayo aliitumia katika vitabu vyake. Mtaalamu huyo wa lugha ameandika vitabu vingi vya tafsiri na hadithi. Kitabu chake muhimu zaidi ni kile cha "Tahdhibul Lugha."

Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita, vita vya kihistoria vilivyopewa jina la al-Alamein vilitokea katika mji wenye jina kama hilo huko kaskazini mwa Misri kati ya wanajeshi wa Uingereza na jeshi la Manazi wa Ujerumani. Vita hivyo vilimalizika baada ya kushindwa jeshi la Ujerumani, japokuwa mapigano kati ya pande hizo mbili yaliendelea katika maeneo mengine ya kaskazini mwa Afrika. Amani kamili ilipatikana katika maeneo hayo baada ya kushindwa kikamilifu jeshi la Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.

Na miaka 41 iliyopita katika siku kama hii ya leo, Ayatullah Sayyid Mustafa Khomeini, mtoto wa Imam Ruhullah Khomeini (MA) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliuawa shahidi kufuatia njama ilizofanywa na askafi usalama wa utawala wa Shah akiwa nyumbani kwake huko Najaf, moja kati ya miji mitukufu ya Iraq. Al Haj Mustafa Khomeini alizaliwa mwaka 1309 Hijria shamsiya katika mji mtakatifu wa Qum na baadaye akajiunga na chuo cha elimu ya dini cha mji huo kwa ajili ya masomo ya juu baada ya kuhitimu elimu ya msingi. Alikuwa hodari mno na alifikia daraja ya juu ya kielimu ya Ijtihadi akiwa na umri wa miaka 27. Ayatullah Mustafa Khomeini alikuwa pamoja na baba yake Imam Khomeini katika kipindi chote cha mapambano dhidi ya utawala wa Shah.
