Ufeministi, Itikadi na Misingi Yake (25)
Karibuni kuwa nasi tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki. Katika kipindi cha wiki iliyopita tuliashiria nafasi ya misingi ya ufeministi katika maazimio ya kimataifa yanayopiga marufuku ubaguzi dhidi ya wanawake na kusema kuwa, baadhi ya vipengee vya maazimio hayo vinapingana na sheria na mafundisho ya Uislamu. Kwa sababu hiyo nchi nyingi za Kiislamu na zisizo za Kiislamu hazikujiunga na maazimio hayo au zimejiunga lakini kwa masharti. Kipindi chetu leo kitaendelea kujadili maudhui hiyo.
Kama tulivyoashiria hapo awali azimio na mkataba wa kufuta ubaguzi dhidi ya wanawake umesisitiza mara kadhaa udharura wa kuondolewa kabisa aina zote za ukosefu wa usawa baina ya mwanamke na mwanaume. Kwa mujibu wa mkataba huo, aina yoyote ile ya ubaguzi dhidi ya mwanamke inapaswa kuondolewa na wanawake wanapaswa kuwa na haki sawa na wanaume. Mkataba huo unatambua hatua yoyote ya kuweka tofauti kwa mujibu wa jinsia ya mtu kuwa ni ubaguzi na unasisitiza udharura wa kupigwa vita hatua hiyo.
Hata hivyo ukweli ni kuwa, katika dunia ya Magharibi wanawake wamepatwa na madhara makubwa zaidi kutokana na nara na kaulimbiu hiyo ya usawa wa pande zote na katika kila kitu baina ya jinsia mbili. Kwani kwa kisingizio cha usawa, majumuku ya familia yamegawanywa baina ya mwanamke na mwanaume kwa kiwango sawa bila ya kutilia maanani sifa makhsusi za kinafsi, kimaumbile na kimwili za kila mmoja kati yao. Huu ni ukweli ambao baadhi ya wasomi na hata mafeministi wa kipindi cha baada ya usasa (postmodern) wamekiri na kuukubali. Wasomi hao wanasema kutekeleza sera ya usawa kamili baina ya mwanamke na mwanaume hakumuweki kila mmoja wao katika nafasi yake bali kitendo hicho chenyewe ni aina fulani ya dhulma na ukosefu wa uadilifu.
Mtazamo wa Uislamu kuhusu usawa baina ya mwanamke na mwanaume unatofautiana na ule wa kiliberali. Jambo linalotoa changamoto kwa Magharibi katika kutekeleza uadilifu baina ya mwanaume na mwanamke ni kuwatambua wawili hao kuwa ni sawa katika kila kitu na pande zote. Uislamu kwa upande wake umewatambua mwanaume na mwanamke kuwa ni sawa katika asli ya ubinadamu na matokeo yake ni kwamba wote wawili wana mazingira sawa ya kukwea na kupanda daraja za juu za ukamilifu wa kiroho, kielimu na kibinadamu. Hata hivyo kila mmoja kati ya mwanamke na mwanaume ana sifa makhsusi kwa kuzingatia nafasi na mchango wake tofauti katika mfumo wa maumbile. Kwa msingi huo wanatofautiana si katika upande wa kimwili na kimaumbile tu bali hata katika pande mbalimbali za kihisia, kiroho, kifikra na kimwenendo.
Ni vizuri kusisitiza hapa kuwa tofauti hizo za nafasi na nyadhifa za kila mmoja wao hazina maana ya mmoja wao kuwa bora kuliko mwingine, la hasha. Katika mtazamo wa Uislamu, tofauti hizo ni chanzo cha muungano na mfungamano baina ya jinsia hizo mbili. Mwanaume na mwanamke wanakamilishana kwa sababu haja ya kila upande ni sababu kuu ya mfungamano na mshikamano baina ya wanadamu na mwanamke na mwanaume pia hawako nje ya kanuni hii. Mtaalamu wa elimu nafsi wa Marekani, Dr. John Gray ameandika katika kitabu chake alichokipa jina la Men Are from Mars, Women Are from Venus kwamba: "Mpambano na mivutano baina ya mwanamke na mwanaume ilianza baada ya wawili hao kusahau tofauti zilizopo baina yao."
Kiongozi wa mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei anasema kuhusu tofauti zilizopo baina ya mwanamke na mwanaume kwamba: "Kuwa mwanamke ni thamani kubwa kwa mwanamke mwenyewe na asili na msingi. Kamwe mwanamke kufananishwa na mwanaume hakuwezi kutambuliwa kuwa ni thamani (Value) na jambo tukufu kama ambavyo si thamani wala jambo tukufu kwa mwanaume kufanana na mwanamke. Kila mmoja kati ya jinsia hizo mbili ana nafasi yake makhsusi, ana nafasi yake ya kimaumbile iliyopangwa na Mola Muumba na Mwenye hikima kwa makusudi na malengo ambayo lazima yatimizwe; hili ni jambo lenye umuhimu", mwisho wa kunukuu.
