Feb 03, 2016 09:10 UTC
  • Ufeministi, itikadi na misingi yake

Karibuni kuwa nasi katika sehemu ya kwanza ya mfululizo wa makala mpya zinazozungumzia na kukosoa ufeministi, itikadi na misingi yake kwa kutegemea mitazamo ya dini tukufu ya Kiislamu.

Maudhui ya wanawake, masuala na matatizo yao kama sehemu muhimu ya jamii, imekuwa ikijadiliwa na kuzungumziwa na wataalamu na wanafikra tangu miaka mingi iliyopita. Hali ya wanawake hususan mijadala inayohusu nafasi ya wanawake katika familia, kushirikishwa wanawake katika masuala ya jamii, mchango wao katika taasisi za umma na kadhalika ni miongoni mwa mambo ambayo siku zote yamekuwa yakijadiliwa na kuchunguzwa kwa njia tofauti kulingana na utamaduni unaotawala maeneo mbalimbali ya dunia. Katika uwanja huo kumetolewa mitazamo mbalimbali na fikra zinazopinga au kufanana na kukajitokeza mifumo ya kifikra yenye utaratibu na mpangilio maalumu. Miongoni mwa mifumo hiyo ni ule wa 'feminism' unaodai kutetea usawa na haki za wanawake.

Wanawake kama sehemu muhimu ya jamii, katika kipindi chote cha historia wamekumbwa na mashaka na matatizo mengi na kudhulumiwa sana. Wanawake katika kipindi cha kabla ya hali ya sasa inayoonekana kidhahiri tu kuwa nzuri na bora, kila mahala na katika vipindi vyote - isipokuwa katika kipindi cha Wahyi na ufunuo wa mbinguni ambapo alipewa nafasi yake inayostahili na kutambuliwa kama mwanadamu,- daima walikuwa wakitambuliwa kama nusu mwanadamu, kiumbe tegemezi na asiye na haki au mwenye haki za chini kabisa. Kwa mfano tu kabla ya kudhihiri Uislamu huko Bara Arabu na katika kipindi cha ujahilia wanawake walikuwa na nafasi duni na chini kabisa. Lakini baada ya kudhihiri dini hiyo mwanamke alipata shakshia na utambulisho wake halisi na kutokana na mafundisho ya Uislamu alipewa nafasi ya juu na anayostahiki.

Ni wazi kwamba kuthaminiwa mwanamke na kupewa utambulisho wake halisi ni kuthamini jamii na matabaka yote ya wanadamu. Mafundisho ya Uislamu yalimpa mwanamke nafasi ya juu na kupambana na itikadi potofu na hurafa zilizokuwa zikitawala jamii ya mwanadamu kuhusu kiumbe huyo. Hayo yote yalifanyika katika zama ambapo baadhi ya mifumo ya wanadamu na dini za kubuni zilikuwa zikimdunisha mwanamke na kumtambua kuwa ni kivuli tu cha mwanaume.

Katika suala hilo la kumdunisha mwanamke hakukuwepo tofauti baina ya mataifa yaliyokuwa yamestaarabika na yale jamii za kijadi na ambazo hazikustaarabika. Kwa mfano tu, katika historia ya Waarabu, mwanamke alikandamizwa na kudhulimiwa na alitambuliwa kama bidhaa inayorithiwa kama shamba na wanyama. Dhulma na ukandamizaji huo pia dhidi ya mwanamke vilionekana sana katika maeneo ya Magharibi mwa dunia. Ushahidi wa historia unaonesha kuwa, hali hiyo ilitokana na mambo mawili muhimu ambayo ni ujinga na ukatili. Ayatullah Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran anasema: Katika kipindi chote cha historia mwanamke alidhulumiwa katika jamii mbalimbali za wanadamu kutokana na ujinga na uhajihi. Kwa kawaida hivi ndivyo mwenye nguvu anavyomdhulumu na kumkandamiza dhaifu..", mwisho wa kunukuu..    >>

Ufeministi unaweza kutajwa kuwa ni radiamali au jibu na mwangwi uliotokana na ukandamizaji na vizuizi vingi vilivyowekwa dhidi ya mwanamke katika ulimwengu wa Magharibi. Mwangwi huo ulijitokeza kwa ajili ya kumfanya mwanamke athaminiwe. Fikra za kifeministi zilitokana na mitazamo ya wanafikra wa mifumo ya kisekurali, kiliberali na humanism na ilitegemea matakwa ya mtu, uhuru mutlaki na kutozingatiwa tofauti za kimaumbile na kimsingi baina ya mwanamke na mwanaume. Harakati hiyo iliyofurutu mipaka ambayo ilijitokeza kwa ajili eti ya kumkomboa mwanamke wa Kimagharibi ilisababisha dhulma nyingine mpya kwa jina la dhulma ya usawa dhidi ya mwanamke kutokana na mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupuuzwa tofauti za kidhati na kimaumbile baina ya mwanamke na mwanaume.

