Jumapili, Oktoba 28, 2018
Leo ni Jumapili tarehe 18 Mfungo Tano Swafar 1440 Hijiria, sawa na tarehe 28 Oktoba 2018 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1403 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya wanahistoria, aliuawa shahidi Uways al Qarani, mmoja kati ya wafuasi waaminifu wa Mtume Mtukufu (saw) na Imam Ali bin Abi Twalib (as) katika vita vya Siffin. Uways Qarani aliishi katika eneo la Qaran lililoko Yemen na alikuwa mchamungu mkubwa. Licha ya kuwa na mapenzi makubwa kwa Mtume Mtukufu (saw), Uways Qarani hakubahatika kumuona mtukufu huyo, kwa kuwa kipindi hicho alikuwa akimuuguza mama yake aliyekuwa mgonjwa. Baada ya Mtume Mtukufu (saw) kufariki dunia, Uways Qarani alikuwa miongoni mwa wafuasi wa karibu wa Imam Ali (as). Shakhsia huyo akiwa pamoja na wapiganaji wengine katika jeshi la Imam Ali (as), alishiriki kikamilifu kwenye vita vya Siffin kati ya jeshi la Imam Ali na lile la Muawiya na akauawa shahidi katika vita hivyo.
Siku kama ya leo miaka 134 iliyopita alifariki dunia Mir Hussein Musawi Hindi, mmoja wa maulama wakubwa wa India. Alizaliwa mwaka 1246 Hijiria nchini India na kujifunza elimu ya fiqhi, hadithi, theolojia na elimu nyingine za kidini. Mir Hussein Musawi Hindi alitumia umri wake katika kutafuta elimu na kuandika vitabu. Athari muhimu zaidi za msomi huyo ni kitabu cha ‘Aqabaatul-Anwaar’ ‘Asfaarul-Anwaar’ na ‘Sham’ul-Majaalis’ pamoja na vitabu vingine.
Siku kama ya leo miaka 114 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Baaqir Kadhimi, mmoja wa maulama wakubwa wa elimu ya fiqhi wa nchini Iraq. Msomi huyo mashuhuri alizaliwa mwaka 1258 Hijiria mjini Kadhimiya, kaskazini mwa Iraq a kuanzia hapo masomo ya msingi. Katika kuendelea na masomo alielekea mjini Najaf na kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo kama vile Sheikh Answari na hatimaye akatokea kuwa mmoja wa maulama wakubwa wa elimu ya fiqhi mjini hapo. Miongoni mwa athari za Ayatullah Baaqir Kadhimi ni pamoja na kitabu cha ‘Miizanul-Haqq’ na ‘Rasaail fi Al-bay’i.’
Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita, wakati wa vita vya kwanza kati ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Waarabu, wanajeshi wa utawala huo waliwaua kwa umati wakazi wa kijiji cha al Dawayima huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Wazayuni hao walivamia msikiti wa kijiji hicho na kuwauwa shahidi Waislamu 75 raia wa Palestina waliokuwa wakisali. Vilevile waliwaua kwa umati watu wa familia 35 waliokuwa wamekimbilia hifadhi katika pango moja nje ya kijiji hicho. Askari jeshi wa utawala haramu wa Israel walikisawazisha na ardhi kijiji hicho baada ya kuwaua kwa umati wakazi wake wote.
Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, yaani sawa na tarehe 28 Oktoba mwaka 1962, ulihitimishwa mgogoro wa makombora wa Cuba baada ya kiongozi wa wakati huo wa Urusi, Nikita Khrushchev kuamuru kurejeshwa nyumbani meli zilizokuwa na makombora ya nyuklia. Hatua ya Urusi ya kujenga vituo kadhaa vya makombora ya nyuklia nchini Cuba katika umbali wa kilomita 90 kutoka Marekani ilizusha mgogoro mkubwa wa makombora uliokaribia kuitumbukiza dunia katika vita vya nyuklia. Wakati huo Marekani na Russia zilitishia kushambuliana kwa makombora ya nyuklia na kuzusha hofu kubwa hususan kwa watu wa Marekani, Russia na nchi za Ulaya. Hatimaye tarehe 28 Oktoba mwaka 1962 Nikita Khrushchev alitoa amri ya kurejea nchini meli zote zilizokuwa na makombora ya nyuklia na kufungwa vituo vya makombora vya Urusi nchini Cuba.
Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, alifariki dunia Taha Hussein mwandishi mahiri na stadi wa Kimsri. Alizaliwa mwaka 1889 katika moja ya vijiji vya Misri. Taha Hussein ambaye alikuwa mtoto wa saba katika familia yake, alipofuka na kupoteza uwezo wa kuona akiwa na umri wa miaka mitatu. Hata hivyo Mwenyezi Mungu alimjaalia kipaji cha hali ya juu. Taha Hussein alifanikiwa kuihafidhi Qur’ani yote katika kipindi kifupi. Akiwa na umri wa miaka 14 alifanikiwa kufaulu mtihani wa watahaniwa wa kuingia Chuo Kikuu cha al-Azhar na akiwa pamoja na kaka yake alijishughulisha na kusoma masomo ya dini pamoja na lugha za kigeni. Mwaka 1914 Taha Hussein alihitimu kwa alama nzuri na kutunukiwa shahada ya uzamivu yaani PhD. Wakati huo Chuo Kikuu cha Taifa cha Misri kilichukua uamuzi wa kuipeleka timu ya wahadhiri nchini Ufaransa kwa ajili ya kwenda kufundisha historia ya Mashariki. Akiwa ahuko alifunza lugha ya Kifaransa pamoja na histotia ya Ugiriki na Roma ya Kale pamoja na lugha ya Kigiriki. Mwaka 1959 mwandishi huyo mahiri wa Kimsri alinutukiwa tuzo ya Nobel kutokana na mchango wake katika uga wa fasihi ya lugha. Taha Hussein ameandika vitabu vingi na baadhi ya vitabu hivyo ni: A Man of Letters, The Days, The Suffers na Tree of Misery.
Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, Imam Ruhullah Khomeini alipinga vikali mpango wa Fahd kuhusu mapatano ya Palestina na Israel. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na baada ya kutiwa saini mkataba wa Camp David baina ya serikali ya Misri na utawala ghasibu wa Israel chini ya upatanishi wa Marekani, tawala vibara za Kiarabu zilifuata nyayo za utawala wa Misri katika suala hilo. Wakati huo Fahd bin Abdulaziz aliyekuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, alitoa pendekezo la kutambuliwa rasmi utawala vamizi wa Israel, suala ambalo lilikabiliwa na upinzani mkali wa Waislamu kote duniani. Kwa msingi huo katika siku kama hii ya leo Imam Ruhullah Khomeini alitoa hotuba akisema: "Ni wajibu kwetu sisi na kwa kila Mwislamu kupinga mpango kama ule uliopendekezwa na Fahd. Tunawajibika kulaani mipango kama hii isiyokuwa na faida kwa watu wanaodhulumiwa. Jambo hatari zaidi kwa sasa ni makubaliano ya Camp David na mpango wa Fahd ambao unaimarisha zaidi Israel na kudumisha jinai zake." Upinzani huo wa wazi wa Imam Khomeini na uungaji mkono wa Waislamu kote duniani kwa misimamo hiyo ya Imam ilikuwa sababu ya kukataliwa na kupingwa pendekezo hilo katika nchi nyingine.
Na siku kama ya leo miaka miwili iliopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Taqi Tabatabai Qumi mmoja wa Marajii Taklidi wa Kishia. Ayatullah Taqi Tabatabai Qumi ambaye ni mashuhuri zaidi kwa jina la Haji Agha Taqi Qumi alizaliwa mwaka 1301 Hijria Shamsia katika mji wa Mash’had. Baba yake ni Sayyid Hussein Tabatabai Qumi aliyekuwa mmoja wa Marajii wakubwa wa Taklidi ambaye kutokana na kupinga amri ya Reza Shah mfalme wa wakati huo wa Iran ya kuondolewa hijabu kwa nguvu, alilazimika kuhama Iran na kuelekea Iraq. Sayyid Taqi alisoma masomo ya awali na ya utangulizi kwa baba yake na alipoelekea Iraq alisoma kwa walimu mahiri wa zama hizo kama Sayyid Muhammad Hadi Milani, Sayyid Abdul-Hadi Shirazi, Hussein Hilli, Muhammad Kadhim Shirazi na wengineo.