Pamoja na haya yote tunapaswa kuelewa kwamba wanawake katika dunia ya sasa ya Magharibi wanasumbuliwa na mashaka mengi ya ukosefu wa usawa na dhulma za chini kwa chini na za siri licha ya mlingano unaoonekana kidhahiri baina ya jinsia mbili. Ukosefu huo wa usawa na uadilifi umemdunisha na kudhalilisha mwanamke. Swali la kuuliza hapa ni kwamba je, katika azimio la usawa wa wanawake kumezungumziwa dhulma na ukosefu huo wa usawa wa batini na usioonekana kidhahiri?
Miongoni mwa matatizo ya azimio la kupiga vita ubaguzi dhidi ya wanawake ni kwamba azimio hilo limeifanya taasisi ya familia ikabiliwe na changamoto nyingi. Hapana shaka kuwa taasisi ya familia ni miongoni mwa misingi na nguzo za jamii na ina nafasi adhimu na muhimu sana. Hii leo fikra za humanism za mrengo unaotanguliza mbele matakwa na matamanio ya mwanadamu kuliko hata sheria za Mwenyezi Mungu ambazo zimekita mizizi katika familia za Magharibi na katika maazimio ya kimataifa, ni miongoni mwa sababu zilizodhoofisha na kuteteresha nguzo za familia. Fikra za humanism zinazotawala azimio la kupiga vita ubaguzi dhidi ya wanawake zimesisitiza sana suala la kujitegemea binafsi kwa mwanamke ndani ya taasisi ya familia. Vifungu kadhaa vya mada ya 16 vya azimio hilo vinapinga kabisa suala la kuwepo mudiri na kiongozi wa familia. Vilevile kifungu cha 4 cha mada ya 15 ya azimio hilo kinasema: Kila mmoja kati ya mke na mume ana uhuru wa kujichagulia mahala pa kuishi". Kwa utaratibu huo mume anaweza kuishi katika mji mmoja na mke wake akaishi peke yake katika mji mwingine.
Utekelezaji wa vifungu hivi katika nchi za Ulaya na Marekani umesababisha hali mbaya sana kwa familia kiasi kwamba baadhi ya wahakiki wa Ujerumani wanasema: Matokeo ya utafiti uliofanyika barani Ulaya yanaonesha kuwa, hii leo maisha ya unyumba ya mwanamke na mwanaume bila ya kufunga ndoa rasmi yamechukua nafasi ya ndoa rasmi na gharama za maisha, maskani na hali ya watoto huainishwa katika mapatano ya kijuujuu tu ya pande mbili...", mwisho wa kunukuu.
Tofauti na sisitizo la azimio la kupinga ubaguzi dhidi ya wanawake juu ya kujitawala kikamilifu mwanamke ndani ya familia, mafundisho na sheria za Uislamu sambamba na kulinda haki za mtu binafsi za wanachama wote wa familia, zimebuni kanuni pana na nyingi zinazowaunganisha pamoja na kujenga uhusiano na mfungamamano imara baina yao. Sheria hizo zinawaondoa mume na mke katika hali ya ubinafsi na kutojali maslahi ya mwenzake na kuwatambua kuwa kila mmoja wao anawajibika mbele ya maslahi na manufaa ya wanachama wote wa familia. Miongoni mwa sheria hizo tunaweza kuashiria sheria ya wajibu wa baba au mume kukimu mahitaji yote ya kimaisha ya mkewe na watoto wake, wajibu wa mume kutimiza matakwa ya ghariza za kujamiiana za mkewe na mke kutimiza za mumewe, wajibu wa mume kutoa mahari kwa mkewe, wajibu wa mke na mume kuimarisha misingi ya familia, ulazima wa kuchunga na kuheshimu sheria za eda baada ya kutalikiana na kanuni za kurejeleana, wajibu wa kuamrishana mema na kukatazana maovu ndani ya taasisi ya familia na kadhalika. Ni vyema kusema hapa kuwa kwa mujibu wa aya ya 6 ya Suratul Tahriim ya Qur'ani Tukufu inayosema: Enyi mlioamini! Zilindeni nafsi zenu na ahali zenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe...." ni kwamba wanachama wa familia wanawajibika kulinda uzima na usalama wa kimaadili na kiroho wa kila mwanachama wa familia husika.
Haya yote na mengine mengi mfuatiliaji wa kipindi hiki ni kielelezo cha mafundisho ya Uislamu yanayowaunganisha pamoja watu wa familia ambayo nguzo yake muhimu ni mke na mume na wala si kuwatenganisha na kumpa kila mmoja wao uhuru kamili wa kufanya alitakalo kwa kutumia visingizio mbalimbali. Katika mafundisho ya Uislamu watu wote wa familia wanawajibika mkabala wa wenzao na wana haki na majukumu ya kufanya kwa ajili ya kulinda na kuimarisha familia nzima. <<<< >>>>