Kwa mujibu wa ripoti za weledi wa mambo na takwimu rasmi, hii leo nara na kaulimbiu zinazovutia za harakati hiyo kama ile ya kupigania usawa baina ya mwanamke na mwanaume, zimekuwa balaa kubwa kwa mwanamke. Dhulma hii mpya ya usawa ni mwendelezo wa dhulma ya siku nyingi lakini kwa sura mpya na tofauti na ile ya zamani. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei anasema katika uwanja huo kwamba: “Wamagharibi wanapaswa kujibu maswali mengi kuhusu jinsia ya mwanamke. Hakika wamefanya hiana dhidi ya mwanamke, na kile kinachotiliwa mkazo kwa sasa huko Magharibi ni ufuska na utovu wa maadili wa mwanamke”, mwisho wa kunukuu.    

Neno “feminism” katika lugha za Kiingereza, Kifaransa na Kijerumani limetokana na “feminine” lenye maana ya mwanamke au jinsia ya kike na limechukuliwa katika neno la kilatini la “femina”. Neno hilo lilitumiwa kwa mara ya kwanza na msoshalisti wa Ufaransa, Charles Fourier, katika karne ya 19 kwa shabaha ya kutetea harakati ya haki za wanawake. Kilugha neno feminism lina maana ya ‘ya kike’, ‘ujike’ au ‘hali ya kuwa mwanamke’. Hata hivyo tunapochunguza historia ya neno hilo na istilahi zake tunaona kuwa, haiwezekani neno hilo kuarifishwa na kulitolea maana kwa kiwango sawa kwa watu wote wanaojiita mafeministi. Ni vyema pia kukumbusha kwamba, neno hilo awali lilikuwa likitumiwa katika masuala ya tiba hususan kwa ajili ya kuashiria aina fulani ya matatizo na maradhi ya kijinsia ambayo yaliwadhihirisha wanaume kuwa na sifa za kike. Baadaye neno hilo lilipoteza maana yake ya kilugha na kuanza kutumiwa kwa ajili ya kuashiria harakati maalumu katika nusu ya kwanza ya karne ya 19 ambayo ilipata mabadiliko makhsusi na kuwa harakati ya wanawake iliyoanza kuchunguza masuala ya jinsia. 

Sababu za kujitokeza ufeministi zinaweza kuchunguzwa katika pande kadhaa. Tulisema kuwa uchunguzi wa kihistoria kuhusu nafasi ya mwanamke huko Magharibi na Ulaya unaonesha kuwa, watu wa jinsia hiyo walikumbwa na dhulma kubwa. Katika jamii za Magharibi mwanamke alitambuliwa kuwa ni kitu na bidhaa au sehemu ya mali na milki ya wanaume. Hata tunapotazama na kuchunguza mitazamo ya wataalamu wa Magharibi tunaona kuwa kila mmoja miongoni mwao alimtazama mwanamke kwa mujibu wa fikra zake na kumpa majina kama ‘jinsia ya pili’ ‘chanzo na sababu ya madhambi’ na majina mengine yaliyokuwa yakitolewa kwa ajili ya wanyama. Wanawake hawakutambuliwa kuwa ni wananchi. Hawakuwa na haki ya kupiga kura wala kushiriki katika masuala ya kijamii na kisiasa. Wakati huo huo hali ya wanawake katika nchi za Magharibi za kijadi ilikuwa mbaya sana. Walibaguliwa na kunyimwa haki zao za kimsingi. Baada ya mapinduzi ya viwanda kulijitokeza mabadiliko katika mitazamo na aidiolojia za Kimagharibi na baada ya hapo misingi ya kifikra ya Magharibi mpya ilijengeka kwa mujibu wa fikra za kisekulari, kiliberali na humanism.

Mbali na hayo mabadiliko ya mfumo wa ubepari na wimbi la ustawi wa viwanda huko katika nchi za Magharibi na vilevile kujitokeza tabaka la mabepari ni miongoni mwa mambo yaliyokuwa na taathira kubwa kwa wanawake. Kwani wanawake wa Magharibi ambao hadi wakati huo hawakuwa na haki ya kumiliki na walikuwa sehemu ya mali na milki ya wanaume, baada tu ya kuenea mitazamo ya mfumo wa kibepari na umiliki wa mtu binafsi walijielekeza zaidi katika mfumo huo, suala ambalo liliwaburuta zaidi kutoka majumbani kuelekea viwandani. Hata hivyo tabaka hilo la wanawake lilipata sulubu na mashaka makubwa kutokana na kazi ngumu na nzito za viwandani. Kwa utaratibu huo mfumo wa ubepari ulipata nguvu kazi kubwa tena ya bei rahisi japokuwa mwenendo huo pia ulibadilisha mtindo wa maisha wa wanawake wa Kimagharibi. Hatimaye dhulma hizo zote dhidi ya wanawake ikiwa ni pamoja na dhulma katika uwanja wa umiliki hadi kunyimwa haki ya kupiga kura na kutoa maoni vilikuwa mwanzo wa uchunguzi wa kifeministi kuhusu nafasi duni ya mwananmke.

Tags